Unayotakiwa kuyafahamu kuhusu viyoyozi

Rodgers George 0330Hrs   Juni 23, 2020 Teknolojia
  • Ni pamoja na kuzingatia muda wa kuifanyia ukaguzi na huduma mashine hiyo.
  • Kushindwa kuihudumia, ni kusababisha uharibifu ambao huenda ukakuongezea gharama usizozitarajia.
  • Dalili za kuwa kiyoyozi chako kinahitaji ukihudumie.

Dar es Salaam. Hakuna anayefurahia kuwasha kiyoyozi na asipate matokeo anayoyatarajia.

Naam! Matokeo hayo ni baridi ambalo hutoka kwenye mashine ya kupooza hewa ambayo huwekwa ofisini, nyumba za makazi na kwenye vyombo vya usafiri kama gari na ndege.

Sintofahamu huibuka pale unapoiwasha ili upate hali ya hewa unayoitaka (joto au baridi) lakini usipate unachokusudia.

Hata hivyo, zipo sababu nyingi zinazosababisha wewe kutokupata matokeo unayoyahitaji kutoka kwenye kiyoyozi chako maarufu kama “Air Condition (AC)” zikiwemo ukosefu wa mlingano wa umeme kwenye mifumo ya jengo lako pamoja na ukosefu wa matengenezo ya kiyoyozi chenyewe.

“AC inatakiwa kufanyiwa service (matengenezo) kila baada ya miezi mitatu. Kushindwa kufanya hivyo, kunasababisha mashine hiyo kushindwa kufanya kazi vizuri,” amesema fundi wa viyoyozi na friji, Baraka Selemani anayefanya kazi zake Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam.

Matengenezo hayo ni pamoja na huduma ya kuvisafisha, kuongeza gesi endapo imepungua na kuangalia kama hakuna kifaa chochote ndani yake ambacho hakifanyi kazi kwa ufasaha. 

Hakuna anayefurahia kuwasha kiyoyozi na asipate matokeo anayoyatarajia. Picha| Rodgers George.

Utajuaje kama AC yako inahitaji matengenezo?

Kupungua kwa ufanisi na utendaji

Selemani amesema dalili kubwa ya kiyoyozi kuhitaji matengenezo ni kupungua kwa ufanisi wake wa kutoa baridi kila unapowasha na kutumia.

Mara nyingi watu hupuuzia hali hii huku wengine wakiihusisha na upungufu wa umeme lakini wasichofahamu ni kuwa AC  inawataarifu kuwa “ninahitaji matengenezo.”

Kumwagika kwa maji

Dalili nyingine ambayo fundi Selemani ameweka wazi ni maji ya AC kudondokea ndani badala ya nje. 

Hapo ndipo mtumiaji wa AC anapoanza kuweka vidumu na ndoo kuyakinga maji akihisi AC yake inafanya kazi vizuri kumbe imeanza kupata tatizo.

“AC inapoanza kutoa maji ndani inamaanisha kuwa kuna uchafu na saa zingine tope ambalo linakiuwa limekwama kwenye bomba la kutolea maji nje. 

“Hali hiyo inasababisha maji yanayotakiwa kutolewa nje yamwagikie ndani,” ameeleza Selemani.

Zaidi, mtaalamu huyo wa viyoyozi amesema kuendeleza kupuuzwa kwa dalili hizo husababisha vitu vingine katika mashine hiyo kuharibika vikiwemo kompresa na vitu vingine vinavyoipatia nguvu AC.


Zinazohusiana


Nini kitatokea endapo utashindwa kuihudumia AC yako?

Maelezo ya Mtaalamu wa viyoyozi na majokofu kutoka kampuni ya ABC Refrigeration iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam, Jacob Sabini yameainisha kuwa utarajie ongezeko la gharama kwani utaishia kununua vifaa vingi ambavyo vinaweza kuwa vimeharibika.

“Unapoifanyia service (huduma) AC yako unaangalia mambo mengi yakiwemo mfumo wa nyaya ambazo huenda zinaweza zikawa zimeliwa na panya, kiwango cha gesi kilichopo na mengineyo,” amesema Sabini.

Sabini ameshauri watu kuwasiliana na fundi walau miezi sita ili kukagua na kuifanyia matengenezo AC yako kuepukana na gharama zisizo za lazima.

Mbali na hilo, unatakiwa kufahamu kuwa, endapo AC yako haifanyi kazi vizuri hasa kutoa baridi, utaishia kutumia umeme mwingi kwani itachukua muda mrefu kukupatia ubaridi katika chumba chako.

Usicheze mbali na ukurasa huu Jumanne ijayo, nitakapokuelezea juu ya swichi za ndani ya nyumba.

Related Post