Ripoti: Afya ya akili chanzo cha watu kujiua, kuua Tanzania

Lucy Samson 0814Hrs   Aprili 25, 2024 Afya & Maisha
  • Utafiti wa Haki za Binadamu umebaini kuwa idadi ya watu wanaojiua nchini Tanzania imefikia 57 kutoka 35.
  • Wanaume na vijana wenye miaka 15 hadi 35 ndiyo waathirika zaidi.

Dar es Salaam. Matukio ya watu kujiua yameendelea kuongezeka nchini baada ya ripoti mpya ya haki za binadamu ya mwaka wa 2023 kubainisha kuwa vifo vya watu waliojiua viliongezeka zaidi ya mara moja na nusu mwaka 2023 vikichochewa zaidi na matatizo ya afya ya akili. 

Ripoti hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam inaonesha kuwa idadi ya watu wanaojiua nchini Tanzania imeongezeka hadi kufikia 57 kutoka 35 ndani ya mwaka mmoja.

“Kwa mwaka 2023 matatizo ya afya ya akili yameendelea kusababisha watu kujiua. LHRC tumerekodi matukio 57 ya kujiua ikiwa ni ongezeko la matukio 22 kulinganisha na yale yaliyorekodiwa 2022,” imesema ripoti hiyo.

Matukio hayo ya kujiua yanayotokana na afya ya akili ni yale yaliyorekodiwa katika mikoa yote nchini isipokuwa mikoa ya Kagera, Katavi, Kigoma, Njombe, Rukwa, Singida na Tabora.


Zinazohusiana:Matatizo ya afya ya akili: Kaburi jipya la wanandoa


Wanaume, Vijana hatarini zaidi

Ripoti hiyo imebainisha kuwa wanaume wanaongoza kwa kujiua kwa asilimia asilimia 79 ikipungua kutoka asilimia 83 iliyorekodiwa mwaka 2022.

Hiyo ni sawa na kusema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wanaume nane kati ya 10 walijua kutokana na matatizo ya afya akili na sababu nyingine ikiwemo madeni, wivu na kufukuzwa kazi.

Kati ya idadi hiyo, karibu nusu (asilimia 46) ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35, ikifuatiwa na watu wa makamo (asilimia 27) wenye umri kati ya miaka 36 hadi 59 na watoto chini ya umri wa miaka 18 kwa asilimia 25.

Miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa matukio hayo ni kukosekana kwa bajeti huduma bora za afya pamoja na ufinyu wa wahudumu wa afya ambao wangewasaidia waathirika wa afya akli kupata tiba mapema.

Ndani ya miaka ya hivi karibuni wadau wa masuala ya afya akili wamekuwa wakitaka Serikali kuongeza jitihada za kutatua tatizo hilo kwa kuongeza wahudumu wa afya, miundombinu na huduma za saikolojia ili kuzuia athari zaidi.

Afya ya akili isipodhibitiwa inaweza kuharibu maisha ya mtu. Picha| Unsplash/Yosi Prihantoro

Udhaifu katika utoaji wa huduma stahiki wa masuala ya afya akili pia umebainishwa na Ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere kwa mwaka 2022/23 baada ya kueleza kuwa kuna mapungufu ndani ya Wizara ya Afya katika kuwabaini wagonjwa wa afya ya akili katika ngazi ya jamii.

Kwa mujibu wa CAG, utambuzi uliofanywa  na wizara hiyo ulilenga  waathirika wa dawa za kulevya, wazee walemavu na watoto walio katika mazingira magumu na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Mbali na kujiua, ripoti hiyo ya LHRC imeeleza kuwa matatizo ya afya ya akili kwa mwaka 2023 yamesababisha vitendo vingine vya kikatili ikiwemo mauaji ya wenza ambapo wanawake ndio kundi lili hatarini zaidi.

Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja jumla ya matukio 50 ya mauaji yaliyoripotiwa sababu kubwa ikitajwa kuwa ni afya ya akili pamoja na sababu nyingine ikiwemo wivu wa kimapenzi.

Related Post