Njia za asili zitakazokusaidia kukabiliana na tatizo la kukosa usingizi

Joshua Sultan 0752Hrs   Septemba 22, 2019 Kolamu
  • Watu wengi hupata shida kupata usingizi kwa sababu ya kula kupita kiasi na matumizi ya vinywaji kama pombe, kawaha, chai muda mfupi kabla ya kulala.
  • Njia za asili za kutatua tatizo hili ni pamoja na kula mlo kamili, kuepuka vinywaji kama pombe na kulala kwenye chumba chenye hewa nzuri. 

Mwili wa binadamu unafanya kazi kwa namna nyingi ili kumuwezesha kuongeza ufanisi na ubora pamoja na kufikia malengo yake. 

Katika namna ya tofauti mwili wa binadamu umewekewa saa ya asili “natural clock” ambayo humfanya kutambua wakati wa kulala na kuzalisha homoni maalumu kwa ajili ya  kuleta usingizi ambayo kitaalamu hujulikana kama “Melatonin”. 

Wakati wa kulala unapokaribia mwili huachilia kiwango fulani cha homoni hii ili kukupatia usingizi. Usingizi ni muhimu sana maana huufanya mwili upumzike na kuufanya ujisikie vizuri.  

Unaweza kuona namna mwili unavyokuwa wa tofauti na kupata nguvu mpya pindi uamkapo na ufanisi wa utendaji wako unavokuwa baada ya kupata usingizi mwanana. 

Kwa lugha ya kisasa tunaweza sema usingizi ni namna mojawapo ya “reboot” mfumo mzima wa mwili wako. Lakini wapo wanaokabiliwa na tatizo la kukosa usingizi, hivyo kuwakosesha mambo mengi ya maendeleo.  

Tatizo hilo linajulikana kama Insomnia. Ni tatizo la kushindwa kupata usingizi mfululizo au mara kwa mara kwa namna isiyo ya kawaida. 

Kwa kawaida unaweza kosa usingizi mara moja au mara mbili kutokana na msongo fulani wa mawazo au mabadiliko  ya kifisiolojia ya kimwili. 

Lakini tatizo hili linapokuwa sugu ni ugonjwa, kwani huathiri mfumo mzima wa maisha yako ya kawida na kukunyima raha na uchovu usio na kikomo. Na hii ndiyo dalili kuu ya tatizo hili.

Tatizo hilo linajulikana kama Insomnia. Ni tatizo la kushindwa kupata usingizi mfululizo au mara kwa mara kwa namna isiyo ya kawaida. Picha|Mtandao.

Inaelezwa kuwa nchini Marekani takribani watu milioni 100 wana insomnia na hunywa wastani wa tani 600 za vidonge vya usingizi kila mwaka kuliepuka tatizo hili. 

Wanawake ndiyo wanakumbwa zaidi na tatizo hilo ambapo ni mara saba zaidi ya wanaume na kuifanya nchi hiyo kuwa na matumizi makubwa ya dawa za usingizi kutibu tatizo hilo.

Licha ya kuwa dawa hizo zinasaidia kupunguza tatizo lakini siyo salama kwa sababu huambatana na madhara kadhaa mwilini ikiwemo kukosa raha, kupata vipele,kukosa hamu ya kula, kukosa ulinganyo (coordination), shida za kuona, kizunguzungu, shinikizo la juu la damu, kuharibika kwa mfumo mkuu wa fahamu na changamoto ya kumbukumbu. 

Sababu za kupata insomnia

Watu wengi hupata shida kupata usingizi kwa sababu ya kula kupita kiasi, kula chakula na unywaji wa vinywaji kama pombe, kawaha, chai muda mfupi kabla ya kulala

Matatizo katika mifumo ya moyo, ini, figo, mapafu, kongosho na homoni pamoja na ubongo huweza fanya mtu kukosa usingizi pia. 


Soma zaidi: 


Njia za asili za kutatua insomnia

Njia ya awali ya utatuzi wa changamoto hii huanza na kile unachokula. Anza kwa lishe madhubuti iliyopangiliwa. Kula chakula chenye lishe zaidi. Kula kifungua kinywa na mlo wa mchana kama vyakula vyako vikuu. Kula mlo mwepesi kabla ya kulala.

Kula vyakula vyenye “amino acids” vyenye “trytophan”  ndani yake, kuchochea usingizi. Mfano mzuri, ni tende na nafaka zisizokobolewa. 

Pata madini ya kalsiamu, ukosefu wa madini haya hukufanya uamke saa chache baada ya kulala na kushindwa kurudi kulala tena. 

Epuka vyakula ghafi na vinasumbua kumen’genywa (ikiwemo nyama) kabla ya kulala. Vyema zaidi ukiachana na vyakula vya haraka “junk foods”. Pia epuka viazi, sukari, spinachi au nyanya ghafi, unywaji pombe, kahawa na chai kabla ya kulala. 

Vitu hivi vina kemikali aina ya “tyramine” ambayo kimsingi huchochea uzalishwaji wa homoni nyingine ya “norepinephrine” ambayo huchochea ufanyaji kazi wa ubongo, jambo linaloweza kukosesha usingizi.

Hakikisha unalala kwenye chumba chenye mazingira mazuri na masafi ikiwemo madirisha yanayoingiza hewa. Picha|Mtandao.

Mwanga wa jua husaidia sana kuchochea usingizi usiku. Uamkapo asubuhi, fungua mapazia ya dirisha lako kisha achia mwanga uingie ndani. Baadhi ya takwimu huonyesha kwamba ratiba nzuri ya kazi na wakati wa kulala inayozingatiwa hurahisisha kupata usingizi. Zingatia kuwa mwaminifu kwa muda wako wa kulala kila siku.

Pia oga maji ya moto saa moja au mawili kabla ya kulala. Kabla ya kulala waweza pata dakika 30 hadi 45 za kutembea kidogo kupata hewa safi. Chumba chako kiwe na mzunguko mzuri wa hewa na kisiwe na kelele. Pia joto la chumba chako liwe la kawaida. Joto kali sana hukufanya uamke na kushindwa kulala.

Jilaze kitandani mwako, jiachie (relax) na mshukuru muumba wako kwa baraka zake. Hii hukupatia mtulizo ndani ya akili na kukupatia usingizi mwanana. 

Related Post