Rais Samia ateua mawaziri wapya wanne, atengua watatu
- Ameteua mawaziri wanne akiwemo January Makamba.
- Ametngua uteuzi wa mawaziri watatu akiwemo Dk Kalemani wa Nishati.
- Amemteua Dk Eliezer Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kutengua uteuzi wa mawaziri watatu akiwemo Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.
Makamba, aliwahi kuwa Waziri wa Mazingira na Muungano tangu kuingia madarakani kwa Hayati Rais John Pombe Magufuli lakini Juni 2019 aliondolewa katika nafasi hiyo.
Tangu wakati huo Makamba hukushika nafasi yoyoye ya uwaziri hadi leo alipoteuliwa na Rais Samia.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Jaffar Haniu leo Septemba 12, 2021 imeeleza kuwa Rais Samia amemteua Dk Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Dk Kijaji ambaye ni Mbunge wa Kondoa Vijijini na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango anachukua nafasi ya Dk Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Pia Rais ameihamisha idara ya Habari katika Wizara itakayoingoza Dk Kijaji kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Prof Mbarawa anachukua nafasi ya Mhandisi Dk Leonard Chamuriho ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Dkt. Stergomena Tax ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Dkt. Tax ambaye Septemba 10, 2021 aliteuliwa na Rais kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania anachukua nafasi ya iliyoachwa wazi na mtangulizi wake marehemu Elias Kwandika.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Tax alikuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye amemaliza muda wake mwezi Agosti mwaka huu.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Dk Eliezer Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Anachukua nafasi ya Prof Adelardus Kilangi ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
Kabla ya uteuzi huo Dk Feleshi alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Latest
