Usifanye makosa haya unapochagua kozi ya kusoma elimu ya juu

Nuzulack Dausen 0015Hrs   Julai 23, 2019 Kolamu
  • Miongoni mwa mambo ya kujizuia ni kusoma kozi kwa kufuata mkumbo.
  • Usiangalie uzuri wa jina la kozi wala kusoma kile usichokipenda.
  • Fanya tathmini ya gharama za kozi unayoenda kusoma kama utaweza kuzimudu. 

Wakati natafuta kozi ya kusoma chuo kikuu ilinichukua takriban wiki mbili kufanya uamuzi. Sikuwa na mtu wa karibu aliyesoma elimu ya juu ambaye angenishauri kwa haraka.

Taarifa kuhusu kozi bora za kusoma chuo kikuu zilikuwa chache na hata kama zilikuwepo mtandaoni wakati huo sikuwa na huduma ya intaneti huko kijijini kwetu Mbarali. Kwa kifupi ilikuwa ni tafrani.

Vyuo ambavyo wakati wote vinanijia akilini vilikuwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho kilikuwa kimetoka tu kuanza.

Licha ya kuwa na matokeo mazuri kidato cha sita, nilikuwa hatarini kukosa chuo kutokana na kuchelewa kupata taarifa muhimu ambazo zingeniwezesha kusoma nachokipenda.Wenzangu waliokuwa na ndugu au jamaa wenye upeo wa kuwashauri kozi za kusoma waliomba mapema tu huku wakitutambishia sisi walalahoi masomo watakayosoma. 

Wiki mbili kabla ya tarehe ya mwisho niliomba kusoma chuo kikuu baada ya uchambuzi wangu wa kina bila kuwa na taarifa za kutosha zaidi ya Muongozo wa Masomo wa UDSM pekee ambao na ulikuwa umeshapitwa na wakati kwa mwaka mmoja zaidi.


Zinazohusiana: 


Tofauti na miaka ya nyuma, miongozo ya masomo ni mingi na kuna taarifa za kutosha lakini kuna baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu hujikuta wakikosa vyuo kutokana na makosa waliyofanya wakati wanachagua kozi za kusoma.

Licha ya kuwa makosa ni mengi, haya ni baadhi ya mambo unayotakiwa kuyaepuka unapochagua masomo ya kusoma elimu ya juu.

Usiangalie uzuri wa jina la kozi

Kwa vijana wengi, ndoto ni kuja kufanya kazi au kuitumikia taaluma yenye staha na heshima kubwa. Vijana wengi tunataka tuje kuwa mabosi na mtego huo hutufanya tukimbilie kusoma kozi zenye maneno mazuri kama “menejimenti”, “utawala” na majina mengine ya kuvutia.

Kwa bahati mbaya siyo kozi zote zenye majina ya kuvutia zina maudhui yatakayokufanya uwe bora au uwe na soko baada ya kuhitimu. Baadhi kozi hizo hutengenezwa kuvutia wateja hivyo ni bora ujiridhishe maudhui ya kozi husika kabla ya kukimbilia kuchagua kozi yenye jina zuri isiyokuwa msaada mbeleni.

Usifuate mkumbo

Kwa kuwa baadhi ya vijana huwa na mtandao wa marafiki waliosoma wote au kukaa nao mtaa mmoja wanaojiunga na vyuo vikuu ni rahisi sana kutengeneza mkumbo wa kusoma kozi inayofanana. Usipende kusoma kitu kutokana na mkumbo bila kufanya utafiti wa kina juu ya manufaa ya masomo husika siku za mbeleni.

Sisemi kusoma kozi inayosomwa na wengi ni kosa la hasha. Kosa ni kuisoma kozi hiyo bila kujiridhisha kuwa itakuwa na manufaa kwako hapo mbeleni.

Omba ushauri kwa waliokutangulia na baadhi ya watu waliopo kwenye tasnia inayohusiana na kozi husika upate taarifa za kutosha kabla ya kuingia kichwa kichwa.


Usichague kozi bila kujua gharama za ujumla

Ni vema kabla ya kusoma kozi yeyote chuo kikuu ni vyema ukajiridhisha na gharama za msingi kuihusu ili kuepuka mtikisiko wa kifedha. Kuna baadhi ya kozi hasa za sayansi na teknolojia zinahitaji fedha nyingi katika kuisoma mbali na ada ya msingi kutokana na mahitaji mengine kama vitendea kazi vya kujifunzia na bei za vitabu vyake.

Jaribu kudodosa gharama za ada na gharama za ziada na ujifanyie tathmini kwa uwezo wako wa kifedha au ukipewa nusu ya mkopo wa elimu ya juu utaweza kuisoma bila matatizo? Hii itakusaidia kujipanga vema wakati unaisoma kozi na itapunguza msongo wa mawazo utakapoanza masomo.

Angalia mustakabali wa masomo husika

Masomo ya elimu ya juu ndiyo nguzo ya taaluma yako hapo baadaye ama kukuwezesha kupata ajira au kujiajiri. Ili uweze kuwa na thamani sokoni ni vema ukasoma kozi ambazo hazipo hatarini sana kutoweka ulimwenguni kutokana na kuongezeka kwa kasi ya matumizi ya teknolojia.

Japo hili jambo lina mvutano kidogo baina ya wadau nchini lakini ni vema kuliangalia ili usije kupoteza muda na fedha zako halafu ukakuta umesomea taaluma ambayo maroboti yameshaanza kuifanya na inaweza kutoweka kabisa miaka 10 ijayo.

Baadhi ya masomo yanayohusisha uchapaji yanaanza kukosa soko kwa kuwa kompyuta zinafanya mambo yote na mabosi wengi kwa sasa wanajifanyia kazi wenyewe. Ni vema kuangalia kazi zinazoendana na mwenendo wa soko na ambazo zitahitajika zaidi hapo baadaye.

Masomo ya elimu ya juu ndiyo nguzo ya taaluma yako hapo baadaye ama kukuwezesha kupata ajira au kujiajiri. Chagua kozi itakayokutengenezea mstakabali mzuri wa maisha yako. Picha|Mtandao.

 Usisome kitu ambacho hukipendi

Licha ya kuwa kuna nguvu mbalimbali zinazofanya watu wasome masomo ambayo hawayapendi matakwa ya wazazi, jitahidi kwa uwezo wako kuzuia nguvu hizo zisikuathiri iwapo zinaepukika. Kusoma kitu usichokipenda ni hatari katika kujenga mustakabali chanya wa kitaaluma.

Ni mara chache sana utalazimika kuisoma kozi hiyo iwapo inakuja na fursa kama kupatiwa mkopo au ufadhili wa masomo. Hata kama itatokea utaisoma kozi ambayo hauipendi kwa sababu zilizo nje ya uwezo wako jitahidi siku za mbeleni utakaposimama kuitumia taaluma husika kwa kuhusianisha na kile unachopenda kukifanya.

Related Post