Nane nane inavyoweza kuchochea kuimarisha usalama wa chakula Tanzania, Africa

Joshua Stephen 0150Hrs   Agosti 04, 2023 Maoni & Uchambuzi
  • Ni kupitia kuwekeza katika kutoa maarifa ya mbinu bora za kilimo kwa wakulima
  • Usalama wa chakula utasaidia kuokoa zaidi ya watu milioni 51.3 wanaokabiliwa na upungufu katika nchi za Sadc 

Dar es Salaam. Kwa miongo minne na nusu sasa, Tanzania imekuwa ikiadhimisha sikukuu ya wakulima, maarufu kama maonesho ya Nane nane ikiwa na lengo la kutambua jitihada na mchango wa kundi hilo muhimu katika uchumi wa nchi.  

Sikukuu hizo awali ziliadhimishwa na kusherehekewa Julai 7 kila mwaka kisha mwaka 1977 zilibadilishwa siku, mwezi wa kuadhimisha pamoja na jina na kuwa Nane Nane ambapo Saba Saba ilibakia kuwa maonesho ya biashara kimataifa. 

Nane Nane iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1977 ili kuiongezea nguvu Sera ya Serikali ya wakati huo ya ‘Siasa ni Kilimo’,  ambapo wakulima katika wilaya, mkoa na kitaifa walionesha mazao yao, pembejeo za kisasa pamoja na kufundishwa namna ya kutumia pembejeo hizo.

Hata hivyo mwaka 2021, Serikali ilisitisha maadhimisho ya sherehe hizo, jambo lililokosolewa vikali na baadhi ya wadau wa kilimo, ndipo Serikali ikatangaza kurejesha tena mwaka 2022 na kuahidi yatakuwa na mfumo tofauti.

Kwa mwaka 2023 maadhimisho hayo yatakua na hadhi ya kimataifa kwa kuwa nchi 9 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajia kushiriki, pamoja na wadau mbali mbali wa sekta za umma, binafsi, taasisi za fedha na watunga sera. 

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mfumo wa chakula endelevu”. 

Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango akizindua maonesho ya kilimo 2023. PichalWizara ya Kilimo

Kauli mbiu hiyo inamulika sehemu ya janga linaloikabili dunia kwa sasa la uhaba na upungufu wa chakula katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Afrika ambayo ndio imeathirika zaidi huku mabadiliko ya tabia nchi pamoja na vita ya Urusi na Ukraine vikitajwa kama sababu.

Itakumbukwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua mkutano wa mabunge ya nchi za Sadc Julai 3, 2023 alitoa rai kwa nchi hizo kuanza kutekeleza sera za kilimo ili kuwaokoa raia milioni 51.3 wanaokabiliwa na upungufu wa chakula katika jumuiya hiyo.

"Watu wanaokabiliwa na upungufu wa chakula wameongezeka kwa asilimia 25.7 kwa mwaka mmoja hii haikubaliki…bado tuna kilomita za mraba milioni 9.8 zinazoweza kulilisha bara la Afrika na zaidi, ikiwa zitatumika ipasavyo,” alisema Rais Samia jijini Arusha.

Maonesho hayo yanaweza kutumika kama chachu ya kuimarisha na kuongeza  usalama wa chakula unaozikabili nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania ambayo imeripoti upungufu wa mazao ya chakula katika msimu wa mwaka 2021/22 kutoka tani milioni 18.7 hadi tani milioni 17.1

Ingawa Tanzania inajitosheleza kwa mahitaji ya chakula kwa asilimia 110, upungufu huo wa asilimia 8.1, unaathiri mikakati ya uwekezaji ya muda mrefu kwenye sekta ya kilimo ili kuhakikisha utoshelevu wa chakula na ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. 


Soma zaidi


Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo makadirio ya mahitaji ya chakula nchini Tanzania yanatarajiwa kufikia tani milioni 20 ifikapo mwaka 2030, kiasi ambacho huenda kisifikiwe kama Tanzania haitachukua hatua madhubuti kisera, kibajeti na katika utekelezaji.

