Maboresho mapya ya WhatsApp Business kurahisisha biashara za mtandaoni

Joshua Stephen 0245Hrs   Septemba 21, 2023 Teknolojia

  • Wafanyabiashara watathibitsha akaunti zao bure 
  • Hautahitaji kukatisha chat kuagiza na kulipia bidhaa
  • Wafanyabiashara watoa maoni mchanganyiko


Dar es Salaam. Kampuni ya Meta inatarajia kufanya maboresho mapya katika mtandao wa ‘Whatsapp Business’ utakaorahisisha shughuli mbalimbali za ufanyaji biashara mtandaoni ikiwemo uagizaji bidhaa.

Mtandao huo wa kijamii ulioanzishwa mwaka 2018 umejipatia umaarufu kutokana na uwezo wake wa kuunganisha wafanyabiashara na wateja kwa njia ya mtandao.

Taarifa iliyotolewa jana (Septemba 20, 2023) na blogu ya mtandao huo inasema hivi karibuni watumiaji wake watakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja pasi na kuumiza kichwa kwani taarifa zote za bidhaa, bei na jinsi ya kufanya malipo zitapatikana katika ‘chat’ ya muuzaji.

Hii inamaanisha wakati unawasiliana na muuzaji katika uwanja wa kutuma ujumbe kwenye  mtandao huo utaweza kujihudumia kwa kutazama bidhaa na mpangilio wa bei.

Awali ilikuwa mteja akihitaji bidhaa alilazimika kwenda kwenye wasifu (profile) wa akaunti husika ili kuona na kuagiza bidhaa anazohitaji jambo lilokuwa linapoteza muda na kukatisha mtiririko wa mazungumzo kati ya mteja na muuzaji.

Hivi sasa mambo yote yatamalizika wakati unapiga soga (chatting) na muuzaji ambapo pia unaweza kufanya malipo papo hapo bila kuhamia kwenye program tumizi au njia nyingine zinazotumika kufanya malipo.


Zinazohusiana


Weka miadi bila jasho

Maboresho mapya ya Whatsapp Business yatarahisha mchakato wa kuweka miadi (appointment) na mteja au watoa huduma mbalimbali kupitia 'chatting' itakayowezesha kuchagua muda na siku ya miadi.

Maboresho haya yatawasaidia watoa huduma wenye idadi kubwa ya wafuasi na wateja ambao wakati mwingine wanashindwa kupata huduma kutokana na kutingwa na shughuli nyingi.

Thibitishwa bila malipo

Kwa wale wanaopenda kuthibitishwa katika mitandao ya kijamii (Verification tick) hapa ndio penyewe, maboresho mapya yatafanya biashara yako ipate tiki ya buluu bila malipo.

Meta imefanya maboresho haya kutokana na kuongezeka kwa wimbi la akaunti feki zenye lengo la kutapeli au kughushi uhalisia na kujipatia wateja kinyume na utaratibu.

Mfanyabiashara akisasisha (update) akaunti yake ataweza kutengeneza ukurasa wa Whatsapp Business utakaoweza kupatikana kiurahisi katika tovuti maarufu kama Google na Safari. Pia akaunti yake itaweza kutumiwa katika simu zaidi ya moja hatua itakayorahisha mawasiliano na wateja.

“Tunafuraha kuendelea kutengeza vipengele bora kwa biashara …tunatarajia kusikia jinsi masasisho haya mapya yanavyosaidia kujenga mahusiano na kufanya mengi zaidi,” imeongeza blogu ya Whatsapp.

Maboresho mapya ya Whatsapp business yatamuwezesha mteja kuona bidhaa na kulipia kwa urahisi.Picha|Whatsap blog.

Wafanyabiashara watoa maoni mchanganyiko

Sara Shayo, Mkurugenzi wa kampuni ya uuzaji wa nguo (SB) ameiambia Nukta Habari kuwa maboresho hayo yatasaidia wafanyabiashara wenye wateja wengi kama yeye kuwahudumia wateja kwa haraka

“Maboresho hayo yatasaidia sana, unakuta wakati mwingine uko ‘busy’ na mteja anataka kuuliza kuhusu huduma unakuwa unapishana na gari la mshahara,”amesema Shayo.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wanasema maboresho hayo hayana msaada mdogo kwa baadhi ya biashara kama za matukio na sherehe kutokana na aina ya wateja kutopenda kupiga soga muda mwingi.

“Sioni kama maboresho hayo yatanifaa kwa kuwa wateja hawapendi kuchat sana, pia binafsi ninapendelea kupiga simu kwa mteja ninae wasiliana nae kwa mara ya kwanza… 

…Biashara yangu inategemea sana idadi ya watu, maeneo shughuli inapofanyika pamoja na aina ya shughuli.” anasema Celestine Moshi, mratibu wa vipindi na matukio kutoka MC Stine Events.

Related Post