Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji

Rodgers George 0816Hrs   Septemba 11, 2018 Teknolojia
  • Ni kile kinachotumia mfumo wa matone kinachopunguza upotevu wa maji na kuongeza mavuno.
  • Wakulima wengi bado wanalima kilimo cha kienyeji cha umwagiliaji.

Dar es Salaam. Licha ya watanzania wengi kuchangamkia kilimo cha umwagiliaji kama njia ya kujipatia kipato, bado wanakabiliwa na changamoto ya kulima kienyeji ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya maji na miundombinu duni ya umwagiliaji, jambo linalowakwamisha kufaidika na kilimo hicho.

Inakadiriwa kuwa hekta 461,000 sawa na asilimia 5 ndiyo zinatumika kwa kilimo cha umwagiliaji kati ya hekta 29.4 milioni zilizopo kutokana na kilimo cha mazoea na uwekezaji mdogo unaofanywa kwenye sekta hiyo

Hata wakulima wanaolima kienyeji bado wanakabiliwa na changamoto ya matumizi mabaya ya maji ikiwemo upotevu wa kiasi kikubwa cha maji kinachopotea kwasababu ya kukosa miundombinu ya kisasa kusimamia maji na ukuaji wa mazao.

Kutokana na changamoto hizo, kampuni ya vifaa vya umwagiliaji ya Vishakha kutoka India imekuja na teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya matone ambayo inaweza kuwa mkombozi kwa wakulima wa Tanzania wenye nia ya kuendeleza sekta ya umwagiliaji nchini.

Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kuboreshwa ikiwa wakulima watapewa teknolojia ya kisasa. Picha| Wikipedia.

Mshauri wa maendeleo ya Biashara kutoka kampuni hiyo, Mayur Parikh amesema teknolojia ya matone inasaidia kuondokana na changamoto za kilimo cha mazoea cha kutumia maji mengi bila kuzingatia mahitaji ya mimea.

“Ni vyema tutumie maji kwa ufanisi katika kilimo cha umwagiliaji kwa maslahi ya kilimo,” amesema Parikh.

Tofauti na mashine zingine za umwagiliaji, mashine za Vishakha humwagilia maji kwa mfumo wa matone hasa kwa mazoa yanayolimwa kwa ukaribu kama miwa, mboga mboga, pamba, ndizi na maua kwa kuunganisha mpira wenye matundu yanayopitisha maji moja kwa moja kwenye shina la mmea.

Kwa kutumia vifaa hivyo, mkulima huweza kutumia kiasi kidogo cha maji kwa siku na hivyo kuepusha gharama za umeme kama anatumia pampu ya kurusha maji shambani. Pia anaokoa muda wa kukaa shambani kwa muda mrefu na kumpa nafasi ya kufanya shughuli zingine za uzalishaji.

Parikh anabainisha kuwa umwagiliaji wa matone unatoa uhakika wa mazao kupata maji ya kutosha na kukua kwa wakati na kumpatia mkulima mazao yanayoendana na gharama za uzalishaji.

Related Post