Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu

July 2, 2020 12:12 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya tembo zaidi ya 300 kuripotiwa kufa huku chanzo cha kifo kikiwa hakijulikani.
  • Vyanzo vya ndani vya nchini humo, vimeripori kuwa asilimia 70 ya tembo hao wamekufa karibu na vyanzo vya maji.
  • Mamlaka za wanyama pori zasema Corona inachelewesha majibu ya vipimo.

Dar es Salaam. Tembo zaidi ya 300 wameripotiwa kuuwawa kaskazini mwa nchi ya Botswana huku chanzo cha vifo hivyo vikiwa hakijafahamika hadi sasa.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, kufa kwa tembo hao kumeanza tangu mwezi Mei ambapo kwa mwezi huo, tembo 169 walianguka baada ya kukutwa katika kingo za Mto Okavango nchini humo.

Idadi ya vifo iliongezeka kwa takribani mara mbili mwezi Juni huku asilimia 70 ya vifo vya wanyama hao vikidaiwa kutokea karibu na vyanzo vya maji.

Nchi hiyo iliyopo Kusini mwa Afrika, inategemea utalii kujipatia pato la Taifa, ikiripotiwa kuwa na tembo wengi kuliko nchi yeyote barani Afrika wanaofikia 130,000 kwa mujibu wa National Geographic.

Asilimia 70 ya vifo vya wanyama vikidaiwa kutokea karibu na vyanzo vya maji. Picha| BBC.

Hata hivyo, hadi sasa Serikali ya nchi hiyo imesema haijafanikiwa kufahamu chanzo cha vifo vya tembo hao licha ya kuwa baadhi ya vyanzo vya ndani ya nchi hiyo kusema kuwa inaweza kuwa ni madhara ya uchafuzi wa mazingira.

Mkurugenzi wa uhifadhi kutoka Shirika la kuokoa hifadhi za Taifa Dk Niall McCann katika mahojiano yake na Daily Mail amesema vifo hivyo ni vingi kuwahi kutokea kwa muda mrefu huku akisema mbali na vifo vya awali vilivyosababishwa na ukame, hajawahi kusikia chanzo kama kilichopo sasa.

Dk McCann amesema, “ukiiangalia mizoga, baadhi yao imedondokea sura, ikionyesha kuwa ni kifo cha haraka. Wengine ni dhahiri wamekufa taratibu kama wale waliozagaa. Ni vigumu kusema hiyo ni sumu gani.”

Wakati huo, wanasayansi wa nchini Botswana wameendelea kuishauri Serikali ya Botswana kuchukua hatua za haraka kufahamu chanzo cha vifo hivyo ili kuzuia uwezekano wa maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kama vifo vimetokana na vimelea vya mambukizi ya magonjwa.

Hata hivyo baadi ya wanasayansi wamehusisha vifo vya tembo hao na ugonjwa wa Corona ambao unaitesa dunia kwa sasa na hivyo kuishauri serikali kuchukua hatua za haraka.


Zinazohusiana


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Wanyama Pori na Hifadhi za Taifa wa Botswana Dk Cyril Taolo akihojiwa na gazeti  The Guardian amekiri kufahamu juu ya vifo hivyo huku akisema hadi sasa kati ya vifo 300, vilivyothibitishwa ni 280.

Dk Taolo ameulaumu ugonjwa wa Corona ambao umesababisha makatazo kwa baadhi ya nchi na hivyo kupunguza kasi ya upimaji wa sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa tembo hao zilizopelekwa nchi zingine kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.

“Bado tupo katika taratibu za kuthibitisha vipimo,” amesema Dk Taolo.

Licha ya kuwa idadi ya tembo barani Afrika inashuka kutokana na ujangiri, tembo nchini Botswana wanaongezeka kutokana na asera nzuri za kuwalinda.

Kwa mujibu wa Shirika la Wanyamapori Duniani (WWF), hadi mwaka 2018, Bara la Afrika lilikuwa na jumla ya tembo 415,000 huku wakiwa katika hatari ya kutoweka kutokana na vitendo vya ujangiri, ukosefu wa makazi na migogoro kati ya wanyama hao na binadamu.

Enable Notifications OK No thanks