Serikali ya Tanzania yaongeza bajeti ya 2021-22 hadi Sh36.26 trilioni

February 8, 2021 4:15 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni jijini Dodoma Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/22, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.


  • Inatarajia kuongeza makusanyo na matumizi hadi Sh36.26 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia nne kutoka Sh34.88 trilioni katika mwaka wa feda unaoishia Juni 2021.
  • Uwiano wa mapato ya ndani kwa mapato yote unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 71.8 ya bajeti ya mwaka 2021/22 hadi asilimia 76.7 ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2023/24.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kuongeza makusanyo na matumizi hadi Sh36.26 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia nne kutoka Sh34.88 trilioni katika mwaka wa feda unaoishia Juni 2021.  

Waziri wa Katiba na Sheria Mwigulu Nchemba amewaambia wabunge jijini Dodoma leo Februari 8, 2020 kuwa ongezeko hilo la bajeti linatokana na mahitaji ya mfuko mkuu wa fedha ikiwemo kulipia deni la Serikali, kuajiri na kupandisha madaraja watumishi wa umma.

Nchemba aliyekuwa akimwakilisha Waziri wa Fedha Dk Philip Mpango amesema mapato ya ndani, yakijumuisha mapato ya halmashauri, yanakadiriwa kuongezeka hadi Sh26.03 trilioni mwaka 2021/22 kutoka makadirio ya Sh24.07 trilioni mwaka 2020/21. 

Mapato hayo ya ndani yanatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 8.6 katika muda wa kati.

Uwiano wa mapato ya ndani kwa mapato yote, kwa mujibu wa Nchemba, unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 71.8 ya bajeti ya mwaka 2021/22 hadi asilimia 76.7 ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2023/24.

“Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka hadi Sh21.47 trilioni mwaka 2021/22 kutoka Sh20.14 trilioni mwaka 2020/21 na kukua kwa wastani wa asilimia 7.1 katika muda wa kati,” ameeleza Nchemba.

Amesema mapato yasiyo ya kodi, yakijumuisha mapato ya halmashauri, mapato ya utalii na mapato mengine yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, yanakadariwa kuwa Sh 4.56 trilioni mwaka 2021/22 na kuongezeka kufikia Sh5.60 trilioni itakapofika mwaka 2023/24.

Serikali inatazamia kuendelea kupunguza utegemezi na kwa mujibu wa Nchemba washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh2.89 trilioni sawa na asilimia 7.9 ya bajeti yote mwaka 2021/22.

Mbali na washirika wa Maendeleo, Serikali inatarajia kukopa Sh4.99 trilioni kutoka soko la ndani ambapo kati ya kiasi hicho Sh 3.15 trilioni kitatumika kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Sh1.84 trilioni sawa na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa ni mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Mikopo ya masharti ya kibiashara kutoka nje inatarajiwa kuwa Sh 2.35 mwaka 2021/22.


Zinazohusiana:


Katika matumizi, Serikali ya Rais John Magufuli anayemalizia muhula wa pili wa uongozi wake, inatarajia kutumia Sh23 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh13.26 trilioni ni matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.

Nchemba amesema matumizi ya kawaida yanajumuisha mishahara Sh 8.15 trilioni (sawa na asilimia 31.3 ya makadirio ya mapato ya ndani), malipo ya riba na mtaji kwa deni la ndani na nje Sh8.88 trilioni na matumizi mengineyo Sh5.97 trilioni.

Matumizi ya maendeleo yanajumuisha Sh10.37 trilioni ambazo ni fedha za ndani na Sh 2.89 trilioni fedha za nje, amewaambia wabunge.

“Makadirio ya matumizi ya maendeleo yamezingatia kukamilika kwa miradi mbalimbali kama vile maboma ya shule na vituo vya kutolea huduma za afya ambayo yanahitaji fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji,” amesema.

Serikali ya Rais Magufuli inatekeleza miradi mikubwa ya ujenzi ukiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na ujenzi wa bwawa la kufufua umeme la Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV