Fanya haya kujilinda dhidi ya kupasuka midomo, ngozi kukauka wakati wa baridi

Lucy Samson 0715Hrs   Juni 30, 2022 Kolamu
  • Wataalam wanashauri kupaka mafuta kwa wingi.
  • Tumia muda mchache wakati wa kuoga hasa unapotumia maji ya moto.
  • Epuka kuota moto kwa muda mrefu unaweza kuharibu ngozi.

Dar es Salaam. Ni kawaida kila ifikapo mwezi Juni hadi Agosti kila mwaka, maeneo mengi nchini Tanzania kuwa na hali ya baridi na upepo. 

Hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk  Ladislaus Chang’a alisema kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), huwa ni kipindi cha baridi na upepo kwa maeneo mengi ya nchi. 

“Katika kipindi cha JJA, 2022 hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki,” alisema Dk Chang’a.

Alisema kutokana na kubadilika kwa mifumo ya hali ya hewa hasa baharini, vipindi vya upepo vinaweza kutokea hasa kwa wakazi wa mikoa ya pwani. 

Hali hiyo husababisha athari mbalimbali za kiafya kwa watu ikiwemo baadhi kupata michubuko kwenye mdomo, pua na sehemu nyingine za mwili. Wengine ngozi zao huwa kavu na kuwapotezea mwonekano wao wa awali. 

ukiwa ni miongoni mwa watu ambao wamepata changamoto hizo za kiafya, usihofu kwa sababu suluhisho lipo.


Hali hii husababishwa na nini?

Dk Joshua Sultan kutoka hospitali ya Ahmadiyya iliyopo mkoani Morogoro  amesema hali ya ngozi kuwa kavu na kupasuka mdomo kunatokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema kipindi cha baridi hali ya hewa inakuwa na ukavu, hivyo inaondoa unyevu nyevu (humidity) kwenye ngozi. 

“Katika kipindi hiki kunakuwa na dry air (hewa kavu) ambayo inanyonya unyevu nyevu wote uliopo kwenye ngozi ndiyo inapelekea kuwa na ngozi kavu, wengine hupasuka mdomo na kuchubuka maeneo mbalimbali mwiini,” amesema Dk Sultan.

Wakati wa baridi, watu wengi hutumia nguo nzito ili kujikinga na hali hiyo lakini baadhi hupata changamoto za kiafya ikiwemo ngozi kukauka na midomo kuchumbuka. Wataalam wa afya wanasema hali hiyo ni kawaida. Picha| BBC.

Hatua za kujikinga na kupasuka midomo na ngozi kukauka

Paka mafuta mengi kwenye ngozi

Dk Sultan anasema ili ngozi isiwe kavu, inatakiwa watu waongeze unyevunyevu kwenye ngozi kwa kupaka mafuta.

“Katika kipindi hiki ni vyema sana kupaka mafuta kwa wingi. Mafuta yawe ya kawaida mfano ya nazi, sishauri mtu atumie losheni kwani  losheni inachochea ukavu,” amesema Dk Sultan.


Tumia mafuta ya kujilinda na mionzi ya jua (sunscreens)

Baadhi ya watu wana ngozi nyepesi ambazo huathirika sana na mionzi ya jua. Katika kipindi hiki watu wa aina hiyo wanatakiwa kutumia mafuta ya kujilinda na mionzi hiyo kwa kiasi kikubwa.

“Paka mafuta ya kukulinda na mionzi ya jua, ili kutunza unyevu nyevu unapokua juani au kwenye mwanga mkali. Hii itakulinda na madhara zaidi yatakayotokea katika kipindi hiki cha hali ya ubaridi,”ameomgeza Dk Sultan.


Soma zaidi


Tumia muda mchache wakati wa kuoga

Kipindi hiki cha baridi watu hupenda kuoga maji ya mojo, Dk Sultan  anashauri mtu akioga maji ya moto atumie muda mfupi, kwa sababu maji ya moto na yenyewe ni chanzo cha kukausha ngozi.

“Mtu anapooga haifai uchukue muda mrefu, uoge maji ya moto lakini kwa muda mfupi ili usipoteze unyevu wa ngozi yako wakati unaoga,” amesema mtaalam huyo wa afya ya binadamu.


Kupaka mafuta kabla ya kuvaa nguo ndefu na kujifunika

Kwa kipindi cha baridi ni kawaida watu kujifunika nguo nzito ili kujikinga na baridi, anashauri mtu ajifunike wakati mwili ukiwa na unyevu wa kutosha.

“Ni vyema mtu akijifunika awe amepaka mafuta ili kuupa mwili unyevu unaotakiwa, ukijifunika ukiwa hujapaka mafuta unachochea ngozi kupata cracks (michubuko),” amesisitiza mtaalamu huyo.

Hata hivyo, ngozi kukauka au kupasuka kwa midmo ni suala la kawaida ambalo hutokea nyakati za baridi.


Tangazo



Tahadhari yatolewa

Dk Sultan ametahadharisha uwepo wa  madhara mengine yatokanayo na hali ya ubaridi, kama mafua, kikohozi  na homa za msimu, ambazo husababishwa na hali ya ubaridi na upepo unaoendelea.

Hali hiyo ni ya kawaida na hutokea zaidi wakati wa msimu wa baridi.

Hata hivyo, amesema watu wasipendelee kuota moto kwa muda mrefu kipindi cha baridi kwa sababu badala ya kuupa mwili joto inaweza kuongeza uwezekano wa kuharibika kwa ngozi.

Related Post