Nyati wa Tanzania waongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 ndani ya miaka mitatu

Baadhi ya nyati wanaopatikana katika hifadhi mbalimbali za Tanzania ambao wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii. Picha| Film Crew Fixers Uganda.
- Wafikia 191,805 mwaka huu.
- Wameongezeka kwa asilimia 64 ikilinganishwa na waliokuwepo mwaka 2018.
- Kutokomezwa kwa ujangili kwachangia.
Dar es Salaam. Idadi ya nyati waliopo Tanzania imeongezeka hadi kufikia 191,805 kwa mwaka 2022 na kuiweka nchi katika nafasi nzuri ya kufaidika na fursa za utalii wa wanyamapori.
Idadi hiyo ya nyati ni sawa na ongezeka la asilimia 64 ya nyati waliokuwepo mwaka 2018.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana aliyekuwa akitangaza matokeo ya Sensa ya Wanyamapori kwa mwaka 2022 amesema idadi ya wanyamapori hao imeendelea kuongezeka zaidi katika maeneo ya ndani ya hifadhi za Taifa.
Akitangaza matokeo hayo leo Novemba 1, 2022 Jijini Arusha, Waziri Chana amesema nyati hao wanapatikana katika mifumo ikolojia ya Serengeti ambapo wapo 69,075, Nyerere-Selous-Mikumi (66,546) Katavi-Rukwa (35,273) pamoja na Ruaha-Rungwa ambapo wapo 20,911.
Licha ya kuwepo kwa changamoto za mifugo katika mifumo ya ikolojia, amesema nyati wameongezeka na hii ni kiashiria kizuri cha udhibiti wa mifugo kwenye maeneo yaliohifadhiwa.
Soma zaidi:
Lengo la sensa hiyo ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitatu katika mfumo Ikolojia wa Katavi-Rukwa na Ruaha-Rungwa ni kujua uwepo, idadi, mtawanyiko pamoja na viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori nchini Tanzania.
Akizungumzia matokeo ya sensa katika mfumo wa ikolojia wa Katavi Rukwa, Waziri Chana amesema idadi ya tembo imeendelea kuimarika na viashiria vya ujangili wa tembo vimeendelea kupungua ukilinganisha na sensa ya mwaka 2018.
Mwaka 2021, uwiano wa mizoga mipya ya tembo ilikuwa asilimia 3 wakati mwaka 2018 ilikuwa asilimia 12.
Pia katika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha- Rungwa idadi ya wanyamapori adimu kama korongo na palahala imeendelea kuongezeka.
“Korongo wameongezeka mara mbili toka korongo 1,436 mwaka 2018 hadi 3,127 kwa sensa ya mwaka 2021,” amesema Dk Chana katika taarifa iliyotolewa na wizara yake leo.
Zoezi hilo la Sensa ya Wanyamapori liliwezeshwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori (WCS) na kuratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI.
Latest