Wanafunzi 10,000 wa diploma Tanzania kupewa mikopo 2024-25

Mwandishi Wetu 1054Hrs   Mei 07, 2024 Habari
  • Wanufaika 2,000 zaidi kunufaika kutoka idadi ya mwaka wa fedha wa 2023/24. 
  • Ni kwa wanafunzi wa fani za  kipaumbele na zenye uhaba wa wataalam nchini ikiwamo fani sayansi na ufundi.
  • Kamati ya Bunge yashauri bajeti ya mikopo iongezwe kutoa fursa kwa wanafunzi wengi zaidi.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kuwapa mikopo wanafunzi 10,000 wa fani za kipaumbele wa vyuo vya kati ngazi ya diploma (stashahada) mwaka 2024/25 ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wake wa kuongeza fursa za mafunzo ya amali inayohusisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 25 ama wanafunzi 2,000 zaidi kutoka wanufaika 8,000 waliopangwa kupatiwa mikopo iliyogharimu Sh48 bilioni mwaka 2023/24 hatua inayoweza kutoa ahueni kwa wanafunzi wa ngazi hiyo ya elimu waliokuwa wanashindwa kumudu gharama za masomo.

Kwa mujibu wa muongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa stashahada uliotolewa na  Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) miongoni fani zinazopewa kipaumbele ni zile za ualimu wa Sayansi, Hisabati na Mafunzo ya  Amali, Usafiri na usafirishaji, Uhandisi na nishati, Madini na sayansi ya ardhi pamoja na Kozi ya kilimo na mifugo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda aliyekuwa akiwasilisha maombi ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma leo Mei 7, 2024 amewaambia wabunge kuwa pamoja na mikopo hiyo Serikali itadahili wanafunzi wapya wa ualimu wa mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza idadi ya walimu wa kada hiyo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo leo Mei 07, 2024 Bungeni jijini Dodoma. Takriban wanafunzi 10,000 wa vyuo vya kati wanatarajia kunufaika na mikopo ya elimu. Picha| Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia/Handouts.

“Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada takribani 10,000 katika fani za kipaumbele na zenye uhaba wa wataalam nchini ikiwamo fani sayansi na ufundi…

…Itadahili wanafunzi 2,089 katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro - MVTTC ili kuongeza idadi ya walimu wanaofundisha vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya ualimu wa mafunzo ya ufundi,” amesema Prof. Mkenda.

Hata hivyo, Waziri huyo hajaainisha ni kiasi gani mahususi kilichotengwa ka ajili ya mikopo ya stashahada kwa mwaka 2024/25 ingawa alibainisha kuwa asilimia 60 ya bajeti ya Sh1.328 ya miradi ya maendeleo iliyoombwa itatumika kugharamia mikopo ya elimu ya juu.

Wanafunzi wa elimu ya juu wakumbukwa

Neema ya ongezeko la wanufaika wa mikopo ya elimu halijaishia kwa wanafunzi wa stashahada peke yake.  Kwa mujibu wa Mkenda idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2024/25 imeongezeka kutoka 223,201 mwaka 2023/24 hadi 252,245.

Kati ya hao, wanafunzi 84,500 ni wa mwaka wa kwanza ambapo kwa shahada ya kwanza wanufaika watakuwa 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na wanufaika wa Skolashipu ya Samia 2,000. Wanafunzi wengine 157,745 ni wale wanaoendelea na masomo.

Kamati yataka bajeti HESLB iongezwe

Kutokana na ongezeko la majukumu kwa HESLB la kuanza kutoa mikopo kwa vyuo vya kati vya elimu, Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeitaka Serikali kuongeza bajeti ya mikopo ili iwafikie wanufaika wengi zaidi na kuleta ahueni kwa familia za kipato cha chini zisizomudu gharama za masomo ya vyuo vikuu au vya kati.

Aidha, kamati hiyo imeishauri HESLB kufanya mapitio ya vigezo vya kupata mikopo,  kutoa elimu ya kwa umma kuhusu mikopo ya elimu ya juu na kurahisisha michakato wa urejeshaji mikopo kwa watu walioko nje ya nchi.

Related Post