Ni panga, pangua: Rais Samia afanya mabadiliko baraza la mawaziri Tanzania
- Awabadilisha baadhi ya mawaziri na kuingiza wapya akiwemo mwanadiplomasia mahiri Tanzania, Balozi Liberata Mulamula.
- Mabadiliko hayo hayakutegemewa na wengi kiasi ya kufanya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kuyaita ni “Surprise”.
- Awataka walioteuliwa kufanya kazi kwa bidii na kuepuka ugomvi kwenye majukumu yao.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuwabadilisha baadhi ya mawaziri na kuingiza wapya akiwemo mwanadiplomasia mahiri Tanzania, Balozi Liberata Mulamula.
Katika mabadiliko hayo aliyoyatangaza mubashara leo Machi 31, 2021 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuapishwa kwa Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Rais Samia pia amemteua Mulamula kuwa mbunge ikiwa ni sehemu ya nafasi zake 10 alizopewa kisheria.
Baraza hilo lilianza kufanya kazi katika Serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu kutokana na maradhi ya moyo.
Hata hivyo, kwenye mabadiliko ya leo Rais Samia hajamuondoa waziri wala naibu waziri zaidi ya kuwabadilisha wizara na kuongeza wawili.
Mabadiliko ya ‘Surprise’
Mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri hayakutegemewa na wengi kiasi ya kufanya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kuyaita ni “Surprise” (yenye kushangaza).
“Ninaomba mtulie viroho visiwananii, maana nimeona nyuso zimeshabadilika, vifua vinapiga vikubwa hivi, naomba tulieni sikuacha mtu,” amesema Rais huyo wa kwanza mwanamke Tanzania kabla ya kutangaza mabadiliko hayo.
Katika kujaza nafasi ya waziri wa fedha baada ya Dk Mpango kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, Rais Samia amemteua Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Sasa Nchemba, aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba kabla ya uteuzi huo mpya, anarudi katika wizara ya fedha ambayo aliwahi kuitumikia kama naibu waziri wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Nchemba ambaye ni mchumi kitaaluma atasaidiana na Hamad Masauni aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango akichukua nafasi ya Mwanaidi Hamis aliyehamishiwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Hamis atakuwa anashughulikia masuala ya maendeleo ya jamii na wanawake chini ya waziri wake Dorothy Gwajima aliyebakizwa katika wizara hiyo ya afya pamoja naibu waziri Godwin Mollel.
Waziri Gwajima na Mollel wamekuwa maarufu siku za hivi karibuni mtandaoni kutokana na kuhamasisha watu kujifukiza (nyungu) kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona na magonjwa mengine ya kupumua.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiagana na Makamu wa Rais Dk Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge Job Ndugai, baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma. Picha| Ikulu.
Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Sheria na Katiba akichukua nafasi ya Nchemba.
Prof Kabudi anarejea katika wizara ambayo alianzia safari yake katika baraza la mawaziri baada ya kuteuliwa na hayati Magufuli mwaka 2017 kabla ya kupelekwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabudi ambaye ni Mbunge wa Kilosa mkoani Morogoro atasaidiwa na Naibu Waziri Geofrey Pinda ambaye alikuwepo kwenye wizara hiyo kabla ya mabadiliko.
Prof Kabudi alikuwa moja ya watu walioaminiwa zaidi na Hayati Magufuli baada ya kupewa majukumu ya kufanya majadiliano na utatuzi wa migogoro ya kimataifa ukiwemo wa kampuni ya madini Barrick na Serikali uliochukua zaidi ya miaka miwili kumalizika.
Jafo ahamishwa Tamisemi
“Ofisi ya Rais Tamisemi waziri wangu atakuwa Ummy Ally Mwalimu na Naibu Waziri watabaki wale wale Festo John Dugange na David Silinde,” amesema Rais Samia.
Ummy amebadilishana wizara na Selemani Jafo ambaye sasa anakuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Naibu W
aziri wake anakuwa Hamad Hassan Chande ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kojani visiwani Zanzibar.
Huenda, Jafo kubadilishiwa wizara kumetokana na onyo alilopewa na Rais Samia Machi 28 mwaka huu kuwa Tamisemi imekuwa ikitumia fedha nyingi za Serikali bila kufuata sheria na kama waziri huyo ameshindwa kusimamia wizara yake aseme ili “asaidiwe”.
Soma zaidi:
- Rasmi: Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
Katika Ofisi ya Utumishi na Utawala Bora, Waziri atakuwa Mohammed Omar Mchengerwa na Naibu Waziri anabakia Degratious Ndejebi na Mwita Waitara.
Rais Samia amesema aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo George Mkuchika anabaki kuwa waziri ndani ya Ofisi ya Rais na anampa kazi maalumu.
Aidha, Mama Samia ambaye aliapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka huu, ameitoa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais inayoshughulikia Uwekezaji na sasa itakuwa inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji ameteuliwa Geofrey Mwambe na Naibu Waziri wake ni William Tate Olenasha ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mwambe ambaye awali alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara nafasi yake imechukuliwa na Kitila Mkumbo na Naibu Waziri wake atabakia kuwa Exaud Kigahe.
Rais Samia amewataka walioteuliwa kusimamia uwekezaji, kuunda upya wizara hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu na ianze kufanya kazi na kubainisha kuwa “venginevyo mnanionyesha kwamba hamjui mnalotakiwa kufanya ndani ya wizara hii.”
“Michezo (Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Waziri ni Innocent Bashungwa na naibu wake atakuwa Pauline Gekul. Nimemtoa Ulega kwenye michezo nimemrudisha kwenye mifugo na uvuvi kwa sababu alikuwa kule na amefanya kazi huko aende akamsaidie waziri kule,” amesema Mama Samia.
Abdallah Ulega ambaye nafasi yake imechukuliwa na Gekul aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wakati wa Hayati Dk Magufuli amerudi tena katika wizara hiyo na atafanya kazi na Waziri Mashimba Ndaki.
Aidha, wizara zingine ikiwemo Wizara ya Elimu, Wizara ya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari, Wizara ya Maliasili na utalii zimebaki kama zilivyokuwa na hakuna mabadiliko yoyote.
Ikumbukwe kuwa baraza la mawaziri la Tanzania lina Mawaziri 23 ambao wanafanya kazi katika wizara mbalimbali.
Amesema mabadiliko aliyoyafanya leo ni mwanzo tu lakini mabadiliko mengine yatategemea utendaji wao na yataamua nani wamuache na nani aendelee kuwepo katika baraza lake.
Makamu wa Rais Dk Philip Isdor Mpango akiapa katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma Leo Machi 31, 2021. Picha| Msemaji Mkuu wa Serikali.
Atoa Maagizo mazito kwa wateuliwa
Baada ya Rais Samia kutangaza mabadiliko hayo, ametoa maagizo mazito kwa walioteuliwa na wale wanaondelea katika nafasi zao za uwaziri kuwa wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii kwa mujibu wa sheria.
“Niwaombe sana mkafanye kazi zenu kila mmoja kwa wizara yake kila mmoja na pahali pake mkafanye kazi zenu,” amesema.
Pia amehimiza ushirikiano miongoni mwa mawaziri hasa katika mgawanyo wa majukumu ili kuwatumikia vizuri Watanzania.
“Alivyosema Hayati Dk Magufuli manaibu mawaziri wakatumike vizuri, mna mtindo huwa hamuwapangii kazi kuna kudharauliana na hata sasa hivi nina baadhi ya kesi manaibu wanadharau waziri wao, waziri anadharau naibu.
“Nimesema tunaanza hii katika awamu ya sita dharau zikiendelea basi tutajua cha kufanya huko mbele. Ninachotaka ni kazi. Ni kazi, ni kazi na sitaki kusikia kingine kwa hiyo ndugu zangu naomba mkachape kazi,” amesema Rais Samia.
Baada ya mabadiliko hayo yaliyofanyika leo, mawaziri na manaibu waziri walioteuliwa katika wizara mpya wataapishwa kesho Aprili 1 Ikulu mkoani Dodoma.
Hata hivyo, Rais Samia amemteua Balozi Hussein Kattanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi akichukua nafasi ya Dk Bashiru Ally aliyeteuliwa kuwa mbunge. Kattanga, mbali na majukumu mengine atakuwa akifanya kazi kama Katibu wa baraza hilo.
Habari hii imeandikwa na Daniel Samson na Rodgers George.
Latest
