Yanayofahamika, yasiyofahamika kuhusu app ya Vsomo

February 1, 2018 4:51 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

  • Ni program ya simu ya mkononi inayotoa kozi fupi za ufundi za Veta.
  • Unaweza kujifunza hadi kutengeneza simu za mkononi lakini ni watu wachache wanaifahamu.
  • Watu takriban 10,000 tayari wameshajisajili kati ya 34,000 walioipakua.
  • Imebainika wengi bado hawajaifahamu app hiyo.
  • Menejimenti huenda ikalazimika kubadilisha mfumo wa malipo na kuruhusu watumiaji wa mitandao mingine kupata maarifa hayo.


Dar Es Salaam. Julai mwaka huu, VSomo, programu ya simu inayotoa kozi fupi za mafunzo ya ufundi kupitia simu ya mkononi, itakuwa ikitimiza miaka miwili tangu kuanzishwa kwake ikilenga kuongeza wigo wa upatikanaji maarifa nchini.

Miezi 18 sasa baada ya kuanzishwa, Vsomo tayari imeshapakuliwa mara takriban 34,000 kwa wakati wote huku watu takriban 10,000 wakijisajili, kwa mujibu wa takwimu za menejimenti ya Vsomo.

Hata wakati Mamlaka ya elimu ya ufundi nchini (Veta) na Airtel walioanzisha Vsomo wakifurahia safari hiyo, bado huduma hiyo ya kibunifu haijawafikia vijana wengi wanaohaha kutafuta ujuzi ili wajiajiri au kuajiriwa kukabiliana na changamoto ya maisha.

Pamoja na kwamba Vsomo ni moja ya programu chache za kibunifu nchini zinazolenga kuongeza ujuzi miongoni vya vijana hasa wakati nchi ikijikita kuwekeza katika uchumi wa viwanda, ni wachache wanafahamu umuhimu wa program hiyo.

Vsomo ilibuniwa na mjasiliamali wa teknolojia Geofrey Magila ambaye ni moja ya wajasiliamali walioingia kwenye orodha ya vijana 30 mabilionea wajao wenye chini ya miaka 30 Afrika kwa mwaka 2017.

“Hadi sasa waliomaliza kozi hiyo ni watu 91 kutoka mikoa mbalimbali nchini na tayari baadhi wameshafungua biashara zao,” anasema Charles Mapuli, Mratibu wa Mradi wa Vsomo.

Mratibu wa mradi wa Vsomo, Charles Mapuli akieleza mafanikio na changamoto ya app ya Vsomo hivi karibuni. Picha na Nukta.


Inafanyaje kazi?

Vsomo inatoa mafunzo ya kozi fupi za ufundi za Veta za wiki nane ndani ya kipindi kifupi tu kisichozidi wiki nne kwa kutumia simu ya mkononi. Msomaji anatakiwa kupakua app hiyo kutoka kwenye Play store kwa wanaotumia simu za Android na kisha kujisajili kwa kutumia laini ya simu ya Airtel. Vsomo ina mpango wa kuweka app kwenye App Store kwa wanaotumia simu au tablet zinazotumia mfumo wa iOS wa Apple.

Sifa kubwa anayejiunga na kozi hiyo ni uwezo wa kusoma na kuandika na awe na uhakika wa kuipata simu janja (smartphone) wakati wote ili kumsaidia kujifunza nadharia ambayo sehemu kubwa ni maandishi na picha.

Kwa anayejisajili anaweza kuona tu kozi zilizopo na maudhui yake bila kuweza kusoma kozi yenye mpaka atakapolipia ada ya Sh120,000 kupitia Airtel Money ambayo inajumuisha hadi gharama za mafunzo kwa vitendo.

Wastani wa ada ya kozi fupi zinazotolewa na Veta kwa mujibu wa Mapuli ni kati ya Sh250,000 hadi Sh320,000 kwa kozi hivyo kufanya Vsomo kuwa nafuu zaidi ya mara mbili ya gharama ya kawaida.

Wanafunzi wa ufundi wakifanya majaribio ya kazi zao. Vsomo inatoa fursa ya wiki mbili kujifunza kwa vitendo kwa yule aliyemaliza masomo ya nadharia kupitia simu ya mkononi. Picha kwa hisani ya Vsomo.

Mwanafunzi anayesoma kupitia Vsomo atasoma nadharia ya kozi husika na kufanya mitihani yote na kufanya miadi katika chuo cha Veta kilichopo jirani kwa ajili ya kufanya mafunzo ya vitendo kwa saa 60 ndani ya wiki mbili.

