Rais Samia afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri, wawili watemwa, Lukuvi, Kabudi waula

August 14, 2024 10:43 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wawili watemwa baraza la mawaziri, mmoja ateuliwa kuwa mshauri wa Rais. 
  • Awarudisha Palamagamba Kabudi na William Lukuvi baada ya kukaa nje ya baraza kwa miaka miwili.
  • Viongozi wateule kuapishwa kesho saa nane mchana.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri kwa kuwaondoa mawaziri wawili, kuhamisha mawaziri wawili, na kumteua Mwanasheria Mkuu Mpya wa Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk Moses Kusiluka na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Sharifa Nyanga, Rais Samia amemteua Prof. Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi ya Balozi Dk. Pindi Chana aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Hii ni mara ya tatu kwa Kabudi kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria ambapo amehudumu nafasi hiyo kati ya mwaka 2017 hadi 2019 na 2021 mpaka 2022 alipoondolewa kwenye baraza la mawaziri na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, taarifa ya Ikulu imebainisha kuwa Rais Samia amemteua William Lukuvi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) akichukua nafasi ya Jenista Mhagama.

Lukuvi anarejea kwenye baraza la mawaziri mara baada ya kukaa nje ya baraza kwa muda wa miaka miwili akiwa mshauri wa Rais katika masuala ya siasa.

Mara ya mwisho Lukuvi alihudumu katika baraza hilo kama Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wizara aliyohudumu kwa zaidi ya miaka 10.

Hata hivyo, Rais Samia amemteua Jenista Mhagama kuwa Waziri wa Afya akichukua nafasi ya Ummy Mwalimu ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Kwa mara ya kwanza Ummy atakaa nje ya baraza la mawaziri mara baada ya kuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja akihudumu kama naibu waziri kwa miaka minne na waziri kamili katika wizara mbalimbali kwa miaka tisa.

Mwingine aliyeondolewa kwenye baraza la mawaziri ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki ambaye nafasi yake imechukuliwa na Balozi Dk Pindi Chana, huku yeye akiteuliwa kuwa Mshauri wa Rais.

Uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Taarifa ya Ikulu imeongeza kuwa Rais Samia amefanya Uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Jaji wa Mahakama ya Rufani.

“Bw. Hamza Johari ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kabla ya uteuzi huu, Bw. Johari alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani,” imebainisha taarifa hiyo.

Aidha, Samwel Maneno ameteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Balozi Prof. Kennedy Gastorn ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Sheria na Mikataba ambapo Kabla ya uteuzi huo Maneno alikuwa Msaidizi wa Rais, Sheria.

Wakati huo huo Rais Samia amemteua Dk. Ally Saleh Possi kuwa Wakili Mkuu wa Serikali ambapo kabla ya uteuzi huo, Dk Possi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi.

Wakuu wa taasisi wapya

Katika hatua nyingine inayotafsiriwa kama kuimarisha utendaji kazi wa taasisi za umma Rais Samia amewateua Crispin Chalamila kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CPA. Moremi Andrea Marwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Dk Irene Isaka ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, uapisho wa mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Jaji wa Mahakama ya Rufani, na Wateule wengine wa Rais kama Katibu Tawala wa Mkoa na Naibu Makatibu Wakuu wateule utafanyika Ikulu Dar es Salaam kesho tarehe 15 Agosti, 2024 saa 8.00 mchana.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW