Funga mkanda: Maumivu bei ya mafuta kuendelea Tanzania
- Ni baada ya Rais kuagiza kurejeshwa kwa tozo ya Sh100 ya mafuta iliyokuwa imeondolewa
- Aagiza viongozi kuwaeleza wananchi sababu za kuendelea kupanda kwa bei za mafuta
Dar es Salaam. Kuna kila dalili kuwa watumiaji wa mafuta Tanzania wakaendelea kupata maumivu zaidi ya baada ya Rais Samia Suluhu kuagiza kurejeshwa kwa tozo ya Sh100 iliyotolewa kwenye bei ya mafuta nchini.
Uamuzi huo wa Rais Samia alioutoa leo Machi 30 jijini Dodoma sasa utafanya bei mpya za mafuta kujumuisha Sh100 kwenye kila lita ambayo iliondolewa mwishoni mwa Februari mwaka huu na Waziri wa Nishati, Januari Makamba ili kupunguza makali ya kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.
“Tumekaa kama Serikali tumerekebisha, ile Shilingi (100) iliyotoka nimeagiza irudishwe,” amesema Rais Samia wakati akipokea Ripoti ya 2020/21 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuongeza kuwa tozo hiyo ilitolewa lakini ilikuwa tayari kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge.
Kutolewa kwa tozo hiyo, Rais Samia amesema bado kusingeleta ahueni kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta duniani na zaidi kungeendelea kukosesha Serikali mapato inayokusanya.
Kurudishwa kwa Sh100 kwenye bei ya mafuta nchini kutaendelea kutoboa mifuko ya wanunuzi wa mafuta nchini ambapo kwa sasa wakazi wa jijini Dar es Salaam wananunua lita moja ya petroli kwa Sh 2,540 wakati wale wa Uvinza mkoani Kigoma wakinunua kwa Sh2,884 kwa lita.
Iwapo bei za mafuta zitabaki kiwango cha sasa kwa mwezi April 2022 hii ina maana watumiaji wa vyombo vya moto Dar es Salaam watanunua lita moja kwa Sh2,640 wakati wale wa Uvinza watanunua kwa Sh2,984.
Zinazohusiana:
-
Mifuko kutoboka zaidi kwa wamiliki wa magari, petroli ikipanda
-
Ahueni bei ya petroli ikishuka Tanzania
Bei ya mafuta imeendelea kupanda katika soko la dunia katika miezi ya hivi karibuni kutoka Dola za Marekani 79.86 (Sh183,678) kwa pipa Desemba 30, 2021 hadi Dola za Marekani 114.27 (Sh262,821) Machi 30 mwaka huu kwa mujibu wa tovuti ya Tradingeconomics huku vita ya Urusi na Ukraine ikichochea zaidi hali hiyo baada ya kuathiri mfumo wa ugavi wa nishati hiyo.
Kuongezeka kwa bei ya mafuta kutapeleka zaidi maumivu kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri vilevile kunasababisha kuongezeka kwa gharama za usafirishaji.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilieleza mapema Machi 2022 kuwa bei za petroli na dizeli ziliongezeka kwa Sh60 na 65 kwa lita mtawalia katika jiji la Dar es Salaam kutoka bei zilizorekodiwa Februari mwaka huu.
Katika mikoa ya kaskazini ikiwemo Arusha na Kilimanjaro bei hizo ziliongezeka kwa Sh165 na Sh207 kwa petroli na dizeli mtawalia, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya ongezeko la Dar es Salaam.
Wakazi wa mikoa ya kusini wenyewe katika Machi 2022 walilazimika kununua petroli na dizeli kwa Sh43 na Sh105 kwa lita mtawalia kiwango ambacho ni juu zaidi ya bei ya walizonunua Februari.
Kutokana na kuendelea kuongezeka kwa bei ya mafuta duniani, Rais Samia amesema kuwa ni muhimu kwa viongozi kuwaelewesha Watanzania mambo yanayochangia kupanda kwa bei hizo ikiwemo vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
“Waambieni wananchi ukweli vita ya Russia (Urusi) na Ukraine imepandisha sana bei ya mafuta na mafuta yanapopanda kila kitu kitapanda, nauli zitapanda, usafirishaji wa bidhaa utapanda…..wasikae tu kulaumu Serikali,” amesema Rais Samia.
Latest



