Mvutano wa tembo, binadamu unavyoacha maumivu Tanzania - 1

Daniel Samson 0942Hrs   Agosti 20, 2020 Ripoti Maalum
  • Ongezeko hilo lafungua fursa za utalii na maendeleo ya vijiji vinavyozunguka hifadhi za Taifa.
  • Katika baadhi ya maeneo, tembo wanavamia na kuharibu mazao ya wakulima na mashine za kusagia nafaka.
  • Serikali imesema wananchi ndiyo wanafuata maeneo ya asili ya wanyama hao.

Rufiji. Baada ya vitendo vya ujangili kupungua wakazi wa Kijiji cha Mloka walianza kupata matumaini mapya kijijini kwao. Sifa chafu ya awali ya kuwa walikuwa ni kitovu cha uwindaji haramu ilitoweka.

Tembo walianza kuongezeka na shughuli za utalii zikapamba moto miaka minne iliyopita.

Wakati Serikali na wadau wa utalii nchini Tanzania wakijivunia kuongezeka kwa tembo hao baada ya kukomesha kwa ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo, wakazi wa kijiji hicho katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kwao wanaeleza “maumivu”.

Tembo sasa wamegeuka karaha kwa wakazi wa kijiji hicho kilichopo kilomita 11 kutoka hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa sababu wanyama hao huvamia mashamba na makazi yao na kuwaletea uharibifu wa mazao, nyumba na mashine za kusagia nafaka.

Katika makala iliyopita tuliangazia namna kukomeshwa kwa ujangili katika wilaya ya Rufiji kulivyochangia kuongezeka kwa tembo na shughuli za utalii.

Kwa sasa, wakazi wa Mloka wanaishi kwa hofu kwa sababu karibu kila siku tembo huingia katika kijiji chao na kufanya uharibifu.

“Tembo walikuwepo lakini walikuwa hawavamii mashambani lakini mwaka huu hali ni tofauti,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Ally Didunda.

Didunda ambaye mwaka huu alilima heka 3 za mahindi lakini tembo wamevamia shamba lake na kuharibu sehemu kubwa ya mazao yake na huenda asivune chochote kwa sababu amebakiwa na heka moja tu.

Matumaini ya Didunda kuvuna mahindi hayo yanayokomaa kwa miezi 3 yanazidi kupungua kwa sababu karibu kila siku tembo wanaingia kwenye mashamba ya wanavijiji na kula mazao hasa mahindi, korosho, mpunga na ndizi.

“Ningevuna mahindi hayo mwezi Agosti ningepata Sh1.5 milioni lakini sasa sina jinsi tena, tembo wameharibu sana shamba langu. Mapato yangu niliyokuwa nategemea niuze ni kwa ajili ya kusomesha mwanangu chuo kikuu na kidato cha nne, lakini sina namna tena,” anasema Didunda ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Mkange kijijini hapo.

Mkazi huyo amesema tembo hao wamekuwa ni pigo kwa familia yake yote kwa sababu mke wake naye amepoteza heka moja ya mahindi kati ya heka mbili alizolima na anafikiria kuachana na kilimo na kutafuta kazi nyingine yenye usalama na uhakika wa kipato.

Tembo hao ambao hutembea kwa makundi hasa wawili hadi wanne siyo tu wanavamia mashamba bali wanafika mpaka katikati ya kijiji hicho ambako kuna makazi na shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo maduka ya mahitaji ya nyumbani na pembejeo za kilimo.

Wakati Didunda akiharibiwa mazao yake, mwenzake Mussa Makuka (35) anayemiliki mashine ya kukoboa na kusaga nafaka hasa mahindi amevamiwa zaidi ya mara 12 na tembo katika eneo lake la kazi.

Makuka mwenye mke na watoto watatu anasema tembo wamekuwa wakivunja kibanda na mashine yake ili kujipatia mabaki ya pumba, jambo linalomuongezea gharama za matengenezo ya mara kwa mara.

