Michael Tumaini: Mwanafunzi wa shule ya kata aliyetengeneza ‘AC’, Power Bank ya simu

Daniel Mwingira 2352Hrs   Januari 16, 2018 Teknolojia

  • Ameshatengeneza AC ndogo ya mezani inayotumia umeme sawa na simu.
  • Ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Sekondari ya Juhudi jiji Dar es Salaam.
  • Anatafuta msaada wa kusomeshwa nje ya nchi masuala ya maroboti.


Dar es Salaam. Baada ya kufunga safari hadi katika Kituo cha kukuzia kampuni changa cha Buni Hub kilichopo katika jengo la Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) jijini hapa, ndani ya chumba kidogo cha ubunifu mwanafunzi wa miaka 15, Michael Tumaini ametingwa akitengeneza ndege ndogo isiyokuwa na rubani (drone).

Katika chumba hicho kilichokuwa na watu wawili, Michael anajaribu kufufua ndege iliyokufa muda mrefu sasa.

Kijana huyo mdogo aliyeingia kidato cha tatu mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya kata ya Juhudi ni mmoja kati ya  wachache ambao  wamepewa nafasi ya kujifunza ili kukuza kipaji chake cha ubunifu wa teknololojia katika kituo hicho maarufu nchini.

Ukiachana na Drone niliyomkuta akihangaika nayo kuifufua, Michael ameshajaribu miradi mingine kwa kutumia vifaa vya elektroniki vilivyotumika ikiwemo benki ya kuchajia simu janja (smart phone) maarufu kama ‘Power Bank.’

Power bank hiyo iliyoundwa kwa kutumia betri ya Drone iliyotumika, ina uwezo wa kuchaji simu kama zilivyo nyingine zilizotengenezwa na kampuni kubwa kama sumsang na nyinginezo licha ya kuwa haifungwa katika kifungashio kizuri.

Abuni Power Bank 

“Mpaka sasa nimeshatengeneza Power Bank tatu ambazo zinatumia betri ya drone; moja nilipoteza darasani nyingine nilimpa rafiki yangu anayoitumia mpaka sasa hivi na ya mwisho naitumia mwenyewe,” anasema Michael katika mahojiano na Nukta hivi karibuni.

Ubunifu wa Michael ni kielelezo kingine cha matunda ya shule za kata katika uboreshwaji wa elimu nchini licha ya kuwa zinakabiliwa na changamoto lukuki za miundombinu ya masomo ya Sayansi na teknolojia.

Mwanafunzi huyo wa Shule ya sekondari ya Juhudi iliyopo Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, anasema Power Bank yake ipo salama kwa sababu umeme wake ni unaoingia na kutoka ni mdogo usiozidi volti 5.1.

“Volti 5.1 ni umeme mdogo sana huwezi kusababisha madhara kama ya kulipuka kama wengine wanavyodhani. Power Bank hii ina uwezo wa kuchaji simu hata mbili ndani ya saa moja na nusu,’’ anasema Michael kwa kujiamini.

Kujiridhisha na uwezo wa Michael, tulimchukua na kumpeleka eneo tofauti na Buni Hub na kumtaka aanze kuunganisha upya Power Bank nyingine jambo ambalo alilifanya ndani ya muda mfupi na iliweza kuchaji simu aina ya Samsung Galaxy A3.

Baadhi ya watumiaji wa Power bank anazotengeneza Michael akiwemo mwalimu wake Denis Lipiki wanaeleza kuwa zinafanya kazi vizuri licha ya mapungufu ya kutofungwa vyema kama zinazotengenezwa viwandani.

Mwalimu Lipiki anasema Power bank hiyo huwa anaitumia yeye na marafiki zake bila wasiwasi wowote wakati wakicheza mpira wa kikapu.

"Power bank hii huwa msaada mkubwa sana kwani huwa tunaitumia sehemu ambayo hatuna uwezo kupata chaji kwa njia ya umeme wa kawaida kwa hiyo ubunifu wa Michael umekuwa mkombozi kwetu,”anasema Mwalimu Lipiki.

“Michael ana uwezo mkubwa katika ugunduzi na huwa na mpa moyo na kumrekebisha pale anapokosea na hata muda mweingine kumpeleka kwa walimu wengine wa Phizikia na hesabu ili wamsaidie,”anasema.


Eti nini, AC ya mezani?

Mbali na Power bank, Michael ametengeneza kiyoyozi kidogo (Air Conditioner(AC) ambacho anasema alipata wazo hilo baada ya kusikia joto darasani. Baada ya hali hiyo, aliamua kujifunza kwanza kuhusu AC na mfumo wake uliopelekea kutengeneza AC hiyo ndogo.

