Rais Samia aeleza sababu kutengua uteuzi mawaziri watatu
Mawaziri wapya walioteuliwa jana wakiapa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) Ikulu, Chamwino, jijini Dodoma. Picha| Ikulu tanzania.
- Ni Dk Kalemani, Dk Ndungulile na Mhandisi Dk Chamuriho.
- Amesema ametumia miezi sita akisoma utendaji wao.
- Amesema mabadiliko mengine ya mawaziri yaja.
Dar es Salaam. Huenda utendaji usioridhisha wa mawaziri watatu akiwemo Dk Medard Kalemani wa Nishati ndiyo sababu iliyofanya teuzi zao zitenguliwe baada ya Rais Samia kusema “kuna watu waliichukulia hii Serikali poa, watu wakafanya wanayoyataka.”
Kauli hiyo ya Rais imeitoa leo Septemba 13, 2021 jijini Dodoma wakati akiwaapisha mawaziri aliowateua jana akiwemo January Makamba ambaye amechukua nafasi ya Dk Kalemani.
Dk Ashatu Kijaji amemuapisha kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Dk Kijaji amechukua nafasi ya Dk Faustine Ndugulile huku Profesa Makame Mbarawa akiapishwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.
Prof Mbarawa anachukua nafasi ya Mhandisi Dk Leonard Chamuriho ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Dkt. Stergomena Tax ameapishwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa baada ya kifo cha Elias Kwandika.
Rais Samia baada ya kuwaapisha mawaziri hao Ikulu, Chamwino jijini humo amesema katika kipindi cha miezi sita tangu aingie madarakani aliwekeza muda katika kusoma utendaji wa mawaziri na viongozi wa Serikali.
Amesema wapo ambao wanafanya yanayowapendeza na kuacha majukumu yao na wengine waliendelea kufanya kazi kwa weledi.
“Katika miezi 6 ya urais wangu, nilikuwa mkimya na mtulivu nikisoma wizara zinavyoendeshwa. Wakati mimi nawasoma, na wao walinisoma. Kati yao walichukulia ukimya na utulivu wangu kama udhaifu wakaanza kufanya yanayowapendeza. Nilikuwa najifunza, nimeona,” amesema Rais.
Kutokana na usomaji wake, amesema kuna uwezekano mawaziri na viongozi wengine wakaondolewa katika nyadhifa zao hapo baadaye.
“Katika kipindi cha miezi sita kuna watu waliichukulia hiii serikali poa, serikali cool, watu wakafanya wanayoyataka… kutokana na jinsi nilivyoona utendaji wa mawaziri na viongozi wengine kwenye wizara, mabadiliko haya bado yatakuwa yanaendelea.
“Hapa nilipofika nimeweka koma, sijaweka nukta. Marekebisho haya (ya baraza la mawaziri) yanaendelea,” amesisitiza Rais.
Aidha, Rais Samaia amesema uteuzi wa mawaziri wapya haumaanishi kuwa ni wazuri kuliko wote waliokuweko bali uzuri wao utaonekana katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Kwangu mimi ninachotaka kuona ni matokeo sitaki kuwaona kwenye Tv tu mnafanya hili mnafanya lile. Nataka matokeo kwa wananchi,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Amewasisitiza mawaziri wapya aliowateua kutokusita kufanya marekebisho katika mambo yasiyofaa kwenye wizara zao kwa sababu anataka wafanye kazi kwa haraka na bidii.
Latest
