Suluhu ya uharibifu wa mapitio ya wanyamapori Tanzania

June 30, 2022 4:15 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kushirikisha wadau wote kwenye jamii katika uhifadhi.
  • Kubuni suluhu za teknolojia na kuwekeza rasimali watu na fedha.

Morogoro. Licha ya kuwepo kwa tishio la kutoweka kwa shoroba kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu, wadau wa uhifadhi wamependekeza kutafutwa kwa suluhu ya kudumu kulinda na kuhifadhi mapitio hayo ya wanyamapori ili waendelee kuzaliana kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania. 

Shoroba ni maeneo ya mapito ya wanyamapori ambayo wanayatumia kupita kutoka sehemu moja iliyohifadhiwa kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kutafuta malisho, kuzaliana na kukidhi mahitaji ya undugu na urafiki. 

Pia wanyama hao hutumia shoroba kwa ajili ya kujihifadhi kujihakikishia usalama wao na kukimbia katika maeneo yaliyoathriwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na mafuriko.

Hata hivyo, kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo makazi, kilimo na ufugaji, athari za mabadiliko ya tabianchi katika mapitio hayo kumeibua migogoro ya mara kwa mara ya binadamu na wanyamapori ambayo imekuwa ikisababisha vifo na uharibifu wa mali. 

Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) Dk Stephen Nindi amesema shoroba bado zinahitajika kwa sababu ni sehemu muhimu kwa ajili ya maisha ya wanyamapori kuzaliana na kuendeleza vizazi vyao ili nchi iendelee kufaidika. 

“Maeneo wanayopita wanakwenda kufanya kazi muhimu ya kibaolojia na ikolojia jamii ya wanyamapori. Wanakwenda kule kuanzisha familia, kupata wachumba, wanaenda kuoa na kuolewa.

“Ili wanyama hao wasiathirike kutoka kizazi kimoja hadi kingine lazima tuhakikishe wanyama hao wanachangamana ili kuendelea kupata wanyamapori,” amesema Dk Nindi wakati wa mjadala wa mtandaoni kuhusu uhifadhi wanyamapori uliondaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania, (JET) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Amesema shoroba hizo zinasaidia wanyamapori wa maeneo mbalimbali kuchangamana na kuzaliana na kuwa na mchanganyiko wa vizazi vya aina tofauti.

Kutokana na umuhimu huo, amesema shoroba lazima ziendelee kuwepo kwa kuhakikisha zinalindwa, zinahifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya Taifa na binadamu. 

“Tunataka tuhakikishe kuna usalama wa wanyama wetu kutoka eneo moja kwenda lingine lakini wanapopita hawasababishi madhara kwa wananchi kwa sababu Serikali yoyote duniani jukumu lake ni kulinda wananchi wake lakini hawa wanyamapori ambao Mungu ametupa tuhakikishe tabia zao ambazo ni kutoka sehemu moja kwenda nyingine zinalindwa,” amesisitiza mtaalam huyo wa wanyamapori.

Shoroba husaidia wanyamapori kupata malisho, maji na makazi. Picha| Gorilla Africa.

Nini kifanyike kulinda shoroba?

Dk Nindi ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) amesema Serikali peke yake haiwezi kazi ya kulinda shoroba, bali unahitajika ushirikiano wa sekta binafasi, wananchi na wadau wa maendeleo kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha mapitio hayo ya wanyamapori hayaharibiwi. 

Amesema ushirikiano huo ujikite katika kubuni njia za kisasa za kiteknolojia, uwekezaji wa rasilimali watu na fedha ili kukomboa na kulinda shoroba hizo ambazo kwa sehemu kubwa zinatishiwa na shughuli za binadamu.

“Hii ni kazi ambayo Serikali imeona haiwezi kufanya peke yake, ni bora kushirikisha wadau mbalimbali, wananchi, sekta binafsi, waandishi wa habari kuelimisha jamii katika kuhakikisha kwamba tunazilinda, tunazikomboa na tunasimamia mapitio hayo ya wanyama,” amesisitiza mtaalam huyo. 

Kwa mujibu wa TAWIRI, Tanzania ina shoroba 52 lakini kwa sasa 44 zinafanya kazi huku zaidi ya asilimia 90 ya mapitio hayo yako kwenye ardhi inayomilikiwa na vijiji, jambo ambalo limekuwa likiibua migogoro ya mara kwa mara ya binadamu na wanyamapori.

Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dk Joseph Layson amesema kwa sasa changamoto kubwa ni migogoro kati ya wanyamapori na binadamu lakini wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali kupima ardhi ili kuhakikisha inatumiwa kwa matumizi sahihi ili kuepusha migongano isiyo ya lazima. 

““Changamoto kubwa inayoendelea ni migogoro ya wanyamapori. Kwa sasa tunaunganisha mipango ya matumizi ya ardhi kwa kizazi cha sasa na kijacho ili kuhakikisha maisha ya wanyamapori na binadamu hayaathiriwi,” amesema Dk Lyson.


Soma zaidi: 


Amesema ili kupata suluhu ya kudumu ya migogoro hiyo, wananchi wanapaswa kuelimishwa kuwa wamevamia katika shoroba za wanyamapori ili kurahisisha kazi ya  kuzifungua kuruhusu wanyama wapite.

“Lazima tuongeze ushirikiano katika ya taasisi za umma na binafsi,” amesema Dk Lyson na kubainisha kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kulinda tunu za Taifa.

Mwenyekiti wa JET, Dk Hellen Otaru aliyekuwa akiongoza mjadala huo amesema inatakiwa itafutwe njia rahisi ya kuwaelimisha na kuwashirikisha wananchi katika utunzaji na uendelezaji wa shoroba kuliko kutumia sheria pekee. 

Amesema suluhu iwe kulinda mapitio hayo ya wanyamapori kabla ya wananchi hajavamia ili kupunguza kazi ya kuwaondoa wakati athari zimetokea tayari.

Amesema pia suala la utunzaji wa mazingira unaosababishwa na kelele za shughuli za binadamu umekuwa ukiathiri maisha ya wanyamapori katika shoroba, hivyo wadau waliangalie hilo wanapotafuta suluhu ya kulinda shoroba. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW