Si kweli : Taasisi ya Mohamed Dewji Foundation haitoi mikopo

Daniel Mwingira 0950Hrs   Agosti 17, 2023 NuktaFakti
  • Taasisi ya Mohemed Dewji hutoa ufadhili wa elimu, upatikanaji wa maji na utatuzi wa changamoto za afya.
  • Video iliyoambatanishwa na taarifa za utoaji mikopo si halisi, imehaririwa.

Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa mtandao wa Facebook huenda umewahi kukutana na chapisho linalohusu fursa ya mikopo kutoka kwenye taasisi ya mfanyabiashara bilionea nchini Tanzania Mohamed Dewji Foundation

Sehemu ya chapisho hilo lianasomeka β€˜π‰πˆππ€π“πˆπ„ 𝐌𝐊𝐎𝐏𝐎 πŠπ”π“πŽπŠπ€ πŒπŽπ‡π€πŒπ„πƒ πƒπ„π–π‰πˆ π…πŽπ”ππƒπ€π“πˆπŽπ kwa maelekezo ya kupata vigezo na masharti njoo hwatspp kwa noπŸ‘‰πŸΏ 0748923136’.

Chapisho hilo pamoja na kuhamasisha watu kuomba mikopo wametaja kigezo cha kutoa kwanza kiasi cha hisa ya mkopo unaotaka kupewa kabla ya kupata mkopo wenyewe.

Ufafanuzi zaidi wa taarifa hiyo unaonesha kama unahitaji kukopa Sh100,000 basi utalazimika kutoa kwanza hisa ya Sh22,000 ndipo upewe mkopo huo.

Taarifa hiyo imesambaa katika mtandao wa Facebook kupitia akaunti zenye majina tofauti tofauti toka mwaka 2022  huku ikiwa imeambatanishwa na  video fupi inayomnukuu Mohamed Dewji kuwa anatoa mikopo.

Hata hivyo, Habari hiyo haina ukweli wowote kwa kuwa ni habari za uzushi zinazotumiwa na matapeli kuwalaghai wananchi na kujipatia vipato kwa njia zisizo halali. 

​

Masharti ya kupata mkopo kama yalivyoainishwa kwenye chapisho hilo.PichalFacebook


Soma zaidi


Tulichokibaini

Nukta Fakti imefanya utafiti ili kubaini ukweli wa akaunti hizo za mtandao wa Facebook na kugundua kuwa akaunti hizo hazina uhusiano wowote na Mohamed Dewji mwenyewe au taasisi yake ya Mohamed Dewji Foundation.

Akaunti sahihi ya Facebook ya mfanyabiashara huyo maarufu nchini ni Mohammed Dewji huku ile ya taasisi yake ni Mo Dewji Foundation na sio Mikopo Tanzania kama inavyojitambulisha akaunti hiyo inayodai kutoa mikopo.

Mohamed Dewji hatoi mikopo

Utafiti zaidi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa, si Mohamed Dewji mwenyewe wala taasisi yake ambayo inajihusisha na utoaji wa mikopo kwa namna yoyote ile.

Kupitia mtandao wa Linkedin Mohamed Dewji amewahi kutoa taarifa kwa umma akifafanua kuwa taasisi yake inajihusisha zaidi kutoa misaada ya kielimu kwa kufadhili masomo, upatikanaji wa maji pamoja na kutatua changamoto katika sekta ya afya.

β€˜Ninapenda kutoa tamko rasmi kwamba, mimi Mohammed Dewji, na taasisi yangu ya Mo Dewji Foundation, hatutoi mikopo na wala hatujihusishi na taasisi za kukopesha,” anasikika Dewji kwenye video hiyo.

Dewji aliwataka watu kuwa makini na taasisi au kikundi ambacho kitadai kinatia mikopo kwa kujihusianisha na taasisi yake.

Video ilihaririwa (edited)

Baada ya kufanya uchunguzi zaidi kwa kutumia Google reverse image search, tumebaini video hiyo ya sekunde thelathini iliyo chapishwa kwenye akaunti ya Mikopo Tanzania  imehaririwa kutoka katika video halisi yenye dakika moja na sekunde thelathini na sita.

Video hiyo ilichukuliwa kutoka kwenye akaunti ya Mohamed Dewji ambapo kupitia video hiyo aliitambulisha taasisi yake pamoja na kutoa onyo kwa Watanzania kujihadhari na matapeli wanaodai kutoa mikopo kwa jina lake.

Related Post