Si kweli: wanafunzi wenye ufaulu chini ya GPA 3.8 hawaondolewi sifa ya kupata kazi

Lucy Samson 1015Hrs   Agosti 16, 2023 NuktaFakti
  • Wizara ya Elimu yasema taarifa hiyo sio ya kweli.
  • Vigezo vya elimu huangazwa na muajiri husika wakati wa maombi ya kazi.

Dar es Salaam. Huenda wanafunzi na wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu wakawa na hofu kubwa mara baada ya kusambaa kwa taarifa ya kuwa wanafunzi wenye ufaulu chini ya GPA ya 3.8 wataondolewa sifa za kupata ajira.

Taarifa hiyo inayosambaa katika mitandao ya kijamii imeiga mfano wa chapisho ‘poster’ zinazo chapishwa na chombo cha habari cha Jamii Forum ikiwa imenukuu sehemu ya maneno ya Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda.

Hata hivyo ondoa shaka, taarifa hizo hazina ukweli wowote, kwani Wizara ya Elimu imekanusha na Nukta Fakti imefanya uchunguzi kujiridhisha kuwa habari hiyo ni ya uongo.

Mapema hii leo Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia ukurasa wa mtandao wa Twitter wamekanusha madai hayo kwa kuchapisha taarifa hiyo na  kuongezea mhuri unaosomeka ‘FAKE’ wenye rangi nyekundu kuashiria habari hiyo ni ya kupuuzwa.




Hata hivyo, utafiti wa Nukta Fakti umebaini  mpaka sasa hakuna muongozo rasmi Tanzania unaozuia wahitimu wenye ufaulu fulani kukosa sifa za kuajiriwa.

Ingawa, kwa baadhi ya taasisi, Mashirika Umma au binafsi pamoja na baadhi ya kazi katika idara nyeti huhitaji kuwa na aina fulani ya vigezo ikiwemo cha ufaulu, ambavyo huwekwa wazi kwenye tangazo la kazi.


Zinazohusiana


Tulichobaini

Huenda taarifa hiyo ya uzushi ikawa imetengenezwa na watu wenye nia ya upotoshaji au kuzua taaruki kwa wahitimu wa elimu ya ngazi ya juu ambao kwa sasa wapo kwenye wimbi kubwa la kukosa ajira.

Julai 28, 2023 Waziri wa Elimu alitangaza azma ya Serikali kutoa ufadhili kwa wahitimu wa Kidato cha Sita 640, ambao hawakutakiwa kushuka ufaulu wa GPA ya 3.6, taarifa iliyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Jamii Forums

Uchunguzi zaidi wa Nukta Fakti  umebaini kuwa maandishi iliyotumika katika mstari wa mwisho wa ‘poster’ hiyo hayaendani na aina ya maandishi ya mistari ya juu au yale yanayotumiwa na chombo cha habari cha Jmiiforums.

Mpaka sasa katika mitandao ya kijamii inayomilikiwa na Jamii Forums hakuna chapisho lolote la kukanusha habari hiyo ambayo huenda imezua hofu au taharuki kwa baadhi ya watu.

Related Post