Sh600 bilioni zaongezwa bajeti ya uchukuzi 2024-25, matumizi ya kawaida yakifekwa

Sayuni Kisige 0812Hrs   Mei 06, 2024 Habari
  • Serikali yaliomba Bunge kuidhinisha Sh2.73 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2024-25.
  • Prof Mbarawa aeleza kuwa wamepunguza matumizi ya kawaida kwa Sh3 bilioni.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imependekeza kuongeza bajeti ya wizara ya uchukuzi kwa zaidi ya Sh600 bilioni hadi Sh2.73 trilioni katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2024/25 huku zaidi asilimia 95 ikipangwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Ongezeko la bajeti hiyo muhimu katika sekta ya uchukuzi ni sawa na asilimia 31 ya bajeti ya wizara hiyo kutoka Sh2.09 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge katika mwaka wa fedha wa 2023/24 unaoishia Juni 30.

Katika hotuba yake ya bajeti, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa ameliambia Bunge leo Mei 6, 2024 kuwa Sh114.7 bilioni kati ya Sh2.73 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh2.61 trilioni ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.


Kwa mujibu wa Prof Mbarawa, robo tatu au Sh86.6 bilioni kati ya Sh114.7 bilioni ya fedha za matumizi ya kawaida zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi za wizara hiyo. Kiasi kingine kilichosalia cha Sh28.8 bilioni kitatumika kwa ajili ya matumizi mengineyo.

“Bajeti ya matumizi ya kawaida katika mwaka wa fedha 2024/25 imepungua kwa Sh3.4 bilioni sawa na asilimia 2.94 ukilinganisha na Sh118.2 bilioni iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024,” amesema waziri huyo.



Katika ugharamiaji wa bajeti ya sekta hiyo muhimu katika ukuzaji wa uchumi nchini, Prof Mbarawa amesema fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa zinajumuisha Sh2.52 trilioni fedha za ndani na Sh90.6 bilioni fedha za nje.

Uchambuzi zaidi wa bajeti hiyo unabainisha kuwa kati ya bajeti yote ya uchukuzi, Sh1.5 trilioni au asilimia 55 ya Sh2.73 trilioni imepangwa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) huku sehemu nyingine ya bajeti ya maendeleo ikipangwa kujenga viwanja vya ndege na miradi mingine ya taasisi za wizara hiyo. 

Prof Mbarawa amesema wizara yake imepanga kutekeleza vipaumbele mbalimbali ambavyo ni kuongeza ufanisi na ubunifu wa utendaji kazi utakao chochea kuboresha huduma za usafirishaji nchini kwa maendeleo ya uchumi.

Kipaumbele kingine ni kuongeza ufanisi na ubunifu katika kukusanya maduhuri katika vyanzo vilivyopo na kubaini vyanzo vipya vitakavyoongeza mapato pamoja na uboreshwaji wa huduma bora ili kukidhi matarajio ya wadau muhimu katika sekta ya uchukuzi wanaochangia mapato.

Licha ya Serikali kupendekeza kushusha fedha za matumizi ya kawaida, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeomba kuongeza fedha hizo kwa matumizi ya kawaida kwa namna inayoakisi kuongezeka kwa fedha za miradi ya maendeleo.

Related Post