Afrika inavyoweza kukabiliana na baa la njaa

Lucy Samson 0702Hrs   Septemba 15, 2023 Kolamu
  • Ni pamoja na ujumuishwaji wa wanawake na vijana pamoja na utengenezaji wa masoko huria.
  • Serikali ya Tanzania yajipanga kuimarisha kilimo.

Dar es Salaam. Wakati baadhi yetu tukipata chakula cha kutosha na  kutupa mabaki, Ripoti ya Hali ya Chakula na Lishe Duniani kwa mwaka 2023 inayotolewa na Shirika la chakula na Kilimo (FAO) inaonyesha kuwa watu milioni 783 duniani wanakabiliwa na njaa.

Kati ya hao watu milioni 11 wanatoka bara la Afrika ikiwa ni idadi iliyorekodiwa kwa miaka miwii tangu mwaka 2021.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) watu 25,000 ikiwemo watoto 1,000 hupoteza maisha  kila siku duniani kote, kutokana na njaa.

“Watu milioni 854 duniani kote wanakadiriwa kuwa na utapiamlo, bei ya juu ya vyakula huenda ikasababisha watu wengine milioni 100 kuingia kwenye umaskini na njaa,” inabainisha UN.

Mbali na kupunguza hatari ya baa la njaa kilimo kinaweza kukuza uchumi wa nchi za Afrika. Picha|Daudi Mbapani.

Fao inasema miongoni mwa sababu zilizopelekea tatizo la njaa katika nchi za Afrika ni pamoja na kupanda kwa bei za vyakula, pembejeo za kilimo na nishati kulikosababishwa  na athari za vita vya Ukraine pamoja na ukosefu wa ajira.

Wakati hayo yakijiri, Josephat Masanja mratibu wa Taasisi ya Africa Youth pastoralist inayojishughulisha na masuala ya kilimo anasema ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za kilimo unaweza kuwa suluhu ya kumaliza tatizo la njaa barani Afrika.

“Huwezi kukwepa Afrika kuwa na usalama wa chakula, kuwa na bidhaa sokoni, kutengeneza ajira pasipo kuwekeza kwa vijana na wanawake,”  amesema Masanja.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB) wanawake huchangia kati ya asilimia 60 hadi 80 ya nguvu kazi katika shughuli za kilimo barani Afrika.

Mtaalamu huyo amesema ili kufanikisha ushiriki wa makundi hayo katika kilimo ni vyema Serikali za nchi za Afrika kutengeneza mazingira wezeshi ikiwemo mitaji ya kutosha, teknolojia ya kisasa pamoja na ardhi ya kutosha.


Soma zaidi


Upatikanaji wa Masoko

Masoko ya bidhaa za chakula ndiyo kimbilio pekee linalotumiwa na nchi nyingi kujipatia chakula, hususan wakati kimepungua katika nchi zao.

Masanja anasema masoko huria miongoni mwa nchi za Africa yatapunguza matatizo ya njaa miongoni mwa nchi hizo na kuziongezea fedha zitokanazo na kilimo.

"Kwa mfano Kenya iweze kununua chakula Uganda, Uganda iweze kuleta Sukari Tanzania…hatupaswi kufurahia Kenya ikiingiza mahindi kutoka Mexico wakati wakulima wetu wana mahindi ya kutosha…

…Nchi kwa nchi ziweze kufanya biashara ili fedha zinazopatikana ziwasaidie wakulima wadogo kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetatua tatizo la ajira na kupunguza umaskini uliokithiri katika bara hili," ameongeza Masanja.

Ili kuimarisha upatikanaji wa masoko kaika nchi za Afrika, Jumuiya ya Nchi za Afrika ( African Union) imeanzisha soko huria litakayowezesha  usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma muhimu ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula, na viwanda vilivyopo barani Afrika.

Kuwekeza kwenye tafiti za kilimo

Kilimo ni sayansi inayohitaji uwepo wa tafiti mbalimbali zitakazo wezesha upatikanaji wa mbegu bora za kisasa zinazoweza kustahimili mabadiliko mbalimbali ya tabia ya nchi. 

Kwa Mujibu wa Masanja tafiti hizo zitawezesha usalama wa mbegu zitakazo hakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha kwa ajili ya masoko ya ndani na nje.

"Ni lazima tuwekeze katika eneo la utafiti,ni nchi Kenya pekee ambayo imetenga angalau asilimia 1 ya bajeti kwa ajili ya utafiti…tafiti zinasaidia kuja na mbegu bora ambazo zitakabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi," amesema Masanja.

Aidha, utafiti wa magonjwa yanayosumbua wakulima mara kwa mara na mbolea ni maeneo mengine yanayopaswa kuangaziwa na Serikali za Afrika ili kumaliza tatizo la njaa.

Kilimo cha mashamba makubwa chini ya mradi wa BBT unatarajiwakupunguza tatizo la ajira nchini.Picha|ITV

Tanzania yajipanga kuimarisha kilimo

Katika kuimarisha sekta ya kilimo  nchini Serikali ya Tanzania imeongeza bajeti ya kilimo hadi ShSh970.7 bilioni zitakazo wezesha shughuli mbalimbali za Wizara na maendeleo ya kilimo nchini ikiweno kilimo cha mashamba makubwa.

Mwezi Machi mwaka huu Rais Samia alizindua kilimo cha mashamba makubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma ili kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao nchini.

Mashamba hayo yanatajiwa kunufaisha zaidi vijana na wanawake kupitia program maalum inayojulikana kama Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) iliyolenga kutoa ajira 1,000,000 ifikapo mwaka 2025.

Miongoni mwa masula yaliyojadiliwa katika Mkutano wa Jukwaa la Chakula (AGRIF) uliofanyika jijini Dar es Salaam Petemba 4 mpaka 8 ni usalama wa chakula, masoko huria pamoja na changamoto zinazokabili nchi hizo.

Related Post