Kufa kufaana: Bei ya mahindi yapaa Tanzania

Mwandishi Wetu 0327Hrs   Mei 07, 2023 Biashara
  • Gunia la kilo 100 liliuzwa Sh119,484 mwaka unaoshia Machi 2023.
  • Bei hiyo imeongezeka kwa asilimia 48.9 ndani ya mwaka mmoja.
  • Bei za mazao mengine ya chakula nazo zapanda.

Dar es Salaam. Huenda Watanzania wakaendelea kutoboa mifuko yao zaidi baada ya bei ya mahindi kupanda kwa asilimia 48.9 hadi kufikia Sh119,484 mwaka unaoshia Machi 2023.

Mahindi ni sehemu ya mazao makuu ya chakula yanayotumiwa kwa wingi. Mazao mengine ni maharage, mtama, uwele na viazi.  

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya April 2023 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Machi 2022 ilikuwa Sh60,996 lakini imepanda hadi Sh119,484 Machi mwaka huu. 

Ni kawaida katika kama hiki ambacho wakulima wanakuwa katika msimu wa kilimo bei za mazao kupanda kwa sababu ya uchache wa mazao hayo sokoni. 

Kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kunawaumiza walaji kwa sababu wanalazimika kutoboa zaidi mifuko yao zaidi ili kupata zao hilo la chakula, wakati wakulima wananeemeka na bei hiyo.


Hata wakati bei ya mahindi ikipaa kwa asilimia 48.9 zaidi ya ile ya mwaka 2022, bei hiyo imekuwa ikipanda na kushuka tangu Januari mwaka huu.

Januari bei ya mahindi ilikuwa Sh115,852, mwezi uliofuata ikashuka hadi Sh114,762 kabla haijapanda hadi Sh119,484 Machi mwaka huu. 

Bei hiyo iliyotumika Machi 2023 ndiyo ya juu zaidi kuwahi kufikiwa mwaka mmoja uliopita unaoishia Machi.

Pia katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, karibu bei za mazao yote ya chakula zilipanda. Mathalan, mchele ulipanda kutoka Sh84,460  hadi Sh294,811 huku maharage hakipanda hadi Sh287,615 kutoka Sh186,497 ya Machi mwaka jana.   

Related Post