Serikali ya Tanzania yaongeza bajeti ya 2022-23 hadi Sh41.06 trilioni

March 11, 2022 2:33 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeongezeka kutoka Sh36.26 ya mwaka 2021/22.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kuongeza makusanyo na matumizi kwa asilimia 4.8 ihadi Sh41.06 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 huku ikiweka kipaumbele katika kujenga uchumi shirikishi.

Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh36.26 trilioni iliyotengwa mwaka wa fedha 2021/22 unaoisha mwezi Juni mwaka huu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewaambia wabunge jijini Dodoma leo Machi 11, 2022 kuwa kati ya fedha hizo, Sh25.5 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 62.2 ya bajeti yote, ikijumuisha Sh11.3 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu.

“Matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh15.5 trilioni sawa na asilimia 37.8 ya bajeti yote. Kati ya kiasi hicho, Sh12.1 trilioni ni fedha za ndani, sawa na asilimia 78.1 ya bajeti ya maendeleo na Sh3.4 trilioni ni fedha za nje,” amesema Dk Nchemba.

Amesema utekelezaji wa bajeti hiyo itazingatia maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ikiwemo kuchochea uchumi shindani na shirikishi na kuimarisha uwezo wa uzalishaji kwenye sekta zinazotoa malighafi viwandani.

Maeneo mengine ni kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Ili kuhakikisha bajeti hiyo inatekelezwa ipasavyo, Serikali itaimarisha na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwa ni pamoja na kuwianisha, kufuta, kuongeza au kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada zinazoonekana kudhoofisha uwekezaji na biashara.


Zinazohusiana: 


Pia itaimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama ya ukusanyaji wa mapato na kuratibu na kusimamia utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali na washirika wa maendeleo.

Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali itapunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo kwenye miradi ya kielelezo na kimkakati. 

“Aidha, Serikali itaendelea kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi ikiwemo kilimo, uvuvi, misitu, mifugo, madini na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji,” amesema.

Maeneo mengine ni pamoja na kuboresha mishahara ya watumishi wa umma, kugharamia deni la Serikali na madeni ya ndani yaliyohakikiwa; kuendelea kuboresha Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (TANePS) katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi za ujenzi na kuimarisha matumizi ya mifumo ya Tehama.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...