Tamisemi yaomba kuidhinishiwa Sh10 trilioni mwaka wa fedha 2024-25

Sayuni Kisige 0857Hrs   Aprili 16, 2024 Habari
  • Bajeti yaongezeka kwa Sh981 bilioni.
  • Fedha ya miradi ya maendeleo yapungua kwa zaidi ya Sh70 bilioni.
  • Awaagiza wakuu wa mikoa kutekeleza vipaumbele saba ikiwemo ukusanyaji wa mapato.


Dar es Salaam. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeliomba Bunge liidhinishe Sh10.125 trilioni ambazo ni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Fedha hizo zimeongezeka kwa Sh981.1 bilioni ambapo kwa mwaka 2023/24 Tamisemi iliidhinishiwa na Bunge Sh9.144 trilioni.

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 leo Jumanne Aprili 16, 2024 bungeni jijini Dodoma, amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha hizo Sh6.709 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara na mengineyo.

“Mheshimiwa Spika, jumla ya Sh3.415 trilioni zinaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Sh2.269 trilioni ni fedha za ndani na  Sh1.145 trilioni ni fedha za nje,” amesema Mchengerwa.

Hata hivyo, bajeti ya maendeleo imepungua kwa zaidi ya Sh70 bilioni ambapo mwaka 2023/24 Bunge liliidhinisha kiasi cha Sh 3.485 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25.PichalPan African Visions

Vipaumbele saba vya wizara 

Aidha, Mchengerwa pia amebainisha vipaumbele saba vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo amewaagiza wakuu wa mikoa kuwasimamia wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa kuzingatia.

“Kuhakikisha ukusanyaji wa mapato uliolengwa unafikiwa kwa asilimia 100 ikiwemo ukusanyaji wa kodi za majengo, kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 na kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya afya ya msingi, elimu msingi na sekondari kulingana na mipango iliyowekwa,” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa ameongeza kuwa  vipaumbele vingine ni kuimarisha vyanzo vikuu vya mapato kwa ajili ya kuchachua uchumi kama ilivyobainishwa katika mpango na bajeti wa halmashauri husika.

Sambamba na hilo viongozi hao wa mikoa watatakiwa kujenga vituo vipya vya polisi katika kata 12 na kukamilisha ujenzi wa vituo vya polisi kata 77.

“Kukamilisha ujenzi wa ofisi za vijiji/mitaa angalau tano kwa kila halmashauri na kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga shule za maadilisho zitakazojengwa katika kila mkoa shule moja,” amesema Mchengerwa.

Related Post