Homa ya ini tishio duniani, Tanzania ikipunguza maambukizi
- Asilimia ya Watanzania wenye maambukizi ya homa ya ini ilipungua na kufikia asilimia 3.5 mwaka 2022.
Dar es Salaam. Leo Julai 28 dunia inaadhimisha Siku ya Homa ya Ini Duniani ambapo licha ya jitihada za kutokomeza ugonjwa huo takwimu zinaonyesha bado ni mwarubaini unaosababisha mamilioni ya vifo ulimwenguni kote.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha idadi ya vifo vitokananvyo na maambukizi ya homa ya ini iliongezeka kutoka vifo milioni 1.1 mwaka 2019 hadi milioni 1.3 mwaka 2024 huku idadi ya watu waishio na maambukizi sugu ikiongezeka na kufikia watu milioni 287.
Homa ya ini ni nini?
Homa ya ini ni hali ya kuvimba kwa ini inayosababishwa na virusi vinavyoambukiza pamoja na visababishi visivyo vya maambukizi.
Ugonjwa huu unaweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya, ikiwemo uharibifu mkubwa wa ini na saratani ya ini, ambayo baadhi yake yanaweza kusababisha kifo
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Eliud Eliakimu ugonjwa huo husababishwa na aina tano za virusi aina A, B, C, D na E.
“ Homa ya ini aina ya B ndiyo inayoongoza kwa maambukizi. Virusi vya aina ya B, C, na D huambukizwa kwa njia zinazofanana na Virusi vya Ukimwi (VVU)…,” anaeleza Dk Eliakimu.
Wizara ya Afya inaeleza kuwa ugonjwa huu huambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kuongezwa damu isiyo salama, kujamiiana bila kinga na mtu mwenye maambukizi, matumizi yasiyo salama ya sindano au vifaa vyenye ncha kali, pamoja na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au kujifungua.
Tanzania yapunguza maambukizi
Licha ya idadi ya vifo na maambukizi kuongezeka duniani Tanzania inaadhimisha siku hii ikiwa imepiga hatua katika kupunguza maambukizi ya homa ya ini aina ya B.
Taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa leo Julai 28, 2026 inaeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2022 asilimia ya Watanzania wenye maambukizi ya homa ya ini imepungua na kufikia asilimia 3.5 kutoka asilimia 4, huku maambukizi ya homa ya ini aina ya C yakishuka hadi asilimia 0.1 kutoka asilimia 1 katika takwimu za awali.
Licha ya kuwepo kwa njia za kuzuia na kutibu ugonjwa huo, WHO inabainisha kuwa bado kuna pengo kubwa katika upatikanaji wa huduma muhimu na uelewa juu ya ugonjwa huu.
WHO inasema mtu mmoja hufariki kila baada ya takribani sekunde 30 kutokana na madhara ya homa ya ini aina B na C, huku ugonjwa huo ukiwa miongoni mwa visababishi vikuu vya saratani ya ini duniani.
Licha ya ukubwa wa tatizo hili, ni asilimia 45 tu ya watoto wachanga waliopokea chanjo ya homa ya ini aina ya B ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa.
Tanzania inaadhimisha siku hii kwa kauli mbiu isemayo “ondoa vikwazo tokomeza homa ya ini” ikisema itaendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwa kuongeza huduma za uchunguzi na matibabu.