Magufuli awateua Prof Kabudi, Dk Mpango kuingia baraza jipya la mawaziri

November 13, 2020 5:21 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Walikuwa ni mawaziri katika baraza la mawaziri lililopita.
  • Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa inaeleza kuwa uteuzi wa mawaziri hao unaanza Novemba 13, 2020.
  • Walikuwa ni nguzo muhimu ya ukusanyaji wa mapato na utatuzi wa migogoro mbalimbali. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewateua Dk Philip Mpango kuwa Waziri Fedha na Mipango na Prof Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikiwa ni uteuzi wa kwanza kabisa katika baraza la mawaziri jipya katika kipindi cha muhula wa pili wa uongozi wake.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa inaeleza kuwa uteuzi wa mawaziri hao unaanza Novemba 13, 2020.

“Mawaziri hao wateule walikuwa wakishika nyazifa hizo katika baraza la mawaziri lililopita,” Msigwa ameeleza kwenye taarifa hiyo.

Dk Mpango anafahamika kwa kuisaidia Serikali ya Rais Magufuli kuongeza ukusanyaji wa mapato yanayosaidia kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya nishati na uchukuzi kama reli ya kisasa (SGR) na bwawa kubwa la kuzalisha umeme la Nyerere la Megawati 2,115 linaloendelea kujengwa.

Waziri huyo anaingia katika baraza hilo la mawaziri kama mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma ikiwa ni tofauti na alivyoingia Desemba 2015 kama mbunge wa kuteuliwa na rais.


Zinazohusiana:


Prof Kabudi yeye amekuwa moja ya nguzo muhimu katika majadiliano ya kutatua migogoro mbalimbali kati ya Serikali na makampuni ya kimataifa.

Miongoni mwa migogoro aliyeshiriki kufanikisha makubaliano ni ule kati ya Serikali na iliyokuwa kampuni ya madini ya Acacia ambapo kwa sasa Serikali ina asilimia 16 ya hisa katika kampuni mpya ya madini ya Twiga Minerals Corporation na ilipata Dola za Marekani milioni 300 kutoka kwa kampuni mama ya Barrick.

Prof Kabudi naye anaingia katika baraza hilo la mawaziri kama mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la Kilosa mkoani Morogoro ikiwa ni tofauti na alivyoingia Desemba 2015 kama mbunge wa kuteuliwa na rais.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW