Sababu za kusinzia kazini na jinsi ya kuzuia

Rodgers George 0201Hrs   Januari 13, 2020 Kolamu
  • Unashauriwa usinywe maziwa wakati wa asubuhinatumia maziwa au chakula chenye maziwa huna haja ya kushangaa.
  • Badala ya maziwa, pendelea kutumia matunda na vyakula vyenye protini huku ukiepuka vyakula vya wanga.
  • Matokeo ya kutumia vyakula vya wanga kwa wingi ni kitambi na maradhi mengine yanayotokana na kuzidi kwa mafuta mabaya mwilini.

Dar es Salaam. Umewahi kuamka asubuhi ukiwa na nguvu nyingi na furaha ya kwenda kazini? Lakini ufikapo kazini na kupata kifungua kinywa unajikuta huna tena hamu ya kufanya kazi. 

Unajikuta unapata uchovu na usingizi, jambo linalopunguza kasi yako ya utendaji wa kazi. 

Wakati mwingine unatamani meza yako igeuke godoro na bosi wako ageuke kipofu ili upate usingizi walau wa nusu saa. Usichofahamu ni kuwa kupata usingizi uwapo kazini kunachochewa na baadhi ya vyakula unavyovitumia asubuhi. 

Endapo haufurahii kazi yako, yapo ambayo unaweza kufanya lakini endapo unasumbuliwa na usingizi kiasi cha kupunguza uwajibikiaji wako kazini, dondoo hizi zinaweza kukusaidia kuondokana na tatizo hilo:


Acha kunywa maziwa asubuhi

Huenda unafurahia kuchanganya majani ya chai na maziwa na kisha kufurahia vitafunwa vyako ukijihisi asubuhi yako imeanza na mlo kamili. 

Daktari kutoka Kituo cha Afya cha Ngare na Nyuki mkoani Arusha Jonas Kaguo amesema ni muda wa kuanza kubadili mlo wako endapo unatumia maziwa kwani yana tindikali ya amino (amino acid) aina ya “tryptophan” ambayo inachochea usingizi.

Siyo maziwa tu, hata bidhaa zake ikiwemo siagi. Lakini siyo watu wote wanaokunywa maziwa wanapata tatizo la usingizi, hii ni mahususi kwa wale ambao wakinywa maziwa wanalala. 


Maziwa yana tindikali ya amino (amino acid) aina ya “tryptophan” ambayo inachochea usingizi. Picha| Dissolve

Baada ya kufahamu kuwa kunywa maziwa kunachochea usingizi wako uwapo kazini, hivi ni baadhi ya vyakula vitakavyokuongezea nguvu na kukufanya uwe mwenye uchangamfu uwapo kazini.


Tangawizi

Unajiuliza utapata wapi tangawizi asubuhi lakini kama ofisini kwenu kuna jagi la kuchemshia maji, zipo tangawizi za unga zinazouzwa madukani kwa gharama kuanzia Sh3,000.

Mbali na kukuondolea adha ya kuhisi usingizi, tangawizi itakunufaisha kwa manufaa mengi yakiwemo kuondoa msongo wa mawazo, kichefuchefu na hata kusaidia mzunguko wa damu.


Sharubati (Juisi ya matunda)

Hakika unahitaji kujipunguzia dozi ya kahawa ambayo umekuwa ukijipatia kila asubuhi na badala yake unaweza kuchagua sharubati ya matunda uyapendayo ili siku yako iwe nzuri zaidi.

Sharubati itakupatia virutubisho vingi mwilini hasa vitamini C ambavyo hakika unavihitaji ili kuwa na siku nzuri kazini. Endapo hautapata sharubati asilia, ni vyema ukatumia matunda kama parachichi, tikiti maji, ndizi na mengineyo. 


Zinazohusiana:



Pumzika vya kutosha

Wakati wenzako wanafunga wikiendi yao kwa mitoko ili kupata vinywaji kama pombe, unaweza kuokoa fedha zako siku ambayo unafahamu utaamkia kazini na kupumzika.

Ukipata usingizi wa kutosha, ni nadra sana kupata usingizi ukiwa kazini. 

Wataalamu wanashauri mtu kupata walau masaa saba hadi tisa ya kulala wakati wa usiku hivyo. Endapo unaamka saa 11:00 asubuhi, unatakiwa ulale mapema siyo zaidi ya saa 4:00 usiku.

Mtaalamu wa afya kutoka Kituo cha Afya cha Ngarenanyuki, Dk Jonas Kaguo amesema kwa ujumla usitegemee kukosa usingizi baada ya kula vyakula vya wanga asubuhi.

“Wengi wanapenda kunywa supu na chapati asubuhi na wengine wakinywa uji hasa mashuleni. Ni lazima utasinzia tu,” amesema Dk Kaguo.

Kaguo ameshauri kutumia mboga za majani, matunda na vyakula vya protini kama nyama na samaki wakati wa asubuhi. Kama huwezi kutumia kama vilivyo, basi jitahidi matumizi yako ya vyakula vya wanga viwe kwa kiasi cha chini kabisa lakini huenda tatizo la usingizi lisikuache.

Wakati mwingine unatamani meza yako igeuke godoro na bosi wako ageuke kipofu ili upate usingizi walau wa nusu saa. Usichofahamu ni kuwa kupata usingizi uwapo kazini kunachochewa na baadhi ya vyakula unavyovitumia asubuhi. Picha|Mtandao.

Naye mtaalamu wa lishe, Filbert Mwakilambo amesema kwa watu ambao hukaa ofisini kwa muda mrefu, wanatakiwa kula matunda na mboga mboga kwa wingi huku kiasi cha protini na wanga kikiwa cha chini.

“Unapotumia chakula cha wanga kwa wingi na haufanyi kazi zenye kuupa mwili kazi, baada wanga kubadilishwa kuwa glucose (sukari) kwa ajili ya ubongo, kiasi kinachobaki hugeuzwa kuwa mafuta na kuanza kuhifadhiwa mwilini na ndiyo maana wengi hupata vitambi.” amesema mtaalamu huyo.

Mwakilambo amesema mboga mboga na matunda vimesheheni makapi mlo ama faiba (kamba kamba) ambazo hukaa tumboni kwa muda mrefu na hivyo kumfaa mtu ambaye hana muda wa kutembea kutafuta chakula.

Wafanyakazi wa maofisini hawana haja ya kuhofia kupata njaa baada ya kula mlo huo badala ya kujijaza na vyakula vyenye wanga.

Related Post