Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Doria, elimu na usaliti wa wafanyabiashara uliwezesha biashara hiyo kukomeshwa kabisa.
- Baada ya kukomeshwa kwa biashara hiyo, wakazi wa wilaya hiyo wameanza kunufaika na miradi ya kiuchumi.
- Tembo waongezeka na kuleta madhara kwa wakulima.
Rufiji. Ni mwendo wa zaidi ya kilomita 100 hadi katika kijiji cha Mloka kilichopo katika kata ya Mwaseni Wilaya ya Rufiji katika mkoa wa Pwani kutoka kutoka katikati ya mji mdogo wa Kibiti mkoani humo.
Ili ufike katika kijiji hicho utalazimika utatembea zaidi ya saa tatu katika barabara ya vumbi kwa kutumia gari binafsi na saa zaidi ya tano kwa basi.
Licha ya vumbi la barabarani, haikunizuia kufika katika kijiji hicho ambacho kimebeba mambo mengi kuhusu biashara haramu ya meno ya tembo iliyokuwa imeshamiri nchini Tanzania kabla ya mwaka 2016.
Kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 2,000 kiko karibu na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambayo imeanzishwa mwaka 2019 baada ya kugawanywa kwa Pori la Akiba la Selous.
Upekee wa kijiji cha Mloka ambacho kiko karibu na geti la kuingilia katika hifadhi hiyo la Mtemere ni kwamba kilikuwa kitovu cha biashara haramu ya meno ya tembo iliyokuwa ikifanyika Rufiji kabla ya operesheni kabande ya kuutokomeza.
Lakini sasa mambo yamebadilika. Kijiji hicho kilichofahamika kwa sifa mbaya ya biashara haramu ya meno ya tembo, sasa kimekuwa ni kiungo muhimu kwa shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, jambo linalofungua fursa kwa wanakijiji kunufaika kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa nini Mloka ilikuwa kitovu cha ujangili?
Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Jonas Nambua ambaye alikuwepo kabla na baada ya operesheni “Tokomeza Ujangili” anasema kijiji cha Mloka kilikuwa kinatazamwa kama kitovu cha ujangili katika mkoa wa Pwani kwa sababu ili mtu aingie hifadhini ni lazima apite katika kijiji hicho.
Hali hiyo ilifanya shughuli za biashara ya kusafirisha meno ya tembo zifanyike hapo zaidi kuliko vijiji vingine ambavyo viko mbali na hifadhi.
“Kijiji cha Mloka ina maana ni mwisho wa reli, huwezi kwenda sehemu nyingine. Kwa hiyo pale ni kama Kigoma ndiyo mwisho, ukitoka pale unaingia Pori la Seleous,” anasema Nambua.
Kwa sehemu kubwa kijiji hicho kimezunguka hifadhi ya Nyerere, jambo lililochochea shughuli nyingi kufanyika hapo ukiwemo usafiri wa mabasi na malori ya mizigo kwenda katika maeneo mengine.
Eneo la Rufiji kikiwemo kijiji cha Mloka liliathirika zaidi na biashara hiyo kwa sababu lilikuwa limezungukwa na Pori la Akiba la Selous upande wa mashariki na magharibi ambalo lilikuwa sehemu nzuri kwa wanyama kuishi hivyo kuwavutia majangili kujipatia meno ya tembo kwa siri.
“Soko la biashara hii lilikuwa kwa siri sana kwa sababu shughuli yake ni pevu. Watu waliofanya biashara hii walitumia njia mbalimbali kusafirisha meno hayp kwa sababu mtu anaweza akawa na mzigo kutoka Rufiji unatengenezwa mazingira ya kufichwa kwenye gari huwezi kujua,” anasema Nambua.
Makundi ya tembo ambao wanapatikana katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Tembo hao wamekuwa wakivamia mashamba ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Picha|Mwaramu Mpunde.
Mambo yaliyochangia kutokomezwa kwa ujangili
Ikiwa ni moja ya hatua za kutokomeza, Serikali iliendesha doria mbalimbali kuwasaka wahalifu, wananchi wa kijiji hicho walipewa elimu kupitia semina, warsha na mikutano ya kijiji ili kuwawezesha kuelewa athari za biashara hiyo ambayo siyo tu iliathiri utalii bali usalama wa kijiji hicho.
“Wakati mwingine viongozi wa Serikali walifika kijijini hapo na kuongea na wananchi ili waachane na matendo hayo kwa sababu familia zinapata shida kwa ndugu zao kukamatwa na kuwekwa jela,” anasema Nambua.
Licha ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kutokomeza biashara hiyo, mifarakano miongoni mwa watu waliohusika katika biashara hiyo yalisaidia kupatikana kwa wahusika kwa baadhi yao kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.
Kwa lugha nyepesi, baada ya wawindaji haramu kusalitiana ilikuwa ni rahisi kwa mamlaka kuwapata majingili wengine na kisha kumaliza mtandao wote.
“Lakini toka aingie Mheshimiwa (Rais John) Magufuli katika awamu yake biashara hii imekuwa kama banned (imefutwa) kwa sababu soko lile ambalo lilikuwa linakwenda nje halipo lakini hao majangili wanafuatiliwa mpaka walipo kwa kutumia operesheni maalum,” anasema mtaalam huyo wa misitu.
Hali ilivyo sasa
Kutokana na baadhi ya wenyeji wa kijiji hicho kushirikiana wageni kufanya biashara hiyo kwa siri, shughuli nyingi za maendeleo zilikuwa zikisuasua kutokana vijana kutokutulia.
“Sasa mambo yamebadilika sana, ukitazama hiyo miaka ya 2000 ambayo kila kona nchini biashara ya meno ya tembo ilishika kasi, maisha yalikuwa duni kwa sababu pesa zilishikwa zaidi na wageni ambao walikuwa hawakai sana hapa,” anasema mmoja wa wanakijiji ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mwanaume huyo (40) anasema kuwa kwa sasa wanayoana maendeleo kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji imeamua kukiendeleza kijiji kuwa na miundombinu ya kijamii inayowawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujiingizia kipato.
“Kwa sasa kijiji chetu kinapitika vizuri, barabara ni ya uhakika na mpaka umeme tumeletewa kijiji hapa. Haya hayakuwepo enzi hizo za ujangili maana ni kama tulitengwa,” anasema mwananchi huyo.
Baada ya kukamilika operesheni “Tokomeza ujangili” iliyoanza mwaka 2013, Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo walibuni miradi ya kiuchumi kuwasaidia wakazi wa Mloka ili kuachana na biashara haramu ya meno ya tembo.
Pamoja na Operesheni tokomeza ujangili kukumbwa na tuhuma kubwa za uvunjifu wa haki za binadamu wakati uendeshaji wake, baadhi ya wakazi hawa wanasema ilisaidia kupunguza ujangili katika eneo hilo.
Ili kufanya wanakijiji wawe na shughuli endelevu baada ya kukomeshwa ujangili, miradi kama ufugaji wa samaki na nyuki vimehamasishwa ikizingatiwa wakazi wa kijiji hicho wamezungukwa na rasilimali ya misitu na Mto Rufiji ambao pia unatumika na Serikali katika mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji wa megawati 2,115.
“Sasa huwezi kusikia eti kuna ujangili, vijana wataanzia wapi? Tanapa (Mamlaka ya hifadhi za Taifa) wapo huku wakikamatwa wanapata adhabu kali. Miradi kama hiyo ya kufuga nyuki na kilimo imesaidia hata wale vijana waliopenda shughuli zisizo halali kufaidika nayo,” Chake Mkali, Mwenyekiti wa kijiji cha Mloka wakati ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kijijini hapo hivi karibuni.
Miradi hiyo imewawezesha baadhi ya wanakijiji kupata vitoweo na kipato cha kuendesha familia kutokana na kuuza samaki, asali na mazao wanayolima ikiwemo mahindi, mpunga na korosho.
Hata hivyo, Mkali anasema mvua za masika zilizonyesha mwezi Machi hadi Mei mwaka huu wa 2020, zimeharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya miradi hiyo, jambo linalowakosesha wakazi hao kipato na kuongeza hatari ya kijiji hicho kupata baa la njaa.
Kifo cha ujangili chainua utalii kijiji hapo
Kijiji hicho ambacho kiko takriban kilomita 11 kutoka geti la Mtemere la kuingilia katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere, kwa sasa kinapokea watalii ambao wanafikia katika makambi (camps) ya watu binafsi yaliyopo nje ya hifadhi hiyo.
Kijiji hicho hujipatia mapato ya ushuru kutoka kwa wamiliki wa makambi hayo yanayotumika kuboresha huduma za jamii ikiwemo shule.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Ali Mbiteheni anasema ilikuwa ni vigumu wakati huo ujangili umeshika kasi kwa watalii kufika kijijini hapo kutokana na sifa mbaya iliyokuwepo lakini sasa wanafaidika na utalii japokuwa mvua za masika na janga la Corona limepunguza idadi yao.
“Kuna kempu ambazo ziko ndani ya hifadhi ambazo sisi hatuna mamlaka nazo lakini kuna kempu ambazo zimezunguka kijiji, hao wamiliki wake wanapopata wageni tunapata ushuru.
“Mwenendo wa watalii ni mkubwa kiasi kwa sababu kipindi kile tulitegemea wawe wamekuja ule msimu lakini baada ya kuonekana kuna matatizo, masika na mafuriko ya Mto Rufiji, wengine wakakatisha ziara zao,” anasema Mbiteheni.
Licha ya kupata watalii, kijiji hicho kinaendesha mradi wa kulima mboga mboga ambazo hulimwa pembezoni mwa Mto Rufiji na kutumiwa na kempu za ndani na nje ya hifadhi.
“Tuna maeneo hapa ya kulima mboga, wamiliki wa kempu walikuwa wanakuja kununua hapa lakini sasa mafuriko na tembo wanaharibu sana mashamba,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Bakari Juma.
Kutokana na kukomeshwa kwa biashara hiyo, idadi ya tembo imeanza kuongezeka hasa katika hifadhi ya Nyerere ambayo ni kivutio kikubwa cha watalii.
“Hakuna biashara ya tembo kwa sasa hivi, tembo wamekuwa wengi mpaka wanavamia katika nyumba za watu.
“Hii ni ishara tosha kuwa tembo wameongezeka na hakuna biashara ya meno ya tembo kwa sababu ingekuwepo, tembo wale wasingeweza kufika kijijini,” anasema Nambua wakati akiongea na Nukta ofisini kwake Utete Rufiji.
Baadhi ya nyara za Serikali za faru, viboko ambazo zilikamatwa wakati wa operesheni tokomeza ujangili ambazo zimehifadhiwa katika ofisi ya Halmashauri ya Rufiji. Picha|Daniel Samson.
Tembo waanza kuongezeka
Rais John Magufuli wakati akifunga Bunge la 11, Juni 16 mwaka huu alisema idadi ya tembo imeendelea kuongezeka nchini ikiwa ni matokeo ya juhudi za kupambana na ujangili dhidi ya wanyama hao.
Dk Magufuli alisema idadi ya tembo imeongezeka kutoka 43,330 mwaka 2015 hadi 51,299 mwaka 2019 ikijumuisha na wale waliopo kwenye hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Idadi hiyo ni ya chini ikilinganishwa na tembo zaidi ya 300,000 waliokuwepo nchini zaidi ya miaka 40 iliyopita, kwa mujibu wa Taasisi ya Wildlife Conservation Society (WCS).
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kuokoa Hifadhi za Taifa iliyosajiliwa nchini Uingereza inakadiriwa kuwa takriban tembo 350,000 ndiyo wamebaki duniani huku tembo 35,000 wanakadiriwa kuuwawa kila mwaka ikiwa ni matokeo ya ujangili, mitego na migogoro kati ya wanyama hao na wanadamu.
Hata wakati idadi ya tembo ikiongezeka Tanzania, kwa wakazi wa kijiji cha Mloka ni kama mkosi kwa sababu wanyama hao wamekuwa wakiwashambulia mara kwa mara na kuwaweka katika hatari ya kupoteza maisha na mali zao.
Usikose sehemu ya pili ya makala haya ambayo itaangazia kwa undani madhara yanayosababishwa na tembo katika kijiji cha Mloka na jinsi wadau mbalimbali wanavyochukua hatua kuwalinda tembo na wanavijiji.