Zingatia haya kabla hujafungua kesi ya madai mahakamani

Hamza Lule 0141Hrs   Machi 06, 2021 Kolamu
  • Ni pamoja na ya kufahamu ukomo wa muda wa kufungua shauri mahakamani na uwezo wa mahakama kushughulikia shauri lako.
  • Pia unapaswa kumtambua kwa ufasaha mdaiwa wako ni wa aina gani. 

Migogoro ni sehemu ya maisha kwenye jamii yetu. Hakuna jamii hai ambayo haina migogoro. Migogoro hii inasabababishwa na mambo mbalimbali kama vile mikataba, ardhi na hata kufukuzwa kazini. 

Uwepo wa migogoro umewezesha kuwepo kwa sheria ambazo zimekua zikitoa ufafanuzi wa jinsi gani mgogoro husika utatatuliwa, hivyo basi mdai anapaswa kufungua kesi ya madai inayoendana na aina ya mgogoro wake ili aweze kupata tiba ya madai yake kwenye mgogoro husika.

Migogoro hiyo inaweza kusuluhishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwemo mahakamani. Ni vyema kuzingatia mambo yafuatayo kabla ya kufungua kesi ya madai kwenye mahakama yoyote ile:


1. Mdaiwa 

Ni vyema kuweza kuainisha kwa kina kwenye kesi yako ya madai kwa kutambua nani ni mdaiwa ikiwa na maana kuwa nani unamdai au unamdhania kuwa amekiuka haki zako za msingi ambazo unaomba mahakama ikutendee haki. Kujua unayemdai au upande wa pili wa kesi kunasaidia kuweza kujua usahihi wa madai yako na hoja za majibu ambazo zitaletwa na upande wa pili au mdaawa.

Aina ya mdaiwa ina umuhimu wake kisheria sababu kuna tofauti kubwa kati ya mdaiwa binafsi na Serikali kwenye uendeshaji wa kesi husika. Kwa mfano, mdaiwa akiwa Serikali kuna hitaji la kupatiwa notisi ya siku ya 90 kabla ya kufungua kesi husika ikiwa na maana kuwa Serikali ipewe taarifa.

Kushindwa kutambua mdaiwa wako vizuri kunaweza kusababisha shauri lako kuondolewa mahakamani.

Ukiweza kuzingatia mambo haya kabla ya kufungua shauri lako utaweza kufanikiwa kusikilizwa kwa kesi yako pasi na kukutana na mapingamizi ya ukomo wa muda, uwezo wa mahakama wala kushindwa kumtambua mdaiwa.  Picha| Unsplash.

2. Ukomo wa muda

Kabla ya kufungua kesi ya madai ni vyema uweze kujua kama uko nje ya muda kisheria au ndani ya muda. Ukiwa nje ya muda kisheria unapaswa kuangalia namna gani utaomba mahakama ikuongeze muda wa kuweza kufungua shauri lako nje ya muda au kuwasilisha maombi yako kwa waziri wa sheria ili uweze kupewa ruhusa hiyo. 

Kufungua shauri au kesi ya madai nje ya muda kunafanya mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo. Unashauriwa kuangalia na kuweza kufahamu kama kesi yako iko ndani ya muda au la ili kuepusha kutupiliwa kwa kesi yako na kupoteza haki zako za msingi kisheria.


Soma zaidi: 


3. Uwezo wa mahakama

Sio kila mahakama inaweza kupokea aina ya kesi yako, na sio kila mahakama inaweza kushughulika na kesi zote. Uwezo wa mahakama kushughulika na kesi unazingatia aina ya kesi au msingi wa madai, thamani ya madai na eneo husika ambalo mgogoro umetokea. 

Ni vyema kutambua madai yako yanahusu nini? Kama yanahusu ardhi ni vyema shauri lako ukalipeleka mabaraza ya ardhi ambako shauri lako litasikilizwa ikiwa na maana kuwa ukilipeleka katika mahakama za kawaida litatupiliwa mbali sawa na kesi za kazi lazima zipelekwe mahakama za kazi. 

Thamani ya unachodai lazima kitambulike vyema ikiwa kiasi kinachobishaniwa ni zaidi ya Sh300 milioni basi shauri hilo lazima likasikilizwe Mahakama Kuu. Na ikiwa kiasi kinachobishaniwa ni chini ya Sh50 milioni kesi hiyo inapaswa kusikilizwa na mahakama ya mwanzo. 

Eneo ambalo mgogoro umetokea ni muhimu sana kuweza kujua uwezo wa mahakama, shauri la mgogoro wa kiwanja wa cha Chanika hauwezi kwenda kufunguliwa kwenye Baraza la Ardhi la Kinondoni, kwa sababu Baraza la Ardhi la Kinondoni linashughulikia migogoro ya ardhi ambayo inatokea ndani ya Wilaya ya Kinondoni pekee.

 

Hitimisho

Ukiweza kuzingatia mambo haya kabla ya kufungua shauri lako utaweza kufanikiwa kusikilizwa kwa kesi yako pasi na kukutana na mapingamizi ya ukomo wa muda, uwezo wa mahakama wala kushindwa kumtambua mdaiwa.     

                                     

Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule,

 Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini

Kwa msaada wa kisheria wasiliana nami kupitiaTwiter@Hamzaalbhanj

Mob; 0717521700

Related Post