"Nilitengeneza AC ndogo ambayo mtu unaweza kuiweka hata katika meza kwa sababu ya joto linalopelekea wanafunzi wengi kusinzia darasani wakati wa masoma.

“AC yangu ni ya kipekee kwa sababu inaweza kutumia umeme mdogo sawa na wa simu ambao huwa natoa kwenye Power bank niliyotengeneza mwenyewe,’’anasema Michael.


AC au Kiyoyozi cha mezani alichobuni Michael kwa kutumia vifaa vinavyotokana na taka za kielektroniki.  AC hii inatumia kiwango cha umeme sawa na ule unatoumiwa na simu ya mkononi. Picha na Daniel Mwingira.

Michael ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto wa Mzee Tumaini Michael, pia ametengeneza ndege inayoongozwa kwa rimoti marufuu kama ‘’RC plane’’ ambayo anaimalizia kwa sasa ili kuanza majaribio.

Iwapo mradi huo utakamilika, Michael anategemea akiendelezwa ndege hiyo itatumika kama sehemu ya michezo ya watoto ya kielektroniki.

Sambamba na hilo ametengeneza vitu vingine kama miwani ya kutazama uhalisia maarufu kwa Kiingereza kama Virtual Reality (VR) ambayo unaweza kuangalia michezo maarufu ya kielektroniki (games) na kuangalia filamu. Matumizi ya miwani hiyo humfanya mtazamaji ajihisi ni mshiriki wa filamu au game husika.


Moja ya VR zilizotengenezwa na Michael zinavyoonekana. Picha na Daniel Mwingira.

Ana ndoto ya kutengeneza miwani ya VR ya bei nafuu

"VR ametengeneza kwa kutumia vifaa vya kawaida kama maboksi na kuifanya iwe ya gharama nafuu ukilinganisha VR za madukani ambazo ni gharama sana,’’anasema Michael.

Miwani aliyotengeneza Michael kwa sasa anaitumia mwenyewe lakini anasema anaweza kutengeneza mingi zaidi ya hiyo iwapo atapata vifaa vya kisasa zaidi badala ya kutumia makopo ya maji na maboksi.

Kijana huyo, anayeomba kupewa msaada wa kusomeshwa nje ya nchi masuala ya utengenezaji roboti, anawashukuru wazazi wake kwa kumpa ushirikiano mkubwa katika kutimiza ndoto zake mpaka sasa katika masuala ya ugunduzi.

Anasisitiza kuwa hata kabla ya kwenda Buni Hub baba yake alikuwa anamletea vifaa vya kumsaidia kutengeneza pamoja na mama yake.

Hata hivyo, tofauti na wengi wanavyokifiri kuwa siku moja angekuwa Mhandisi, Michael anasema ndoto yake ya pili baada ya ubuifu wa masuala ya kielektroniki ni kuwa Daktari bingwa wa Upasuaji.

Alipoulizwa kilichomsukuma, Michael anasema alishawishiwa na mjomba wake ambaye ni fundi wa vifaa vya elektroniki na kipindi cha televisheni cha chaneli ya Discover Family cha “What could person go wrong”.


Michael akiangalia michezo maarufu ya kielektroniki (games) kutumia VR aliyoitengeneza.


Wamtabiria makubwa

Baadhi ya watu wanamfuatilia kwa karibu Michael, wanasema kuwa kijana huyo ana kipaji kikubwa lakini hapati msaada unaohitajika ili afanikiwe zaidi.

“Shule anayosoma Michael haina uwezo wa kumuwezesha kufanikiwa zaidi katika kipaji chake. Huyu hatakiwi kubaki kwenye shule za kawaida inabidi apelekwe kwenye shule za ufundi au vyuo vya ufundi ili awe bora zaidi,” anasema Sisty Basil, Mratibu wa taasisi ya Energy Change Lab inayojishughulisha na masuala ya ubunifu wa nishati rafiki nchini.

Basil anasema mbali na shule, Michael anatakiwa kusimamiwa vizuri katika mawazo yake kwa kuwa huwa anatamani kufanya kila kitu kila tu anapopata wazo jambo ambalo siyo zuri.

“Miradi anayobuni mingi inalenga kusaidia jamii ikiwemo kwenye sekta ya nishati tatizo hapati msaada unaohitajika. Tunao mpango wa kumtafutia mshauri wa kazi zake tunasubiri tu fedha zitufikie ili kumuwezesha mambo makubwa,” anasema Basil.


Related Post