Rais Magufuli asema Uchaguzi Mkuu hautaihirishwa

Daniel Samson 0650Hrs   Machi 26, 2020 NuktaFakti
  • Asema licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa Corona, uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.
  • Aagiza shughuli za uzalishaji na uchumi ziendelee. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema shughuli za Serikali, Bunge zinaendelea kama kawaida na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kama ulivyopangwa utafanyika licha ya kuwepo mlipuko waugonjwa wa virusi vya Corona.

Ameagiza shughuli nyingine za uzalishaji na kiuchumi ziendelee wakati Serikali ikipambana kuthibiti maambukizi ya ugonjwa huo ambao ni janga la dunia.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo (Machi 26, 2020) Ikulu ya Chamwino, Dodoma wakati akipokea ripoti ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru). 

Amesema baadhi ya watu wanafikiri shughuli za Serikali na Bunge hazifanyiki na watendaji hawakutani kwa sababu ya Corona, huku akibainisha kuwa hata nchi ambazo zimeathirika sana na ugonjwa huo wabunge wao wanakutana.

“Sisi tunaendelea kukutana na ndiyo maana hata Bunge linaendelea na vikao vyake, hata huko kwenye nchi zilizoathirika kabisa, mamilioni ya watu wamekufa kwa Corona, bado mabunge yao yanakutana. Kazi lazima ziendelee…,” amesema Rais na kuongeza kuwa,

“Na uchaguzi tutafanya, wapo wanaofikiri kwamba tutaahirisha, nani anataka kukaa kwenye maofisi haya muda wote huo.”


Zinazohusiana


Aidha, amesema shughuli zote lazima ziendelee ikiwemo mikutano ya mabaraza ya madiwani na Bunge licha ya kuwepo kwa Corona. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mpaka kufikia jana Machi 25 watu 414,179 walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo huku 18,440 wakipoteza maisha duniani kote.  

Awali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amesema ofisi yake ilitoa mapendekezo 266 mwaka 2018/2019 lakini ni mapendekezo 82 pekee ndiyo yametekelezwa kikamilifu.

Amesema  mapendekezo 95 utekelezaji wake unaendelea, mapendekezo 65 hayajatekelezwa kabisa na mengine 22 yamepitwa na wakati.

“Hali ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na CAG hairidhidhi,” amesema CAG Kichere wakati akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Magufuli. 

Related Post