Usidanganywe: Kunywa maji mengi hakuui virusi vya Uviko-19

Daniel Samson 0549Hrs   Machi 09, 2023 NuktaFakti
  • Hakuna ushahidi wa kitabibu kuthibitisha madai hayo.
  • Chanjo ndiyo njia pekee ya kujikinga na ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Ni ukweli usiopingika kuwa maji ni muhimu kwa miili yetu kwa sababu husaidia kuimarisha kingamwili, mzunguko mzuri wa damu na kumkinga mtu na magonjwa nyemelezi.

Hata hivyo, unywaji wa maji mengi hasa kipindi hiki cha janga la Corona  (Uviko-19) hakusaidii kuua virusi vya ugonjwa huo kwa mtu aliyeambukizwa kama baadhi ya wanavyoamini. 

Mpaka sasa wataalam wa afya hawajathibitisha madai hayo kwa utafiti wa kisayansi kama ambavyo hakuna dawa ya ugonjwa huo bali mtu hutibiwa kulingana na dalili alizozionyesha. 

Pia baadhi huamini kuwa kunywa maji mengi hukifanya kirusi cha Uviko-19 kushuka kwenye tumbo ambapo kitaenda kubadilishwa na kuwa tindikali (acidic pH).

Hata hivyo, bado haijathibitishwa kama kirusi kinaweza kuwa hai kwenye tindikali. 

Inashauriwa kupata chanjo ya Uviko-19 ili kukabiliana na ugonjwa huo wakati wanasayansi, watafiti na watalaam wa afya wakiendelea kusugua vichwa kupata dawa ya ugonjwa huo ambao umegharimu maisha ya watu zaidi ya milioni 6 duniani.

Pia inashauriwa kuvaa barakoa hasa kwenye mikusanyiko ya watu wengi, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na kutumia kitakasa mikono.

Related Post