Mambo magumu: Bei ya petroli, dizeli yazidi kupaa Tanzania

April 6, 2022 5:48 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka hadi Sh2,861 kwa lita.
  • Bei mpya ya dizeli itakuwa Sh2,692 kwa lita ikiwa imepanda kwa Sh289 kutoka Sh2,403 ya sasa.
  • Vita ya Urusi na Ukraine yachangia kupaisha bei.

Dar es Salaam. Watumiaji wa mafuta nchini Tanzania watalazimika kutoboa mifuko yao zaidi baada ya mafuta ya petroli kuongezeka kwa zaidi Sh300 kwa lita ndani ya mwezi mmoja na kufikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka 13 iliyopita. 

Katika bei mpya za rejereja zilizotangazwa leo na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) bei petroli jijini Dar es Salaam imepanda hadi kufikia Sh2,861 kwa lita kutoka Sh2,540 iliyokuwa ikitumika Machi 2022 ikiwa ni ongezeko la Sh321. 

Wakazi wa Uvinza mkoani Kigoma wao ndiyo watanunua mafuta hayo muhimu kwa vyombo vya moto kwa bei ya juu kuliko wote nchini baada ya Ewura kubainisha kuwa bei kikomo ya petroli itakuwa Sh3,105 kwa lita.

Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Gerald Maganga amewaambia wanahabari jijini Dodoma leo (Aprili 5, 2022) kuwa kupanda kwa bei hizo kumesababishwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mafuta duniani kulikochagizwa na vita ya Urusi na Ukraine.

Kupanda kwa bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa kulitegemewa kutokana na vita inayoendelea sasa kati Urusi na Ukraine ambayo imetatiza mifumo ya usafirishaji nishati hizo duniani. Urusi ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani.

Ewura imeeleza kuwa bei mpya kikomo za rejareja za dizeli kwa Aprili 2022 iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia Aprili 6 itakuwa Sh2,692 kwa lita ikiwa imepanda kwa Sh289 kutoka Sh2,403 ya sasa.


Zinazohusiana: 


Maumivu hayo yatawapata pia watumiaji wa mafuta ya taa ambapo bei imepanda kutoka Sh2,208 hadi Sh2,682 ikiwa ni ongezeko la wastani wa Sh474.

“Hali hiyo imesababishwa na mgogoro wa kivita uliopo kati ya Urusi na Ukraine. Mgogoro huu umepelekea kuwepo kwa uhaba wa upatikanaji wa mafuta duniani na pia gharama za usafirishaji kupanda,” amesema Maganga. 

Amesema Tanzania siyo nchi pekee inayoshuhudia ongezeko la mafuta bali karibu kila nchi inapitia changamoto hiyo.

Maumivu hayo pia yatawagusa watumiaji wa nishati hiyo wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, inayopokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda. 

Lita moja ya petroli itauzwa kwa Sh2,848 kutoka Sh2,563, dizeli bei itaongezeka kutoka Sh2,484 hadi Sh2,779 ikiwa ni ongezeko la Sh295 kwa lita moja.


Tangazo:


Bei pia zimepanda kwa mafuta ambayo yanapitia Bandari ya Mtwara. Petroli itauzwa kwa Sh2,678 kwa lita moja kutoka Sh2,577 ikiwa ni ongezeko la Sh100.

Bei ya dizeli kwa lita moja itakuwa Sh2,811 kutoka Sh2,530.

Bei hizo zimejumuisha tozo ya Sh100 ambayo Serikali ilitangaza kuiondoa mwezi Machi, 2022 kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kuirejesha wiki iliyopita akieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa kinyume na taratibu za kibajeti na itapunguza mapato serikalini.

Bei hizi mpya zilizotangazwa leo ndiyo za juu kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka 13 iliyopita. Mfano, takwimu za Ewura zinabainisha kuwa bei kikomo ya mafuta ya petroli Machi 2009 jijini Dar es Salaam ilikuwa Sh1,361 kwa lita huku dizeli ikiwa Sh1,301. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW