TTCL yatoa gawio la Sh2.1 bilioni kwa Serikali ikiendelea kusaka mtaji mkubwa

May 21, 2019 8:54 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL, Omar Nunduamesema kuwa pamoja na changamoto ambazo kampuni hiyo inakabiliana nazo bado wameendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za mawasiliano nchini. Picha|Mtandao.


  • CEO wa kampuni hiyo amesema gawio hilo limekuja baada ya hesabu kukaguliwa na ni takwa la kisheria.
  • Mwenyekiti wa bodi wa TTCL Omar Nundu amesema sehemu ya faida iliyobaki itatumika kwenye miradi midogo ya kimkakati.
  • Nundu amesema bado kampuni hiyo inatafuta mtaji mkubwa wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma zake.

Dar es Salaam. Kampuni ya simu ya TTCL imeipatia Serikali gawio la Sh2.1 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh600 milioni zaidi ya kiasi kilichotolewa mwaka jana baada ya kuongezeka kwa faida kwa taasisi hiyo ya umma nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL, Omar Nundu amesema leo (Mei 21, 2019) wakati wa hafla ya utoaji wa gawio kwa Serikali jijini Dar es Salaam kuwa gawio hilo la 2.1 bilioni ni kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.

“Gawio hilo ni ongezeko la Sh600 milioni zaidi ya gawio la Sh1.5 bilioni tulilolitoa mwaka jana. Gawio hili lilitokana na faida ya Sh8.3 bilioni ambapo mapato yalikuwa Sh119 bilioni na matumizi yalikuwa Sh111 bilioni.

“Kwa ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyetupa hati safi tumejibakizia takriban Sh6.7 bilioni zituwezeshe kuanza kuwekeza kwenye miradi midogo midogo ya kimkakati wakati tukitafuta mtaji mkubwa na kuwezeshwa zaidi,” amesema Nundu katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Rais John Magufuli.

Nundu amesema kuwa pamoja na changamoto ambazo kampuni hiyo inakabiliana nazo bado wameendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za mawasiliano nchini.

Tayari mwaka huu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu ya TTCL, Waziri Kindamba ameeleza mapato yamefikia Sh167 bilioni.


Zinazohusiana: TTCL yavunja rekodi watumiaji wa simu baada ya ‘kudumaa’ kwa miaka nane


Katikati ya Juni mwaka jana kampuni hiyo ilitoa gawio la Sh1.5 bilioni na kuzua maswali iwapo TTCL ilikuwa imefikia hatua ya kuweza kutoa gawio hilo ikizingatiwa kuwa bado inahitaji mtaji mkubwa kuboresha huduma zake.

Leo katika hotuba yake katika hafla ya utoaji gawio kwa Serikali, Kindamba ametumia jukwaa hilo kujibu maswali hayo akisema kuwa hesabu za kampuni hiyo zinaruhusu gawio hilo kutolewa.

“Kuna maswali mengi yanaulizwa kwenye vyombo vya habari na huko kwenye mitandao kuwa ni vipi taasisi iliyokuwa hoi kiuchumi na pengine imeshapotea kwenye ramani na leo ikatoa gawio kwa Serikali?” ameeleza Kindamba na kuongeza;

“Mheshimiwa Rais mahesabu haya hayajatengenezwa na mzee Omar Nundu wa Tanga wala hayajatengenezwa na kijana wa Kariakoo Waziri Kindamba. Yametengenezwa na wahasibu wabobezi ndani ya TTCL.

“Baada ya mahesabu hayo kutengenezwa yanakuja kukaguliwa na mkaguzi wa ndani (Internal Auditor). Akimaliza huyo anakuja anapita The Controller and  Auditor General (CAG) ndiye anayethibitisha hesabu na kusema kitabu hiki ni kisafi au kichafu kwa maana ya hati safi ama chafu halafu baadaye ndiyo anadeclare (anatangaza) kwamba kitabu hiki kinafaida ama hasara”.

Kindamba amesema baada ya CAG kuthibitisha hesabu hizo, TTCL ilipeleka mapendekezo ya kutoa gawio kwa Bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo yenye makao makuu Barabara ya Sokoine Jijini Dar es Salaam.

“Kutoa gawio ni matakwa ya kisheria na ni maelekezo yako kama mkuu wa nchi ambayo umekuwa ukitoa mara kwa mara na pia ni muongozo wa msajili wa hazina, “ amesema Kindamba.  

Enable Notifications OK No thanks