Bei ya petroli, dizeli yashuka baada ya kupaa kwa miezi miwili mfululizo

September 7, 2022 7:17 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeshuka Septemba kwa viwango tofauti.
  • Alikuwa ikipanda mfululizo tangu Julai mwaka huu.
  • Kushuka bei ya dunia na ruzuku ya Serikali vyachangia kushusha bei. 

Dar es Salaam. Baada ya bei ya mafuta kupanda kwa miezi miwili mfululizo, hatimaye wamiliki wa vyombo vya moto watapata ahueni kidogo kutokana na bei ya nishati hiyo kushuka kwa viwango tofauti Septemba 2022.

Bei za dizeli, petroli na mafuta ya taa zilikuwa zikipanda mfululizo tangu Julai mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine na kupanda kwa nishati hiyo katika soko la dunia. 

Licha ya Serikali kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni kwa baadhi ya miezi, bado watu wamekuwa wakilalamika kuwa bei hizo ziko juu na zinachangia kuongeza ukali wa maisha. 

Hata hivyo, maumivu hayo ya miezi miwili yanaweza kupungua kidogo mwezi huu baada ya bei ya petroli na dizeli kushuka kwa viwango tofauti.

Kwa mujibu wa bei kikomo za mafuta zinazoanza kutumika leo Septemba 7, 2022 zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), wakazi wa Dar es Salaam wananunua petroli kwa Sh2,969 kwa lita moja kutoka Sh3,410 iliyokuwa ikitumika Agosti mwaka huu. 

Dizeli inauzwa kwa Sh3,125 kutoka Sh3,322 ya mwezi uliopita huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh3,335 kwa lita kutoka Sh3,765 kwa lita.

Hiyo ina maana kuwa ikiwa mtu ana Sh10,000 akienda katika kituo cha mafuta atapata lita 3.4 za mafuta ya petroli huku dizeli akipata lita 3.2. 

Licha ya bei hizo kushuka, wakazi wa Ruberwa, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ndiyo wananunua petroli kwa bei ya juu kuliko maeneo mengine nchini. Bei ya petroli katika eneo hilo ni Sh3,206 kwa lita moja. 

Ahueni hadi mikoani

Kwa mikoa inayotumia mafuta yanayopitia bandari ya Tanga ikiwemo Kilimanjaro na Arusha, nako wanafurahia kushuka kwa bei ya mafuta ambapo petroli wananunua kwa Sh3,033 kwa lita kutoka Sh3,435.

Dizeli inauzwa kwa Sh3,131 kutoka Sh3,349.

Petroli inayopitia bandari ya Mtwara sasa inauzwa Sh3,082 kwa lita huku dizeli ikiuzwa kwa Sh3,213.

 

Mambo yaliyochangia bei kushuka

Mkurungenzi Mkuu wa Ewura, Modestus Lumato amesema kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kumechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa bei za mafuta nchini Septemba. 

“Bei za Mafuta katika soko la dunia za Julai 2022 zimepungua ikilinganishwa na bei hizo kwa Juni 2022. Hivyo, bei za mafuta katika soko la ndani zimepungua vilevile kwa kati ya shilingi 271/lita na shilingi 362/lita kwa petroli na kwa shilingi 430/lita kwa mafuta ya taa ukilinganisha na bei zenye ruzuku za Agosti 2022,” amesema Lumato  katika taarifa yake iliyotolewa jana. 

Kuhusu mafuta ya dizeli, amesema “ukiiacha bei ya Tanga ambayo inashuka kwa Sh13 kwa lita, bei za Septemba 2022 zimeongezeka kwa Sh37 kwa lita na Sh86 kwa lita kwa Dar es Salaam na Mtwara, sawia, ukilinganisha na bei zenye ruzuku za Agosti 2022.”

Amesema ili kuendelea kupunguza madhara ya ongezeko la bei za dizeli hapa nchini ambapo shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea dizeli na pia ili kupunguza tofauti kati ya bei za petroli na dizeli, Serikali imetoa ruzuku ya Sh65 bilioni ili kupunguza bei za mafuta Septemba 2022. 

 “Kwa kutoa ruzuku hiyo, Serikali imepunguza bei za bidhaa za mafuta kwa mwezi Septemba 2022,” amesisitiza.


Soma zaidi:


Bei za mafuta ni himilivu?

Licha ya bei za mafuta kushuka Septemba, baadhi ya wananchi wakiwemo madereva wamesema bado zipo juu, hivyo wangependa kuona zinashuka zaidi ili kuwapunguzia makali ya maisha yanayosababishwa na nishati hiyo.

“Tunashukuru kwa jitihada za Serikali kushusha bei ya mafuta lakini iende mbali zaidi zishuke jamani maisha magumu kwa sasa,” amesema Abdallah Mbotea, dereva daladala jijini Dar es Salaam.

Wananchi wengine wameiomba Serikali kushusha nauli za daladala na mabasi ya mikoani ili nao wapate ahueni ya maisha. 

Mtumiaji wa Twitter, Handsome La Kijiji  @ManenoIzaak amesema “hakuna faida ya kushuka bei mafuta then (halafu)  nauli zikabaki kama zilivyo , bado mzigo ni mzito kwa wananchi wa hali ya chini.”

“Tuwapongeze EWURA mafuta yameshuka bei jamani, nauli nazo zishuke sasa watu wanaumia sana huko mtaani,” amesema Adventure-360 @Adventure_36 katika andiko lake la Twitter. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW