Ni zaidi ya maumivu: Bei ya petroli, dizeli yazidi kupaa Tanzania
- Bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka hadi Sh3,148 kwa lita.
- Bei mpya ya dizeli ni Sh3,258 kwa lita ikiwa imepanda kwa Sh2,692.
- Gharama za usafiri na kuongezeka kwa bei ya dunia kwachangia.
Dar es Salaam. Unaweza kusema ni maumivu juu ya maumivu kwa watumiaji wa mafuta nchini Tanzania kwa sababu watalazimika kutoboa mifuko yao zaidi baada ya mafuta ya petroli kuongezeka kwa zaidi Sh287 kwa lita ndani ya mwezi mmoja.
Katika bei mpya za rejereja zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) bei petroli jijini Dar es Salaam imepanda hadi kufikia Sh3,148 kwa lita kutoka Sh2,861 iliyokuwa ikitumika Aprili 2022 ikiwa ni ongezeko la Sh287.
Wakazi wa Serengeti mkoani Musoma wao ndiyo wananunua mafuta hayo muhimu kwa vyombo vya moto kwa bei ya juu kuliko wote nchini baada ya Ewura kubainisha kuwa bei kikomo ya petroli itakuwa Sh3,372 kwa lita.
Taarifa ya Ewura iliyotolewa jana Mei 3, 2022 imeeleza kuwa kupanda kwa bei za mafuta kumetokana na ongezeko la bei za mafuta katika soko la dunia zinazochangia takribani asilimia 93 ya ongezeko la bei hizo na gharama za uagizaji (premium) ambazo zinachangia takribani asilimia nne.
Kuendelea kupanda kwa bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa kulitegemewa kutokana na vita inayoendelea sasa kati Urusi na Ukraine ambayo imetatiza mifumo ya usafirishaji nishati hizo duniani. Urusi ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani.
Bei mpya za rejareja za dizeli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Mei ni Sh3,258 kwa lita ikiwa imepanda kutoka Sh2,692 iliyotumika mwezi uliopita, sawa na ongezeko la Sh566.
Maumivu hayo yatawapata pia watumiaji wa mafuta ya taa ambapo bei imepanda kutoka Sh2,682 hadi Sh3,112 kwa lita kwa mafuta yanayopitia Dar es Salaam.
“Bei za bidhaa hiyo kwa mikoa yote nchini zimekokotolewa kulingana na gharama za kupokelea mafuta hayo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka miji husika,” imeeleza Ewura kuwa bei ya taa katika maeneo mengine ya Tanzania itategemea bei za Dar es Salaam.
Kupanda kwa bei za mafuta, kunaongeza bajeti za wamiliki wa vyombo vya moto kwa sababu wanalazimika kutoboa zaidi mifuko yao ili kuipata nishati hiyo, jambo linaloweza kuongeza ugumu wa maisha.
Zinazohusiana:
- Funga mkanda: Maumivu bei ya mafuta kuendelea Tanzania
- Mifuko kutoboka zaidi kwa wamiliki wa magari, petroli ikipanda
- Ahueni bei ya petroli ikishuka Tanzania
Maumivu hadi Mtwara na Tanga
Maumivu ya mafuta pia yatawagusa watumiaji wa nishati hiyo wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, inayopokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda.
Lita moja ya petroli inauzwa kwa Sh3,161 kutoka Sh2,848, dizeli bei imeongezeka kutoka ShSh2,779 hadi Sh3,264 kwa lita moja.
Bei pia zimepanda kwa mafuta ambayo yanapitia Bandari ya Mtwara. Petroli itauzwa kwa Sh3,177 kutoka Sh2,678 kwa lita moja.
Bei ya dizeli kwa lita moja itakuwa Sh3,309 kutoka Sh2,530 ya mwezi Aprili.
Tangazo:

Ili kuwapunguzia maumivu wamiliki na mabasi ya mikoani na daladala, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ilitangaza kupandisha nauli kikomo ambazo zitaanza kutumika katikati ya mwezi huu.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamelalamika kuwa mabadiliko ya nauli na bei za mafuta zinamuumiza zaidi mtumiaji wa mwisho ambaye ni Mtanzania wa kawaida.
“Tunaiomba Serikali iangalie namna ya kutupatia ahueni maana kila kitu kimepanda bei maisha yanazidi kuwa magumu. Ni kweli bei zimepanda duniani kote lakini itafute suluhu itakayotatua changamoto hiyo nchini,” amesema Henry Mwandu, mkazi wa Bunju, jijini Dar es Salaam.
Latest
