NBC yatoa gawio la Sh4.5 bilioni kwa Serikali ikiongeza faida

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba, akiwa ameshikilia mfano wa hundi ya Sh4.5 bilioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, (kulia) ikiwa ni gawio la Serikali kwa mwaka 2021, jijini Dodoma. Anayeshuhudia ni Kamishna Idara ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Charles Mwamwaja. Picha| Wizara wa Fedha na Mipango.
- Linatokana na asilimia 30 ya hisa inazomiliki katika benki hiyo.
- NBC yalipa kodi ya Sh20 bilioni kwa Serikali.
- Fedha hizo zitatumika kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imevuna gawio la Sh4.5 bilioni kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kutokana na faida iliyopata benki hiyo mwaka 2020/21.
Serikali imepata fedha hizo ambazo zitatumika kugharamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji kwa sababu inamiliki asilimia 30 ya hisa za benki hiyo kongwe ya biashara Tanzania.
Waziri wa Fedha na mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akizungumza katika hafla fupi ya kupokea gawio hilo Juni 3, 2022 jijini Dodoma, ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kuimarika na kuongeza faida kila mwaka inayosababisha kuongezeka kwa kiwango cha kodi kinacholipwa serikalini na gawio linalotolewa kwa wanahisa wote.
“Nimefarijika sana kusikia kuwa kwa mwaka 2021 benki ya NBC ilipata faida kabla ya kodi ya Sh60 bilioni, ambalo ni ongezeko la asilimia 702 kutoka faida ya Sh6.2 bilioni iliyopatikana mwaka 2020. Haya ni mafanikio makubwa sana,” amesema Dk Nchemba.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru, amesema kuwa kutolewa kwa gawio hilo kutoka NBC inathibitisha kuwa maamuzi yaliyofanywa na Serikali katika kubinafsisha mashirika ya umma yalikuwa ni maamuzi yenye tija ambayo sasa yanatoa mchango mkubwa wa kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Soma zaidi:
- TTCL yatoa gawio la Sh2.1 bilioni kwa Serikali ikiendelea kusaka mtaji mkubwa
- Ukopeshaji sekta binafsi waongezeka zaidi ya mara 10 Tanzania
Mafuru amesema kuwa sekta ya benki nchini kwa sasa imekua kwa asilimia 10, hivyo kusababisha sekta hiyo kuwa taasisi muhimu inayogharamia shughuli za uchumi nchini.
Taasisi zinazomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 zimetakiwa kujifunza kutoka kwenye mashirika yanayomilikiwa kwa ubia na Serikali ili kuona ni jinsi gani yatajiendesha kwa faida.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi ameshukuru Serikali kwa kuiwezesha benki hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kueleza kuwa mwaka 2021 benki hiyo imetoa kodi Sh20 bilioni serikalini pamoja na kutoa gawio hilo la Sh4.5 bilioni.
Benki hiyo pia imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji wa zaidi ya Sh1 bilioni iliyotumika katika misaada ya kijamii, na uwekezaji kwa zaidi ya Sh9 bilioni zilizotolewa kwenye mchezo wa soka kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia msimu huu wa ligi kuu ya “NBC Premier League”.
Uwekazaji huo uliofanywa na NBC umezalisha ajira zaidi ya 9,000 na ajira zaidi zinaendelea kutolewa kutokana na mnyororo wa thamani kupitia sekta ya michezo.
Kaimu Msajili wa Hazina ambaye ofisi yake inasimamia mashirika ambayo Serikali imewekeza hisa zake pamoja na mashirika ambayo inamiliki hisa chache, Joseph Mwaisemba amesema kuwa hadi kufikia mwezi Mei, Ofisi yake ilifanikiwa kukusanya maduhuli ya Sh691 bilioni na inahitaji Sh86 bilioni ili iweze kufikia lengo na kwamba gawio hilo la NBC linapunguza nakisi hiyo.
Latest