Migogoro ya binadamu, wanyamapori yazua mjadala Bungeni
- Ni kutokana na ongezeko la visa vya wanyama hao kuua na kuharibu mazao.
- Wanyamapori wazidi kuongezeka kwa kiasi nchini.
- Serikali yawatuliza Wabunge wakati ikitafuta suluhu ya suala hilo.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kukiri wanyamapori kuongezeka nchini baada ya kufanikiwa kudhibiti ujangili, Wabunge wamesema wanyama hao wameendelea kuwa kero kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa na maeneo tengefu.
Wamedai wanyamapori hao wamekuwa wakivamia makazi na mashamba ya wananchi na kufanya uharibifu wa mali na wakati mwingine kujeruhi watu na kusababisha vifo.
aziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana amesema kutokana na kuimarika kwa ulinzi na uhifadhi, kudhibiti ujangili, biashara haramu ya nyara, uvunaji haramu wa mazao ya misitu na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa, idadi ya wanyamapori imeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Dk Chana aliyekuwa akinukuu takwimu za matokeo ya Sensa ya Wanyamapori iliyofanyika mwaka 2021 amesema idadi ya tembo imeongezeka kwa asilimia 30, nyati (asilimia 80), pundamilia (asilimia 36), palapala (asilimia 65) na faru weusi walio hatarini kutoweka wameongezeka kwa asilimia 27.5 ikilinganishwa na sensa iliyofanyika mwaka 2018.
“Matokeo ya sensa katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha – Rungwa yanaonesha kuwa kuna tembo 15,608, nyati (20,911), swala pala (8,643), pundamilia (10,552), palapala 6,636 na kongoni 4,017.
“Aidha, matokeo hayo yakilinganishwa na yale ya mwaka 2018 yanaonesha kuimarika kwa idadi ya tembo sambamba na ongezeko la nyati kwa asilimia 80, pundamilia asilimia 36, na palahala asilimia 65,” amesema Chana.
Tembo ni miongoni mwa wanyamapori ambao wameongezeka Tanzania na wamekuwa wakivamia makazi ya watu. Picha| Tanapa.
Waziri huyo aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 amesema ongezeko hilo limesaidia kuimarisha shughuli za utalii nchini ikiwemo kuvutia watalii na kuzidi kuitangaza Tanzania kimataifa.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika taarifa yake kuhusu watalii wanaotembelea Tanzania iliyotolewa Mei 19, 2022 imeeleza kuwa kati ya Januari na Aprili wataliii 367,632 waliingia Tanzania.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la watalii 92,535 kutoka watalii 275,097 waliotembelea vivutio vya Tanzania katika kipindi kama hicho mwaka jana wakati Uviko-19 ukiwa unaitesa dunia.
Kati ya watalii walioingia nchini, 124,212 waliingia kupitia Zanzibar sawa na zaidi kidogo ya theluthi moja ya watalii wote walioingia Tanzania.
Wabunge wasema wanyamapori ni kero
Pamoja na habari hizo za ongezeko kuwa njema kutokana na kuwa miongoni mwa kiungo muhimu katika sekta ya utalii, Wabunge wameibuka na kuhoji Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti wanyamapori wanaovamia makazi ya binadamu na kufanya uharibifu.
Makamu Mwenyekiiti wa Kamati ya Kudumu ya Maliasili na Utalii, Shaaban Shekilindi amesema kwa muda mrefu sasa kumekuwa na muingiliano kati ya binadamu na wanyama wakali ambao wamekuwa wakisababisha uharibifu huku akiitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti wanyama hao.
“Serikali ichukue hatua madhubuti na ya haraka katika kukabiliana na changamoto ya muingiliano wa binadamu na wanyama wakali na waharibifu kama vile tembo, mamba, tumbili ili kuondoa madhara yanayoweza kujitokeza bila kuathiri uwepo wa wanyama hao,” amesema Shekilindi.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu
- Mvutano wa tembo, binadamu unavyoacha maumivu Tanzania – 1
Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amewataka wataalamu wa wanyamapori kufanya uchunguzi na kubaini sababu inayofanya wanyama vamizi kutoka nje ya hifadhi kwani baadhi ya maeneo yako mbali na mbuga.
“Lazima wenzetu wataalamu wa wizara hii wakae, wasiwe wanatuletea stori iliyozoeleka ya korido, mapito ya tembo ya miaka. Leo hii watu wengi wanaumia ,wanakufa, mali zao zinaharibiwa kwa sababu tu tembo wanazunguka kila mahali,” amesema Mtaturu huku akionekana kukerwa na jambo hilo.
Pamoja na jimbo lake kuwa linakabiliwa na uvamizi na usumbufu kutoka kwa wanyama hususan tembo kwa sababu liko karibu na hifadhi ya Taifa ya Mkomazi,
Mbunge wa Mwanga Joseph Tadayo ameiomba Serikali kutoa kifuta machozi kwa waliopoteza maisha na fidia kwa walioharibiwa mazao yao na wanyama hao.
“….tulikwenda na mheshimiwa Naibu Waziri kule hali haikuwa nzuri lakini kuna mambo ambayo tuliwaahidi wananchi wa Mwanga ambayo yangesaidia kupunguza tatizo hili…… kuna suala la kifuta machozi kwa waliopoteza maisha na fidia kwa waliopoteza mazao hayo pia hayajakamilika,” amesema Mbunge Tadayo
Serikali inafanya nini?
Dk Chana mwezi Mei mwaka huu alitoa tahadhari za kuchukua ili kuepukana na wanyamapori wakali na waharibifu kama tembo, simba, mamba na viboko ambao matukio yao yamekuwa yakijirudia hasa katika Wilaya 53 kati ya 134 nchini.
Katika taarifa hiyo Waziri alibainisha miongoni mwa hatua ambazo Serikali imezichukua ni pamoja na kuwajengea uwezo wananchi kwa kuwapatia mafunzo na vifaa vya kujilinda ambapo hadi sasa mafunzo yametolewa kwa wanafunzi 660 katika Wilaya 21 kati ya 53 zenye mgongano
Pia wizara yake inaendelea kukamilisha mafunzo kwenye wilaya zilizosalia sambamba na kuanzisha vituo 11 vya kudumu kwa askari wanyamapori kwenye maeneo yanayoathirika zaidi ili kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.
Latest