                     

Tembo hao ambao hawaleti madhara kwa binadamu ikiwemo kuua au majeraha, huingia kijijini hapo nyakati za asubuhi na jioni kutoka hifadhini, jambo linalowaweka wanakijiji katika hofu na taharuki ya kupoteza mali zao.

“Kwa kweli tunaishi kwa hofu sana kwa sababu hujui tembo atakuja saa ngapi na atafika wapi. Zamani walikuwa wanaishia mashambani lakini sasa wanafika mpaka kwenye makazi yetu,” anasema mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mloka ambaye hakutaka jina lake litajwe.

 

Mashamba na mashine zilizoharibiwa na tembo

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mloka, Ali Mbiteheni anasema katika kipindi kifupi cha mwaka huu, mashamba ya wananchi 50 na mashine za kusagia nafaka nne zimeharibiwa kwa nyakati tofauti na tembo hao ambao wamekifanya kijiji hicho kama sehemu ya wao kutalii.

Takwimu za wakulima walioharibiwa mazao yao na tembo katika vijiji vya Mloka na Mtanza Msona kwa mwaka 2019/2020 zilizotolewa na Idara ya Wanyamapori katika Halmshauri ya Wilaya ya Rufiji zinaonyesha katika kipindi hicho tembo wameharibu zaidi ya ekari 112.5 za mazao ya wakulima 115.

Mazao yaliyoharibiwa ni pamoja na mpunga, mahindi, mikorosho, miembe, ndizi, miwa na ufuta.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa nyumba tano za mashine za kusagia nafaka katika vijiji hivyo zilivunjwa na tembo katika kipindi hicho.

Ripoti ya migogoro ya binadamu na tembo ya mwaka wa fedha 2020 iliyotolewa na Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori Duniani (WWF Tanzania) na Halmashauri za Wilaya za Rufiji na Ruvuma inaeleza kuwa mashamba yenye ekari 172 na mazao yenye thamani ya Sh88.1 milioni yameharibiwa katika wilaya hizo mbili.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 61 au zaidi ya nusu ya mazao yote yaliyoharibiwa ni mahindi.

 Serikali inasema kuwa ongezeko la tembo halina uhusiano na uharibifu wanaofanya bali ni binadamu ambao wamevamia maeneo ya wanyama hao. Picha| Mwaramu Mpunde.

Kifuta machozi nacho changamoto

Licha ya Didunda na Makuka kutoa taarifa kwa mamlaka husika kutokana na madhara waliyoyapata, mpaka sasa hawajapata kifuta machozi chochote kutoka serikalini.

“Niko katika wakati mgumu. Awamu ya kwanza wakati wa masika tulijiorodhesha katika Ofisi ya Kijiji na majina yapo na sijui kama yalienda wilayani (Halmashauri ya Rufiji). Hii ni awamu ya pili lakini hakuna msaada wowote mpaka leo licha ya kutoa taarifa mara kadhaa,” amesema Didunda.

Hata hivyo, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mloka, Mbiteheni anasema kazi yao ni kukusanya taarifa za madhara yaliyotokea na kuziwasilisha katika ofisi ya Wilaya ambapo wao hufanya uamuzi wa kutatua changamoto zilizojitokeza ikiwemo kulipa kifuta machozi kwa waathirika.

 

Kwanini tembo wanaingia kijijini?

Kwa mujibu wa Mbiteheni, ukaribu wa kijiji chao na hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambayo zamani ilikuwa Pori la Akiba la Selous umesababisha kupata matukio mengi ya kuvamiwa mara kwa mara na wanyamapori wakiwemo tembo, viboko na mamba.

Kutokomezwa kwa vitisho na ujangili uliokuwa unafanyika wakati wa biashara ya meno ya tembo nako kumechangia wanyama hao kuwa huru kutembea katika maeneo mbalimbali yaliyo karibu na hifadhi.

Hali hiyo imeongeza muingiliano wa tembo na binadamu kwa sababu wanyama hao hawaogopi tena binadamu na hujikuta wakiingia hadi katika makazi bila ya kuwadhuru.


