Maumivu juu ya maumivu: Bei ya mafuta yaendelea kupaa Tanzania
- Petroli yapanda kwa Sh14 huku dizeli ikipanda kwa Sh324 kwa lita.
- Kupanda kwa bei ya uagizaji na maamuzi ya kisiasa vyatajwa kama sababu.
Dar es Salaam. Huenda wamiliki wa vyombo vya moto Tanzania watapata maumivu baada ya bei ya petroli na dizeli kuendelea kupanda mfululizo kwa miezi mitatu tangu Julai 2023.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) katika taarifa yake ya bei mpya za mafuta zinazoanza kutumika leo Septemba 6, 2023 imeeleza kuwa lita moja ya petroli jijini Dar es Salaam inauzwa Sh3,213 huku ya dizeli ikiuzwa Sh3,259.
Hii ina maana kuwa bei ya petroli imeongezeka kwa Sh14 kutoka Sh3,199 ya Agosti huku ya dizeli ikiongezeka kwa Sh324.
Ewura imesema kupanda kwa bei ya mafuta kumechagizwa na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia pamoja na maamuzi ya kisiasa katika nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi.
“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Septemba 2023 yanatokana na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia kwa hadi asilima 21, gharama za uagizaji wa mafuta hadi ailimia 62 na maamuzi ya kisiasa katika nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi (OPEC+),” imeeleza Ewura katika taarifa yake iliyotolewa Septemba 5.
OPEC ina wanachama 13 ikiwemo Saudi Arabia na washirika wake 10 wakiongozwa na Urusi ambapo Julai 2023 waliazimia kupunguza uzalishaji wa mafuta ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo muhimu duniani.
Maumivu ya kupanda kwa mafuta hayajaishia Dar es Salaam pekee, mikoa mingine yenye bandari kama Mtwara na Tanga nako moto ni ule ule.
Mafuta yanayopitia bandari ya Mtwara bei ya petroli imepanda kwa Sh14 na kufikia Sh3,285 kwa lita huku dizeli ikiuzwa Sh3,323 kutoka Sh3,008 ya mwezi uliopita.
Soma zaidi
-
Haya ndiyo magari 10 yanayopendwa zaidi na Watanzania
-
Yafahamu magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta
Aidha, wanaotumia mafuta yanayopitia bandari ya Tanga wao watanunua petroli kwa Sh3,259 kutoka Sh3,245 huku dizeli ikiongezeka zaidi na kufikia Sh3,305 kutoka Sh2,981.
Licha ya kupanda kwa bei ya mafuta kwa viwango tofauti, wakazi wa Ruberwa, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera wao ndio wananunua mafuta kwa bei juu kuliko maeneo mengine nchini.
Katika eneo hilo petroli inauzwa kwa Sh3,450 na dizeli Sh3,497.
Hii ina maana kuwa wakazi wa eneo hilo wananunua lita moja ya petroli kwa Sh237 juu zaidi ya wakazi wa Dar es Salaam, na Sh238 zaidi kwa lita moja ya dizeli.
Maumivu juu ya maumivu
Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, wamiliki wa vyombo moto watalazimika kutoboa zaidi mifuko yao ili kuipata bidhaa hiyo muhimu kwa shughuli za kiuchumi na usafirishaji.
Mathalani, Julai 2023, wakazi wa Dar es Salaam walitumia Sh10,000 kununua lita 3.6 za mafuta ya petroli, lakini mwezi huu pesa hiyo inanunua lita 3.1 za mafuta hayo.
Kwa watumiaji wa dizeli wa mkoa huo maumivu hayatofautiani sana na wale wanaotumia petroli ambapo kwa sasa Sh10,000 inaweza kukupatia lita 3.4 ikilinganishwa na lita 3.9 za Agosti.
Kutokana na kupanda kwa bei za mafuta mwaka 2022 kuliko changiwa na vita kati ya Ukraine na Urusi, Mei mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilitangaza kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni katika bidhaa hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi kila mwezi ili kuwapunguzia Watanzania ukali wa maisha.
Hata hivyo, iliondolewa Januari 2023 baada ya bei za mafuta kuanza kupungua.
Latest
