Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 4.7 mwaka 2022
- Unatarajiwa kukua zaidi kwa asilimia 5.3 mwaka 2023.
- Ushiriki wa Sekta binafsi na uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo vyatajwa kuwa vichocheo.
Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 4.7 mwaka 2022 kutoka ukuaji wa asilimia 4.9 uliorekodiwa mwaka 2021ukichagizwa na ushiriki wa sekta binafsi na uwekezaji katika miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, Dk Nchemba amesema mwaka 2023 kasi inatarajiwa kuongezeka na kufikia ukuaji wa asilimia 5.3 kutoka asilimia 4.7 inayotarajiwa katika mwaka huu unaoishia Desemba.
Katika mwaka 2021, Nchemba ameeleza uchumi ulikua kwa kasi ya asilimia 4.9 nyuma kidogo ya matarajio ya ukuaji wa asilimia 5 ukiathiriwa zaidi na madhara ya Uviko-19.
Katika hotuba yake ya Taarifa hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021 na Mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2022/23 , Dk Nchemba amesema matarajio hayo yanategemeana na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za maendeleo, kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili kama vile ukame, vita na magonjwa ya mlipuko.
“Ukuaji huo pia utategemea na misingi ya kuendelea kuwa na utoshelevu wa chakula nchini pamoja na uwepo wa amani, usalama, umoja, utulivu wa ndani na katika nchi jirani,” amesema Dk Nchemba leo (Juni 14, 2022) jijini Dodoma.
Zinazohusiana:
- Serikali ya Tanzania yaanika vipaumbele vinne bajeti 2019-2020
- Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 5.5 mwaka 2020
Huu ni mpango wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) unaolenga kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.
Hata hivyo, Dk Nchemba ameeleza kuwa shabaha za uchumi kwa mwaka 2022/23 ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani kati ya asilimia 3 hadi 7.
Shabaha nyingine ni mapato ya ndani kufikia asilimia 14.9 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23, Mapato ya kodi kufikia asilimia 11.7 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23 na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Fedha hadi Aprili 2022 akiba iliyokuwepo ilikuwa ni Dola za Marekani bilioni 5.6 sawa na Sh12.88 trilioni zinazotosha kugharamia uingizaji wa bidhaa na huduma kwa muda usiopungua miezi 4.8 juu kidogo ya ukomo wa miezi minne.
Bajeti kuu ya taifa itasomwa hii leo Juni 14,2022 majira ya saa 10 jioni bungeni jijini Dodoma na Dk Nchemba huku tayari Watanzania wakiwa na vilio lukuki vya kupunguziwa gharama za maisha kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma miezi ya hivi karibuni.
Je, bajeti hiyo itabeba matumaini ya Watanzania? Ni suala la muda.
Latest
