Bajeti ya Wizara ya Kilimo yaongezeka kwa asilimia 29

May 8, 2023 12:15 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Asilimia 84 ya bajeti kutekeleza miradi ya  maendeleo. 
  • Itaimarisha utafiti wa kilimo, uzalishaji wa mbegu, utoaji wa ruzuku na  kilimo cha umwagiliaji.
  • Wadau wasema fedha bado hazitoshi, wakiishauri Serikali kuanzisha somo la kilimo.

Dar es Salaam. Huenda sekta ya kilimo nchini Tanzania ikapata msukumo mpya kwa kuleta matokeo chanya kwenye uchumi na kuboresha hali ya maisha ya wakulima mara baada ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 kuongezeka kwa asilimia 29 huku asilimia 84 ikienda kwenye miradi ya maendeleo.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyekuwa akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 leo Mei 8, 2023 bungeni amewaomba Wabunge waidhinishe bajeti ya Sh970.7 bilioni kwa ajili ya wizara yake.

“Katika mwaka 2023/ 2024, Wizara ya Kilimo inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Sh970.7 bilioni kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24, kati ya hizo Sh767.83 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema Bashe jijini Dodoma.

Fedha hizo zilizoeleekezwa katika miradi ya maendeleo ni sawa na asilimia 84 ya bajeti yote, licha ya kuwa imeongezeka kwa asilimia tano tu. 

Kiwango cha fedha katika bajeti ya mwaka 2023/24 kimeongezeka kwa Sh219.6 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 29 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita.

Vipaumbele vya Wizara

Kwa mujibu wa Bashe, fedha hizo zinatarajiwa kutekeleza vipaumbele kadhaa ikiwamo kuimarisha utafiti wa kilimo, uzalishaji wa mbegu, utoaji wa ruzuku, kilimo cha umwagiliaji, miundombinu ya uhifadhi wa mazao, na huduma za ugani.

“Kipaumbele namba moja ni kuongeza tija na uzalishaji ambacho kitatekelezwa kwa kuwekeza kwenye maeneo ya kimkakati  ambayo ni utafiti wa mbegu bora, uzalishaji wa mbegu na miche bora pamoja na usambazaji wa mbegu na miche…,” amesema Bashe.

Bashe amebainisha kuwa wizara hiyo inakusudia kuongeza ajira zenye staha pamoja na ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo kwa kutekeleza mikakati kadhaa ikiwemo kuwawezesha vijana kupata ardhi, kuimarisha mradi wa jenga kesho bora, kuendeleza vituo mahiri vya kusambaza teknolojia na kuhamasisha uanzishaji wa kampuni za ugani za vijana. 


Soma zaidi


Vipaumbele vingine ni kuongeza usalama wa chakula na lishe ambapo Serikali inakusudia kufanya uwekezaji kwenye miundombinu ya uhifadhi kuweza kufikia uwezo wa kuhifadhi tani milioni tatu ifikapo mwaka 2030.

Hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza kiwango cha upotevu wa mazao baada ya kutoka shambani ambapo kwa sasa takribani asilimia 35 ya mazao hupotea kutokana na kuhifadhiwa katika njia zisizo sahihi.

Wizara ya kilimo kwa mwaka 2023/24 pia inakusudia  kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya mazao nje ya nchi, pamoja na kuboresha maendeleo ya ushirika.

Bajeti yaongezeka, fedha hazitoshi

Bajeti ya kilimo imeongezeka kwa mara ya pili mfululizo ambapo mwaka 2022/23 iliongezeka kwa Sh456.9 bilioni sawa na asilimia 155.3 ambapo kwa mara ya kwanza bajeti ya kilimo ilivuka Sh500 bilioni na kuibua matumaini mapya ya kuimarika kwa sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.

Pamoja na ongezeko hilo, bado bajeti hiyo ipo chini ya maazimio ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za  Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo yanataka kila mwanachama kutenga bajeti ya kilimo ambayo ni asilimia 10 ya bajeti yote ya Serikali. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo David Kihenzile  akisoma uchambuzi wa bajeti ya kilimo mwaka 2023/24. Picha | Bunge 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo David Kihenzile aliyekuwa akisoma uchambuzi wa bajeti hiyo amewaambia Wabunge kuwa bajeti ya kilimo ya mwaka ujao ni asilimia 2 ya bajeti Kuu ya Serikali ya Sh44.3 trilioni ya mwaka ujao kiwango hicho bado ni kidogo kwani ni ni sawa na asilimia 2 tu ya bajeti nzima.

“Kiwango kinachotakiwa kiuhalisia ni Sh2.2 trilioni hii ni kwa mujibu wa azimio la Maputo la mwaka 2002 na azimio la Malabo la mwaka 2014 ambapo kila nchi mwanachama wa SADC anapaswa kutenga asilimia 10 ya bajeti yake kama bajeti ya kilimo,” amesema Kihenzile.

Pamoja na kuishauri Serikali kuongeza kiwango cha bajeti ya Wizara ya Kilimo, Kihenzile ameishauri pia Serikali kufikisha pesa za miradi ya maendeleo kwa wakati ili itekelezwe ndani ya muda uliopangwa na kuleta tija kwa Taifa.

Kilimo liwe somo la lazima

Aidha, kamati hiyo imeishauri pia Serikali kuanzisha somo la kilimo kuanzia ngazi ya shule ya msingi ili kuwajengea vijana misingi bora ya kilimo na kuongeza ushiriki katika sekta hiyo ambayo ni uti wa mgongo wa Watanzania wengi.

“Kwa umuhimu wa sekta ya kilimo, kamati inaishauri Serikali kuanzisha somo la kilimo kama somo la lazima kuanzia ngazi ya msingi ili kuwajengea vijana wa kitanzania uwezo wa kukielewa na kushiriki kikamilifu katika sekta na kuongeza ajira,” amesisitiza Kihenzile.

Sekta ya kilimo nchini Tanzania inachangia asilimia 26 ya pato la Taifa, asilimia 65 ya ajira pamoja na asilimia 65 ya malighafi za viwandani ambapo Serikali inakusudia kufikisha mpaka asilimia 30 ya mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato la taifa ifikapo mwaka 2030.

Enable Notifications OK No thanks