Serikali ya Tanzania kutumia zaidi ya Sh1.9 trilioni wizara ya elimu

Esau Ng'umbi 0544Hrs   Mei 07, 2024 Habari
  • Zaidi ya nusu ya bajeti ya miradi ya maendeleo kutumika kugharamia mikopo ya elimu ya juu.
  • Kamati ya Bunge yaonya juu ya Serikali kutotoa fedha zilizoidhinishwa.
  • Yasema inaathiri utekelezaji wa baadhi ya shughuli za wizara.


Dar es Salaam. Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh1.965 trilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2024/25 huku zaidi ya nusu ya matumizi ya miradi ya maendeleo ikielekezwa kugharamia utoaji wa mikopo ya elimu ya juu nchini. 

Bajeti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda leo Mei 7, 2024 bungeni jijini Dodoma imeongezeka kwa Sh289 bilioni sawa na asilimia 17.2 kutoka Sh1.675 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2023/24. 

Prof Mkenda amesema kati ya Sh1.965 trilioni, theluthi mbili au Sh1.328 trilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo huku Sh637.29 bilioni ikipangwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya wizara hiyo. 

Kati ya fedha zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Serikali imepanga kutumia Sh585.23 bilioni kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi na kiasi cha Sh52.06 bilioni kilichosalia kitagharamia matumizi mengine. 

Prof Mkenda ameongeza kuwa kati ya fedha za maendeleo zilizoombwa Sh1.032 trilioni ni fedha za ndani ambazo asilimia 60 zitagharamia mikopo ya elimu ya juu.


Soma zaidi: Sh600 bilioni zaongezwa bajeti ya uchukuzi 2024-25, matumizi ya kawaida yakifekwa


Vipaumbele vitano vya wizara 2024/25

Kwa mujibu wa Prof Mkenda, kwa mwaka 2024/25 Serikali imeweka vipaumbele katika maeneo matano ikiwemo utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo, kuongeza fursa na uimarishaji ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (Amali na Amali Sanifu). 

Vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu pamoja na kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu pamoja na kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu.

Bajeti yaongezeka utoaji wa fedha si wa uhakika

Wakati bajeti ya wizara hiyo muhimu ikiongezeka kwa zaidi ya Sh289.57 bilioni ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2023/24, Serikali imepeleka theluthi mbili au asilimia 68 tu ya Sh1.675 trilioni iliyodhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2024.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Husna Sekiboko kutotolewa kwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa wakati kunaweza kuathiri utendaji baadhi wa shughuli za wizara.

“Hadi kufikia Februari 2024 kiasi cha fedha kilichopatikana kilifikia asilimia 68 ya kiasi kilichoidhinishwa, hata hivyo, upatikanaji wa fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida ulikuwa asilimia 46, ambayo ni pungufu ya nusu.

Hali hii ni ishara ya matumizi ya kawaida kutopatikana ipasavyo, kwa mwenendo huo utelekelezaji wa matumizi ya kawaida utakuwa umeathirika,” amebainisha Sekiboko.

Related Post