Ili kuimarisha usalama kwenye eneo hili, maonesho ya Nane Nane yanaweza kutumika kama fursa ya kuwafundisha wakulima mbinu bora za kilimo, matumizi sahihi ya pembejeo na namna ya kufanya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kufanya kilimo tija.

Aidha, Serikali ni lazima kuendelea kuwekeza katika mifumo imara na himilivu ya kilimo inayotumia teknolojia za umwagiliaji za kisasa kwa kuwa Tanzania bado ipo nyuma katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji ambayo ingeweza kutoa matokeo chanya zaidi.

Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo mpaka mwaka 2023, ni  hekta 727,280.6 tu sawa na asilimia 2.5 ndizo ambazo zinatumika katika kilimo cha umwagiliaji.

Aidha, Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa Umwagiliaji ilikagua na kubaini miundombinu ya umwagiliaji katika skimu 137 ina matunzo hafifu ya miundombinu ya umwagiliaji.

Pamoja na Serikali kuongeza bajeti ya umwagiliaji kwa mwaka 2023/24 Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi wanachama wa Sadc kama Eswatini ambapo asilimia 95 ya hekta 90,000 zinazotumika kwenye kilimo nchini humo zinamwagiliwa. 

Wadau wa kilimo wanasemaje

Josephat Masanja ambaye ni mtaalamu na mshauri wa masuala ya kilimo nchini Tanzania ameiambia Nukta Habari kuwa maonesho ya Nane Nane yanaweza kuwa chachu ya kuimarisha usalama wa chakula ikiwa wakulima watapewa elimu ya njia bora za uzalishaji kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi.

Masanja ameongeza kuwa, maadhimisho hayo ni jukwaa mahususi kwa wakulima kupata mbegu bora, zana bora za kilimo pamoja na pembejeo bora kutoka kwa taasisi mbalimbali zilizowekeza kwenye kilimo hivyo ni nafasi nzuri kwao kujifunza na kwenda kuyafanyia kazi.

“Matumizi ya rasilimali ardhi, maji, na mbegu yanaendana na maarifa, wakulima wanapaswa kutumia fursa ya nane nane kupata elimu zaidi kuhusu kilimo, afya ya udongo, aina za mbegu, utunzaji wa vyanzo vya maji na matumizi bora ya pembejeo, wajikite kwenye kupata maarifa zaidi,” amesema Masanja.

Masanja amesisitiza kuwa matokeo ya wakulima kupata maarifa sahihi yatayowasaidia kuboresha mbinu na mikakati ya kilimo yataonekana kwenye uzalishaji ambao utaimarisha zaidi usalama wa chakula.


Mikakati ya Serikali

Sekta ya kilimo imeanza kuchechemuliwa upya na huenda ikawa na matokeo chanya kwani kwa miaka miwili mfululizo bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka ambapo kwa mwaka 2023/24 imefika zaidi ya Sh970 bilioni.

Kiwango cha fedha katika bajeti ya mwaka 2023/24 kimeongezeka kwa Sh219.6 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 29 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita ambapo asilimia 80 ya bajeti itatumika kwa shughuli za maendeleo.

Miongoni mwa vipaumbele katika bajeti iliyoanza Julai Mosi, 2023 ni kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 727,280  mwaka 2021/22 hadi hekta milioni 1.07 mwaka 2024/25 kwa miradi inayoendelea ambapo pia imetengwa Sh197.8 bilioni kwa ajili ya kuboresha kilimo cha umwagiliaji.

Hatua nyingine ambazo zinatarajiwa kuwa na mwitikio chanya ni pamoja na programu ya Jenga Kesho Bora (BBT) ambapo baadhi ya vijana wanapewa mafunzo ya kilimo na kisha kukabidhiwa mashamba.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Serikali inakusudia kuifanya sekta ya kilimo ichangie asilimia 30 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia 26.9 iliyoripotiwa mwaka 2020.

Umoja wa Mataifa kupitia programu yake ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, (SDG’s) inaainisha lengo lake la pili ni kuhakikisha hakuna njaa duniani ifikapo 2030.

Related Post