Ahueni, Serikali ikipunguza ada za huduma kwa ‘content creators’
- Ada ya maombi ya leseni ya huduma za maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka Sh 50,000 hadi shilingi 10,000.
Dar es Salaam. Huenda watengeneeza maudhui mtandaoni nchini Tanzania wakapata ahueni mara baada ya Serikali kupunguza ada za huduma kwa kundi hilo hatua inayotarajiwa kuongeza ushiriki wa vijana katika majukwaa ya kigitali.
Waziri wa Fedha wa Tanzania Balozi Khamis Mussa Omar alipokuwa akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo June 11, 2026 amesema marekebisho hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kukuza uchumi wa kidigitali na ajira kwa vijana.
Hatua hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya kifedha vilivyokuwa vinawakwamisha vijana wengi kuingia na kukua katika sekta ya ubunifu wa kidigitali.
Kwa mujibu wa marekebisho hayo katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni), ada mbalimbali zimepunguzwa kwa kiwango kikubwa.
Ada ya maombi ya leseni ya huduma za maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka shilingi 50,000 iliyokuwa ikitumika awali hadi shilingi 10,000.
Aidha, ada za awali za mwaka pamoja na za kuhuisha leseni ya huduma za maudhui mtandaoni zimepunguzwa kutoka shilingi 500,000 hadi shilingi 50,000, hatua inayoweka mazingira rafiki zaidi kwa watumiaji wengi hasa vijana.
Punguzo hilo la asilimia 80 kwa upande wa maombi ya leseni za huduma na asilimia 90 kwa ada za awali za mwaka huenda zikawapunguzia maumivu watengeneza maudhui hao ambao wamekuwa wakiongezeka katika siku za hivi karibuni.
Tangu kuanzishwa kwa ada hizo wadau mbalimbali wamekuwa wakipiga kelele ili zipunguzswe ili kuongeza ushiriki wa vijana katika majukwaa ya kidigitali
Kwa upande wa wakusanyaji wa maudhui mtandaoni (Online Content Aggregators), ada ya maombi imepunguzwa kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 20,000, huku ada za leseni (initial, annual na renewal) zikishushwa kutoka shilingi 1,000,000 hadi shilingi 100,000.
Katika kipindi ambacho uchumi wa kidigitali unaendelea kukua kwa kasi, maboresho haya yanatarajiwa kuongeza ajira, kuchochea ubunifu na kuongeza mapato ya Serikali kupitia sekta hiyo.