Soma zaidi:


Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dk Iddi Lipende anasema tembo wana mapitio yao ya asili (shoroba) ambayo wanayatumia kupita kutoka sehemu moja kwenda nyingine kizazi hadi kizazi hata kama kuna makazi ya watu au mashamba.

Anasema hali hiyo husababisha migogoro ya tembo na binadamu na hivyo kuwaletea madhara kwa sababu wanyama hao wanakariri njia za kupita na hawawezi kubadilisha.

“Hata ukilima katika njia zao watapita tu kwa sababu wamezoea na wataleta madhara. Binadamu wanatakiwa kufahamu tabia za wanyama hawa ili kuepuka migogoro,” anasema Dk Lipende.

Mtaalam huyo wa wanyamapori anasema kwa wanyama hao kula mazao ya wakulima ni kutokana na kuvutiwa na madini yaliyopo kwenye mazao kama mahindi na matunda ambayo wakiwa hifadhini hawayapati.

“Ni kama mtu anavyokwenda ugenini, utajaribu kula chakula kipya, na tembo ni hivyo hivyo, wanajaribu vitu vipya kwa sababu mazingira yamebadilika,” anasema mtaalam huyo.

Hata hivyo, Serikali inasema kuwa ongezeko la tembo halina uhusiano na uharibifu wanaofanya bali ni binadamu ambao wamevamia maeneo ya wanyama hao.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiambia Nukta kuwa tembo wanapita katika maeneo yao waliyozoea ambayo sasa yana shughuli za binadamu na kwamba uvamizi wa wanyama hao hauna uhusiano na kuongezeka kwao.

“Tembo wanawasumbua wananchi kwa sababu wamejenga au wamelima kwenye mtawanyiko au maeneo ambayo zamani yalikuwa makazi ya tembo (shoroba) kwa hiyo wale tembo wanapita katika maeneo yale ili kufuata malisho na vyanzo vya maji,” anasema Kanyasu.

Anasema katika maeneo hayo, wanatumia askari wanyamapori kuwadhibiti tembo na wanatoa elimu ili wananchi wafahamu mtindo wa maisha ya wanyama hao na jinsi gani wanapaswa kuepuka shoroba ili wasiendelee kupata madhara.

Baadhi ya askari wanyamapori katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere wakishirikiana na wananchi kutengeneza uzio wa fensi unaosaidia kuzuia tembo kuingia katika mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Rufiji. Picha|WWF.

Kuhusu fidia kwa wananchi wa Mloka walioharibiwa mashamba yao, Kanyasu anasema Serikali inatoa kifuta jasho au machozi na siyo fidia na ili mkulima apate stahiki zake anapaswa kutoa taarifa Serikali za mitaa ili zipelekwe wizarani kwa ajili ya taratibu za malipo.

“Shida ya ucheleweshaji wa kifuta jasho ni wingi wa taarifa tunazopata za uharibifu wa wanyama kama tembo ambazo zinazidi wingi wa uwezo wa mfuko (Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF)) ambao unaweza ukalipa kwa wakati watu wote waliopata madhara,” anasema Kanyasu.

Hata hivyo, anabainisha kuwa Serikali itaendelea kutatua migogoro yote ya wanyama na binadamu ili maeneo ya hifadhi yanakuwa na ustawi mzuri wa mendeleo.

Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii za mwaka 2020/21 inaeleza kuwa hadi Machi, 2020 wizara imelipa jumla ya Sh984.76 milioni kwa waathirika 9,060 wa matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kama kifuta machozi na kifuta jasho.

Kifuta jasho hicho kilikuwa ni kwa ajili ya mwaka 2019/2020 ambao umeisha Juni mwaka huu.

“Aidha, TAWA imefanya jumla ya siku doria 6,612 za kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo wanyamapori wakali 61 waliuawa baada ya kuhatarisha maisha ya wananchi na mali zao,” inaeleza sehemu ya hotuba hiyo.

Related Post