StraightBook: Mwokozi wa wajasiriamali asiyefahamika

January 24, 2018 6:45 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Biashara yoyote kubwa au ndogo huitaji angalau taaluma kidogo ya uhasibu wakati wa kuiendesha ili kuifanya ikue vyema.

Miaka ya nyuma ilikuwa ni vigumu kwa mtu wa kawaida kutumia taaluma ya uhasibu lakini mbele ya mabadiliko ya teknolojia, kwa sasa kila kitu ni rahisi.

Kutumia fursa ya teknolojia, Bukhary  Kibonajoro(30) mwazilishi mwenza mfumo wa kihasibu wa StraightBook anasema walianzisha huduma hiyo ili kurahisisha uhasibu kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa.Katika mfumo huo, anasema mfanyabishara ataweza kujua mapato na matumizi au faida na hasara kwa haraka na urahisi zaidi bila kuwa na elimu kubwa ya taaluma ya uhasibu.

Mbali na kutohitaji elimu kubwa ya uhasibu, mfumo huo unatoa huduma zake kwa Kiswahili na Kiingereza ili kutoa fursa kwa wajasiriamali wote ndani na nje nchi.

Mfumo rafiki kwa wote

“Hata mfanyabishara mwenye elimu ya darasa la saba anaweza kutumia mfumo wetu ukilinganisha na hapo awali,” anasema Kibonajoro.

“Wafanyabiashara wanaweza kupata taarifa lukuki za kiuhasibu ambazo mhasibu wa kawaida ingemchukua muda mrefu kuziandaa,” anaongeza.

Watumiaji wa StraightBook ni wafanyabishara wote–wakubwa, kati na wadogo kutoka katika maduka ya dawa, ujenzi, umeme, vitabu, hoteli, viwanda, vituo vya mafuta, kampuni za mikopo, maduka ya nguo, mawakala, biashara ya jumla au rejareja.

Ili kutoa mwanya wa kupata taarifa muda wote, mtumiaji wa mfumo huo anaweza kupata taarifa popote walipo kwa kutumia kompyuta au simu zao za mkononi.

Kibanojaro anafanya kazi na ndugu zake wengine wadogo wawili kama waazilishi wenza ambao Suleman Kibonajoro (27) ,Muslim Kibonajoro (24)  pia katika umiliki huo wapo na Haji Rubibi  . Huku yeye akiwa ndiye mkurugezi mtendaji 

Kilichofanya waanzishe StraightBook

Kibonajoro anaeleza kuwa wazo la kuanzisha StraightBook lilitokana na kuona changamoto wanazokutana nazo wafanyabishara hapa nchini.

Kutokana na kuwa na sehemu kubwa ya wafanyabishara wasio rasmi, ni wachache wanaoweza kujua kiwango cha faida walichopata kutokana na kukosa elimu msingi ya uhasibu na ughali wa mifumo husika ya mahesabu.

 ‘’Mfumo wetu una lengo la kuona faida kwa urahisi kwa kudhibiti mali, stoku na mtaji kupitia ripoti zaidi ya 300 huku mfumo wenyewe ukikuandalia mahesabu yote bila kuhitaji nguvu na akili nyingi,” anasema Kibanojaro.

Tangu akiwa mwanafunzi wa Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Kompyta katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Kibanojaro anaeleza kuwa lengo lake lilikuwa ni kutatua changamoto katika jamii na anaona lengo limefikiwa baada ya kuasisi kampuni hiyo mwaka 2015.

                                  Bukhary   Kibonajoro mwazilishi mwenza wa  mfumo wa kihasibu wa StraightBook.

Kampuni yake ya Straightbook Limited inayomiliki mfumo wa Straightbook kwa sasa inahudumia wafanyabiashara zaidi ya 200 ambao wanahusisha aina mbili tofauti: wanaotumia program isiyotumia intaneti (desktop application) na wale wanaohitaji intaneti (online application).

“Mteja anayetumia huduma ya StraightBook online hutakiwa kujisajili na kulipia kwa mwezi Sh 20,000 kwa mtumiaji mmoja,” anasema Kibanojaro.  

Katika kuhakikisha kila mteja anapata kilicho na thamani ya fedha zake, anasema mtumiaji wa Desktop application anakuwa na nafasi tatu za kuweza kutumia mfumo huo ikiwemo ya kwanza malipo kwa mwezi Sh 25,000 kwa mtumiaji mmoja.

Watumiaji wa aina ya pili wanatakiwa kulipia Sh500,000 kama gharama za ufungaji kwa miaka yote lakini atawajibika kulipa Sh100,000 kila mwaka kwa mwaka unaofuta baada ya kufungiwa mfumo huo.

Mkurugezi mkuu huyo anasema mbali na mfumo huo kuwasaidia wajasiriamali wengi pia amefanikiwa   kushinda tuzo mbalimbali ndani ya miaka miwili ikiwemo ile aliyoipata kwenye shindano lililokuwa likiandaliwa na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi. Fedha alizopata katika shindano kiasi cha Sh10 milioni ndizo alizotumia kama mtaji. 

Bukhary Kibonajoro  mwazilishi mwenza wa  mfumo wa kihasibu wa StraightBook wa kwanza kushoto akipokea zawadi kutoka kwa Mweyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Reginald Mengi.   

Vilevile amewahi kuwa mshindi wa Tuzo maarufu za Tony Elumelu Entrepreneurship Program (TEEP) zinazotolewa na mfanyabishara maarufu Afrika na huko Nigeria Tony Elumelu mwaka 2015.

Pamoja na kuwa StraightBook imeanza kusimika mizizi yake nchini, bado watahitaji kupambana katika ubunifu kutokana na kuwepo washindani wenzao kutoka Tanzania wakiwemo Duka Pro, Mini Shop na Mauzo Sheet.

Kampuni hiyo yenye maskani yake katika jengo la DTBI yaliyopo ndani ya Ofisi za Tume ya Sayansi wanaeleza kuwa wapinzani wao hawawezi kwakuwa bidhaa yao bado ni bora sana sokoni.

Mbali na mfumo huo wa kihasibu, kampuni hiyo changa ya StraightBook Limited  pia imefanikiwa kutengeneza mfumo wa kuhibiti dawa kwenye hospitali za Serikali uitwao OKOA.

Okoa iliyoanza kufanya kazi katika Mkoa wa Kigoma chini ya ufadhili wa DLI, unawasaidia wakazi wa eneo hilo kuangalia uwepo wa dawa na hali ya foleni katika hospitali za Serikali kupitia tovuti ya www.okoa.co.tz kabla ya kwenda ili kuepusha kukosa dawa au foleni.

Baada ya kuingia katika tovuti hiyo, mtumiaji anatakiwa kutembelea www.okoa.co.tz hapo atabonyeza   ‘Niende Kituo Gani?’

Pamoja na kuanzisha mifumo hiyo miwili, bado StraightBook inakabiliana na changamoto lukuki ikiwemo uelewa mdogo wa Watanzania juu ya huduma zinazorahisishwa na Tehama na uhaba wa mtaji kuisukuma biashara katika ngazi ya juu.

Enable Notifications OK No thanks