Wabunge wahoji ucheleweshaji malipo waliopisha upanuzi viwanja vya ndege

Sayuni Kisige 0904Hrs   Aprili 08, 2024 Habari
  • Ni pamoja na wananchi wa Nachingwea mkoani Lindi.
  • Serikali yasema watalipwa uhakiki ukikamilika. 


Dar es salaam. Kufuatia kuwepo kwa madai ya ucheleweshwaji wa malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo ikiwemo upanuzi wa kiwanja cha ndege cha  Nachingwea, Serikali imesema inaendelea kufuatilia kwa ukaribu suala hilo ili walipwe stahiki zao.

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ametoa ufafanuzi huo leo April 8, 2024 Bungeni jijini Dodoma akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Maimuna Pathan aliyetaka kujua mpango wa Serikali kulipa fidia kwa wananchi wa Nachingwea mkoani Lindi ambao hawajalipwa pesa zao kwa muda mrefu.

“Je, Serikali kwa kuchelewa kulipa pesa ya wananchi zaidi ya miaka mitano sasa, haioni kwamba imerudisha nyuma maendeleo ya wananchi hao kwa kukosa sehemu za kulima?” amehoji Pathan na kuomba thabiti ya Serikali ni lini wananchi wa Nachingwea watalipwa fedha zao.


Soma zaidi: Gumzo Bungeni: Magari ya Serikali kuwepo maeneo ya starehe


Naibu Waziri Kihenzile akijibu swali hilo amesema hatua ya awali ya kutambua fidia na mali zao imekamilika na kuidhinishwa na mthamini mkuu wa Serikali.

“Maombi hayo yamewasilishwa serikalini kwa ajili ya malipo. Aidha, Serikali inahakikisha kuwa wananchi wote waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa miradi mbalimbali wanalipwa fidia za stahiki,” amesema Kihenzile.

Uwanja wa ndege Nachingwea umekuwa na umuhimu mkubwa tu siyo kwa kusafirisha abiria bali kukuza shughuli za kiuchumi za Mkoa wa Lindi ikiwemo kilimo cha korosho na ufuta na uchimbaji wa madini.

“Tulifanya uhakiki kwa wale wananchi 116 awali ilikuwa tuwalipe Sh3.4 bilioni lakini baada ya kufanya uhakiki wa ongezeko la bei ya mazao tukapata Sh3.5 bilioni hii yote ni dhamira ya Serikali katika kuona kuwa wanachi wanakamilishiwa mradi wao,” ameongeza Kihenzile.

Mbali na hilo maeneo mengine ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Musoma amesema, Serikali ipo katika hatua za mwisho kwa Wizara ya Fedha na Mipango na mara itakapofanikisha hatua hizo wananchi watalipwa fedha zao.

“Serikali imefanya uhakiki kwa wananchi waliopunjwa malipo yao na kama kuna malalamiko mengine Serikali ipo tayari kuyapitia tena,” amesema. 

Related Post