“   Mtu anayesoma kupitia Vsomo anakuwa na uhuru na muda wake na anapunguza gharama za masomo. Ukiamua kusoma kwa siku mbili au mwezi au miezi mitatu sawa tu ilimradi mitihani yote ufaulu,” anasema Mapuli.

Uhuru huo, kwa mujibu wa Mapuli ndiyo unaowafanya hata watu waliopo shuleni au kazini wasome mafunzo ya ufundi kuongeza ujuzi wa kujiongezea kipato.

Kuna kozi 13 katika app hiyo ambazo hutolewa na Veta nchini zikiwemo ufundi umeme wa majumbani, umeme wa viwanda, ufundi wa simu za mkononi, urembo na upishi.


Mchakato wa kudhibiti ubora

Ili kukabiliana na udanganyifu katika mafunzo hayo, Mapuli anasema kuwa kabla ya mwanafunzi kufanya mafunzo ya vitendo karibu na chuo cha Veta cha karibu hutakiwa kufanya mtihani wa ana kwa ana ambao utajumuisha pia maswali ambayo aliyowahi kuyafanya kupitia simu ya mkononi.

“Akifaulu mtihani huo na kwa kutumia taarifa muhimu tulizonazo wakati wa usajili tutajua ni yule aliyejisajili kwenye app,” anasema.

Mwanafunzi anayemaliza katika mafunzo hayo hupewa cheti sawa kabisa na yule aliyesoma kozi fupi ya wiki nane katika chuo chochote cha Veta nchini.

Mapuli anasema wahitimu wa kozi hizo wanatambulika na mamlaka zote nchini zikiwemo Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (Ewura), Shirika la ugavi wa umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa nishati vijijini (Rea) na nyinginezo.

“Hii ni fursa kwa mafundi waliokuwa wakikosa ajira kwa kuwa hawana vyeti kwa kuwa wanaosoma kozi hizi kwenye Vsomo wanatambulika,” anasema.

Mafundi simu ni miongoni mwa watu wanaoweza kujipatia ujuzi zaidi kupitia programu ya Vsomo na kutambulika na mamlaka za udhibiti. Picha na Mtandao.

Pamoja na urahisi wa kujifunza, baadhi ya mambo katika app hiyo huenda yamefanya baadhi ya Watanzania wapakue kwa wingi na baadaye wakashindwa kuisoma.

Mlima wa changamoto

Moja ya changamoto ambazo Nukta imebaini huenda zimechangia Vsomo kutonufaisha wengi ni malipo ya Sh120,000 kwa mkupuo wakati wa kuanza, kuamuru laini yaAirtel pekee itumike kujisajili na ukosefu wa matangazo ya kutosha hasa kwa vijana waishio vijijini.

Hadi sasa zaidi ya theluthi mbili ya waliopakua app hiyo hawajajisajili na ni wachache waliomaliza kozi hiyo.

Mapuli anasema wanatarajia angalau wafikishe wahitimu 500 ifikapo Juni mwaka huu ikiwa ni ongezeko la wanafunzi wapya zaidi ya 400.

Uzoefu unaonyesha kuwa miradi mizuri kama hiyo mingi hushindwa kuwanufaisha wengi kutokana na kushindwa kutatua changamoto ndogondogo zinazojitokeza kadiri watu wanavyotumia huduma husika.

Hata hivyo, Mapuli anasema ili kuvutia vijana wengi zaidi katika mafunzo hayo, wamepanga kuongeza kozi mpya za usafi, upishi wa keki na upishi wa mikate na vitafunwa vingine.

Anasema baada ya kufanya utafiti walibaini kuwa asilimia 80 (watu nane kwa kila 10) ya waliojisajili na Vsomo hawana uwezo wa kulipia Sh120,000 kwa mara moja.

“Hivyo, Airtel na Veta tumeainisha kuwa tutafungua mfumo wa malipo ya awamu. Tutaangalia walipe nusu au mara tatu ila kwa sasa tunalifanyia kazi hili,” anaeleza Mapuli.

Mbali na malipo, anasema wameshajadiliana na Airtel kuhusu namna ya kuruhusu watumiaji wa mitandao mingine kusoma kozi hizo na wanatarajia hadi Juni jambo hilo liwe limetatuliwa.

Vsomo ni sehemu ya mradi wa huduma za jamii wa Airtel kwa kushirikiana na Veta ili kuwapa fursa zaidi vijana kupata ujuzi.


Enable Notifications OK No thanks