Maoni mchanganyiko bei ya petroli, dizeli ikishuka Tanzania
- Bei zimeshuka kwa viwango tofauti Juni mwaka huu.
- Ni baada ya Serikali kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni.
- Baadhi wataka bei ziendelee kushuka zaidi.
Dar es Salaam. Licha ya bei mpya za mafuta zinazoanza kutumika leo kushuka, watumiaji wa nishati hiyo kwa ajili kuendeshea vyombo vya moto wamekuwa na maoni tofauti huku baadhi wakisema bei ziendelee kushuka ili kupunguza ukali wa maisha.
Bei kikomo za petroli na dizeli za Juni 2022 zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) zinaonyesha nishati hizo zimeshuka kwa viwango tofauti baada ya Serikali kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni.
Hatua hiyo ilikuja kama mkakati wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwapunguzia maumivu Watanzania kwa sababu bei za mafuta zinaendelea kupanda duniani, jambo linaloongeza gharama za maisha.
Kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia ni matokeo ya vita kati ya Urusi na Ukraine ambayo imetatiza mifumo ya usafirishaji wa bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali duniani ikizingatiwa kuwa Urusi ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura iliyotolewa Mei 31, 2022, bei ya petroli inayopitia bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh306 kwa lita kutoka Sh3,301 hadi Sh2,994 kwa lita.
Dizeli imeshuka hadi Sh3,131 kwa lita kutoka Sh3,452 kwa lita sawa na punguzo la Sh320 huku kukiwa hakuna mabadiliko ya bei ya mafuta ya taa ambayo itabaki kuwa Sh3,299.
Neema hiyo pia ya kushuka kwa mafuta itawafaidisha watumiaji wa mikoa ya kaskazini ambao wanapokea mafuta kupitia bandari ya Tanga ambapo kwa mwezi Juni petroli inauzwa kwa Sh2,985 kwa lita ikishuka kutoka Sh3,137 kabla ya ruzuku ya Serikali.
Dizeli sasa inauzwa kwa Sh3,162 kutoka Sh3,639 kwa lita sawa na punguzo la Sh476 kwa lita.
Kwa wanaopokea mafuta kupitia bandari ya Mtwara, petroli imeshuka kwa Sh282 kwa lita huku dizeli ikishuka kwa Sh486 kwa lita.
Licha ya bei ya mafuta kushuka, Wakazi wa Serengeti mkoani Musoma wao ndiyo wananunua mafuta hayo muhimu kwa vyombo vya moto kwa bei ya juu kuliko wote nchini baada ya Ewura kubainisha kuwa bei kikomo ya petroli itakuwa Sh3,218 kwa lita.

Bei hizo ni himilivu?
Kushuka kwa bei za mafuta, kunapunguza bajeti za wamiliki wa vyombo vya moto kwa sababu hawatalazimika kutoboa zaidi mifuko yao ili kuipata nishati hiyo. Lakini bei hizo ni himilivu?
Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imeongea na madereva wa daladala, bodaboda, bajaj na watumiaji wa kawaida kujua mtazamo wao kuhusu bei hizo.
Licha ya kuipongeza Serikali kwa kupunguza bei lakini watumiaji na wamiliki wa vyombo vya moto wameomba bei zipungue zaidi ili kupunguza gharama za maisha ambazo ziliongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.
Christofa Musa ni dereva bodaboda katika kituo cha daladala cha Makumbusho jijini Dar es salaam anasema kuna unafuu kidogo tofauti na awali lakini kutokana na hali ya kipato anatamani bei ipungue zaidi.
“Sasa hivi unaweza ukaweka mafuta ya 6,000 ukapata lita mbili na pointi 76 kuna uangalau kidogo zamani ulikuwa ukiweka ya 6,000 hupati lita mbili…..tunamshukuru Raisi lakini tunaomba apunguze zaidi ili kuweza kuendana na hali yetu ya kipato,” amesema Musa.
Rodgers Mwengo, mkazi wa jijini hapa amesema Serikali imefanya vizuri kulitupia macho suala la mafuta kwa sababu bei ya mafuta huchangia bidhaa nyingine kupanda bei huku akiwa na matumaini kuwa bei ya mafuta itaendelea kushuka zaidi.
Kwa upande wake Tumaini Mchomvu amesema kupungua kwa bei ya mafuta kutaleta unafuu kwa kiasi fulani lakini bado kiwango cha bei kilichopungua ni kidogo ukilinganisha na hali ya maisha ya Watanzania walio wengi.
“Bado inahitajika Serikali iangalie kwa jicho la tatu kushusha bei ya mafuta ili kusaidia wananchi wa hali ya chini kwa sababu mafuta yanapokuwa juu vyakula huwa vinapanda……. Serikali imefanya jitihada lakini bado wafanye jitihada wasaidie bei ishuke zaidi,” amesema Mchomvu.
Soma zaidi:
-
Fursa zilizojificha uzalishaji wa michikichi Tanzania
-
Fursa ya mabilioni kilimo cha alizeti kwa vijana Tanzania
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
Unafuu gani unatarajiwa?
Unafuu unaotarajiwa kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta ni kushuka kwa kiwango cha nauli ambazo zilipanda sambamba na bei za mafuta.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Mkoa wa Iringa, Melabu Kiwele amezungumza na nukta habari (www.nukta.co.tz) kwa njia ya simu amesema jambo hilo limewapa ahueni madereva wa bajaji mkoani humo na vijana wote watafutaji.
“Nafikiri sasa abiria wategemee mabadiliko kutoka kwa madereva kwa sababu kisheria sisi ni chombo cha kukodiwa kwa hiyo bei ya kukodiwa ilikuwa juu angalau madereva bajaji watapunguza kidogo kama Serikali yetu imetujali basi na sisi lazima tuwajali abiria wetu,” amesema Kiwele.
Kwa upande wake Obeid Luhwago, Katibu wa Idara ya Barabara Taifa Chama Cha Kutetea Haki za Abiria Tanzania (CHAKUA) amesema kupungua kwa bei kutapunguza manung’uniko yaliyokuwa yanatolewa na wasafirishaji na hivyo itasaidia huduma ya usafiri kuwa wa uhakika zaidi.
“Hicho kiwango ambacho kimepungua kina unafuu kwa wasafirishaji lakini kwa upande wa abiria sisi kwa kweli baada ya Serikali kutoa maelekezo huduma ya usafiri imekuwa ikiendelea….na hakuna malalamiko ya kuongeza nauli tofauti na maagizo ya Serikali,” amesema Luhwago.
Habari hii imeandikwa na Esau Ng’umbi na Daniel Samson