Tanzania yasaka Sh8 trilioni kukamilisha mradi SGR
- Fedha hizo zitawezesha ujenzi wa vipande vitatu kutoka Makutupora hadi Kigoma.
Dar es Salaam. Tanzania inatafuta fedha zaidi ya Sh8 trilioni kukamilisha ujenzi wa vipande vitatu vya Reli ya Kisasa (SGR) ikiwa ni moja ya mambo yanayoendelea kuipa presha ya kifedha Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Fedha hizo zitasaidia kujenga sehemu za mtandao wa reli hiyo ya kisasa kuanzia Makutopora hadi Mwanza na Kipande cha kuanzia Tabora – Kigoma hadi Malagarasi. Awamu ya kwanza ya mtandao wa reli ya SGR ina urefu wa kilomita 1,219 ikianzia Bandari ya Dar es Salaam hadi jijini Mwanza.
Katika jitihada za kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amefanya ziara katika nchi ya Hispania na kufanya majadiliano na kampuni ya Wakala wa Bima wa nchi hiyo (ECA) na kujadili uwezekano wa kupata fedha hizo.
Taarifa kutoka wizara hiyo iliyotolewa leo (Septemba 21, 2023) inabainisha kuwa Hispania imeonyesha nia ya kushiriki kufanikisha upatikanaji wa kiasi hicho cha fedha.
Soma zaidi
Katika taarifa hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii nchini Hispania, Xiana Mendez amesema nchi hiyo inatambua umuhimu wa mradi huo kwa Tanzania kwa kuwa kukamilika kwake kutaongeza mnyororo wa thamani wa uwekezaji na biashara na kuwa Kituo cha biashara katika Ukanda wa Afrika.
Mendez amefanya mazungumzo na Dk Nchemba ikiwa ni miongoni mwa jitihada za kuzisaka fedha hizo.
“Ushiriki wa ECA katika kutekeleza mradi huu wa kimkakati ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na kwa ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu kati ya Hispania na Tanzania, na kwa maendeleo ya wananchi kwa ujumla” amesema Dkt. Nchemba leo Septemba 21, 2023.
Mradi wa SGR ni muhimu miongoni mwa miradi muhimu nchini kutokana na kuwa lango la biashara kwa nchi saba za ukanda wa Afrika na maziwa makuu zisizopakana na bahari na utakapokamilika utachochea shughuli za biashara, usafiri na usafirishaji mizigo na kuongeza pato la Taifa.
Katika kuimarisha uhusiano na maandalizi ya kutekeleza ufadhili huo wa SGR, Dk Nchemba amesema mkandarasi ametafuta kampuni 12 za Kihispania zitakazosambaza vifaa vitakavyotumika kujenga reli hiyo.
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara, na Utalii wa Hispania, Bi. Xiana Mendez, kwenye picha ya pamoja na Waziri waa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba baada ya kukutana na kufanya mazungumzo mjini Madrid, Hispania.Picha|Wizara ya Fedha.
Sanjari na kuwepo kampuni hizo, waziri huyo amemuomba Mendez na serikali yake kwa ujumla, kuzishawishi kampuni nyingi za Hispania kujitokeza kushiriki katika ujenzi wa mradi huo.
Mradi huo umegawanyika katika awamu mbili, ya kwanza ni ile inayoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na ya pili ni kuanzia Tabora hadi Kigoma ambapo kukamilika kwake kunatarajia kugharimu zaidi ya Sh23 trillioni.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa, awamu zote za mradi huo zinaendelea kwa kasi ambapo mpaka kufikia Agosti 26, 2023 kipande cha kwanza cha Dar es Salaam mpaka Morogoro kimefikia asilimia 99, Morogoro mpaka Makutupora kimefikia asilimia 95.
Kwa upande wa awamu ya pili ya ujenzi wa reli hiyo inayoanzia Tabora mpaka Kigoma yenye urefu wa kilometa 506 hatua za awali za ujenzi bado zinaendelea.